January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lutambi: Serikali ipunguze gharama za pembejeo kwa sekta ya elimu

Na Esther Macha, Timesmajira,Online,Mbarali

MKURUGENZI wa shule ya awali na msingi ya Kelly’s ya mchepuo wa kiingereza iliyopo kata ya Mapogoro wilayani Mbarali  ,Kennedy Lutambi ameiomba serikali kuona namna ya kupunguza gharama za pembejeo za kilimo,vifaa vya ujenzi ambavyo vimekuwa mwimba  kwa  wakulima na wawekezaji hususan katika sekta ya elimu katika uboreshwaji wa miundombinu ya vyumba vya madarasa.

Lutambi amesema hayo leo wakati akizungumza na timesmajira ofisini kwake kuhusiana upandaji wa uendeshaji wa shule hususani vifaa vya ujenzi  ambavyo vimekuwa na gharama kubwa kwa wakulima na wawekezaji wilayani humo ambao wanategemea kilimo kuendesha shule.

Aidha Mkurugenzi huyo amesema kuwa hali ni mbaya kwa wawekezaji wote si shule yake tu hivyo tunategemea kuona busara ya Serikali kwani tuna kundi kubwa la watoto zaidi ya 500 wanaopata elimu na wakisema wawerejesh nyumbani itakuwa mzigo mkubwa kwa Serikali na jamii kwa ujumla.
 

“Kwetu sisi athari ni kubwa na idadi kubwa hii watoto iliyopo  tunafikiri nambna ya kujiendesha  kwani idadi kubwa ya wanafunzi wanatoka katika jamii ya wakulima na wafugaji”amesema Mkurugenzi wa shuleya Kelly’s.

Akielezea zaidi Lutambi amesema uwekezaji alioweka katika shule hiyo umelenga jamii ya kipato cha chini na ndio  sababu  ya kutengeneza mifumo rahisi ya ulipwaji wa karo ya shule baada ya mavuno ili kuwaondoa  katika dhana ya kuona  umuhimu wa elimu kwa watoto.

Aidha amesema kuwa kufuatia uwepo wa gharama za vitu mbali mbali kumeongezeka ugumu wa gharama za uendeshaji wa shule ,hata biashara nyingi zimedorora  maisha kuwa magumu kutokana na mfumko wa bei za bidhaa.

“Sasa hivi wanaolima mazao ni wale wale tena wanaotoka mjini  tu zaidi wakulima wenyeji wanaishia  kukodisha tu mashamba yao kutokana na kushindwa kumudu gharama za pembejeo za kilimo”amesema Mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake Ofisa Kilimo Kata ya Mapogoro wilayani humo, Hebron Mwilwa amesema kuwa kuwa athari ya ukame imegusa maeneo mengi katika kata hiyo ambayo imetokana na mvua kuwa chache katika msimu huu wa kilimo.

Aidha amesema kuwa kuna Skimu tano za umwagiliaji ambazo zinatumika na vijiji tisa zimeathirika na ukame hali ambayo ni hatari kwa wakulima kwani idadi kubwa wanategemea  mikopo na uzalishaji kwa ajili ya  kusomesha watoto na mahitaji mengine.

“Kuna hekta 111 za mazao  za Mahindi, Mpunga na Alizeti zilizopo kwenye Skimu za kilimo cha  umwagiliaji kata ya Mapogoro Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya zimeathiriwa na ukame hali ni mbaya sana”amesema.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Kata ya Mapogoro , Francis Makombe amesema kuwa ukame huo umechangia changamoto ya  kuathiri uendeshaji wa sekta ya elimu kwa shule binafsi kutokana na asilimia kubwa ya wanafunzi wanaodaili kutoka jamii ya wakulima na wafugaji katika kujiendesha.

Amesema kuwa kutokana na hali hiyo wanaiomba Serikali kuona namna ya kuboresha Skimu za kilimo cha umwagiliaji kulingana na idadi ya wakulima ikiwa ni pamoja na kuwezeshwa kuvuna maji  katika mito mikubwa hususan Ruaha ili waweze kuzalisha katika misimu tofauti na kuepukana na hali ya ukame inayoweza kusababisha njaa.

Kwa upande Katibu wa Skimu ya Umwagiliaji ya Isenyela ,Samweli Ngeve ametaja  skimu za kilimo cha umwagiliaji  zilizoathirika ni pamoja na  Mbuyuni,Makengelewe,Isenyela ,Lyahamile na Msesule ambazo zinahudumia wakulima 11,023 katika vijiji tisa ambavyo vinategemea kilimo cha umwagiliaji.

Ngeve amesema kuwa hivi sasa katika mashamba hayo kuna foleni ya kumwagalia mashamba ambayo hata hivyo kutokana na maji kuwa machache kumekuwa kukitokea ugomvi kwa wakulima.

Ngeve ameomba serikali kuona hali hiyo  miundombinu sio mizuri kabisa na maji yaliyopo hayajitosherezi kutokana na hali hiyo kumekuwepo na migogoro ambayo inahatarisha usalama wa wakulima wenyewe kwa wenyewe .