December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lushoto DC yapitisha bajeti ya bilioni 52.2,2024/2025

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

HALMASHAURI ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga imependekeza bajeti ya zaidi ya bilioni 52.2 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali.

Bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 0.2 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2023/2024 ya bilioni 52.1na ongezeko hilo limetokana na ongezeko la makisio ya mapato ya ndani.

Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Victoria Chilewa akisoma bajeti ya 2024/2025 kwenye Baraza la Madiwani la Bajeti.

Fedha hizo kutoka Serikali Kuu ni mishahara ya watumishi (PE) zaidi ya bilioni 33.4,miradi ya maendeleo (ruzuku) zaidi ya bilioni 9 na matumizi ya kawaida (OC) zaidi ya bilioni 1.8 huku mapato ya ndani kwa mapato halisi (Own Source Proper) zaidi ya bilioni 1.8 na mapato lindwa zaidi ya 1 pamoja na wadau wa maendeleo (wahisani) zaidi ya bilioni 5.

Bajeti hiyo ilisomwa Februari 10, 2024 na Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Victoria Chilewa kwenye Baraza la Madiwani la Bajeti, ambapo madiwani wote waliridhia bajeti hiyo kwa kauli moja.

Ambapo ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto imekisia kukusanya zaidi ya bilioni 2.9 kutoka vyanzo vya ndani ambapo mapato halisi ni zaidi ya bilioni 1.8na mapato lindwa ni zaidi ya 1.

“Mapato haya yameongezeka kwa kiasi cha zaidi ya milioni 93.8 sawa na asilimia 3.3 ikilinganishwa na makisio ya mwaka 2023/2024 ya kiasi cha zaidi ya bilioni 2.7,” amesema Chilewa.

Chilewa alitaja maeneo ya kipaumbele ya bajeti hiyo ni uimarishaji wa mfumo na uwezo wa ukusanyaji wa mapato kwa kuongeza vifaa vya kielektroniki zikiwemo POS kwa ajili ya ukusanyaji na utunzaji wa takwimu sahihi za vyanzo vya mapato ya ndani pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato (defaulters) kwa kuziba mianya na kuchukua hatua stahiki.

Kuongeza wigo wa mapato kwa kupata takwimu sahihi za vyanzo vya mapato na kuibua vyanzo viipya vya mapato, kuimarisha Kamati ya Mapato na kufanya usimamizi na ufuatiliaji wa makusanyo ya mapato ya ndani kwa ushirikiano wa madiwani pamoja na Kamati ya Ulinzi ya Wilaya.

Pia kutoa huduma za ugani kwa wakulima katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao hatimaye kuongeza mapato kupitia ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.

Kwenye kuimarisha huduma za jamii afya na elimu, wana mpango wa kuimarisha miundombinu na upatikanaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na kuendelea na uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo vituo vya afya, zahanati na ukarabati wa Hospitali ya Wilaya, ambapo lengo ni kukamilisha ujenzi na usajili kwa zahanati zilizokamilika.

“Kuimarisha miundombinu ya shule za msingi na sekondari kama vile madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo, mabweni na bwalo, pamoja na ukarabati wa shule chakavu,kuongeza kiwango cha ufaulu kwa kutoa motisha kwa shule zilizofanya vizuri sambamba na kulenga muda wa ziada kwa wanafunzi wenye ufaulu wa chini,”ameeleza.

Sanjari na kuongeza idadi ya watumishi kwa kuendelea kuomba vibali vya ajira katika kada zenye uhitaji mkubwa ikiwemo elimu na afya ili kukidhi mahitaji ya utoaji huduma.

Uendelezaji wa shule shikizi ili ziendelee kusajiliwa na kuongeza idadi ya shule za msingi na sekondari, uanzishwaji wa shule ya mchepuo wa kingereza katika Jimbo la Lushoto na Jimbo la Mlalo.

Chilewa amesema pia watahamasisha wananchi kujiunga na iCHF ili kufikia huduma ya Bima ya Afya kwa wotena kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na kuendelea na utambuzi na utoaji wa huduma muhimu kwa makundi maalumu wazee na walemavu.

Amesema katika uimarishaji na ujenzi wa miundombinu na huduma za kiuchumi, wana mpango wa kuzijengea kaya uwezo wa kuzalisha na kuwepo kwa usalama wa chakula kupitia program mbalimbali kama uanzishaji wa mashamba darasa, ukarabati wa miundombinu ya mifugo ikiwemo majosho, minada na machinjio.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wakiwa kwenye kikao cha bajeti 2024/2025.

Ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji, kusaidia wakulima katika uendeleaji wa kilimo cha mkonge, pamba, tangawizi, kahawa na parachichi kwa ajili ya kukuza uchumi badala ya kutegemea zaidi mazao ya asili kama mahindi, maharage, mbogamboga na mpunga sambamba na kuendelea kufanya utafiti juu ya uanzishwaji wa mazao mapya mfano ngano na karafuu.

Pia wataboresha miundombinu ya masoko na magulio kwa kuwezesha ujenzi wa vyoo na vizimba ili kutoa huduma kwa hali ya usafi.