May 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lulida ataka viwanda vilivyofungwa vifufuliwe 

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

“Tusifumbie macho, tusifunge midomo viwanda vya nguo virejee Tanzania.”

Haya yalikuwa maneno ya Mbunge wa Kuteuliwa Riziki Lulida, wakati akichangia kwa msisitizo mkubwa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara, akitoa wito kwa Serikali  wa kufufuliwa kwa viwanda vya nguo nchini ambavyo kwa miongo kadhaa vimekuwa vikiteketea kimya kimya, huku Watanzania wakinyimwa ajira na fursa ya kuinua maisha yao.

Akichangia bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara Bungeni jijini Dodoma Leo Mei 14,2025,Lulida amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti ulioleta mageuzi makubwa katika sekta ya viwanda.

 “Leo hii, ukitaka kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Lindi, mpaka unamaliza Mkuranga, eneo lote ni la viwanda,” amesema. 

Amesema miaka ya nyuma Mkuranga ikionekana kama wilaya ya watu masikini lakini sasa inabadilika kwa kasi na kuwa kitovu cha uchumi na ajira.

Mbunge huyo alieleza pia ukuaji wa viwanda vya ndani kutoka Dar es Salaam hadi Kibaha na Chalinze, ambako viwanda na uwekezaji wa ndani vimeanza kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

 “Ajira zinapatikana, uchumi wa wananchi unakua, haya ndiyo maendeleo ya kweli,” amesema.

Amesema kamati ya Bunge ilipotembelea kiwanda cha Saadan Kigamboni, walishuhudia uzalishaji wa malori zaidi ya 1,000  hatua iliyowashangaza wengi kwani kwa muda mrefu magari yalikuwa yakiagizwa kutoka nje.

Alitaja  mafanikio mengine, ikiwemo uzalishaji wa marumaru za Mkiu zinazouzwa hadi Uganda, Kenya, Ruanda, na nchi nyingine za Afrika Mashariki, na kiwanda cha gypsum cha Knauf kilichopo Mkuranga kinachozalisha bidhaa bora zinazokubalika kimataifa.

Hata hivyo  pamoja na mafanikio hayo Lulida alieleza kusikitishwa na   kufungwa kwa viwanda 13 vya kotosho ambapo alivitaka baadhi kuwa ni pamoja na  Lindi, Mtama, Newala, Mtwara, Kibaha – ambavyo tangu mwaka 1997 havijafanya kazi, huku korosho zikiuzwa nje kama malighafi badala ya kuchakatwa nchini.

 “Kwa nini tunauza korosho ghafi wakati tuna uwezo wa kuzalisha bidhaa kamili?” alihoji kwa uchungu.

Ametumia nafasi hiyo kuitaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wale waliovichukua viwanda hivyo na kuviacha vife.

 “Waziri usione aibu,umepewa dhamana na Rais, na mbele ya Mwenyezi Mungu,unapaswa kusimama kwa ajili ya Watanzania masikini wanaoteseka kwa sababu ya ubinafsi wa wachache,” amesema kwa msisitizo.

MBUNGE huyo amesema,miongoni mwa viwanda vilivyoanguka ni pamoja na kiwanda kikubwa cha General Tyre kilichokuwa Arusha, kiwanda cha mafuta ya kula cha Okay, Tanbond na viwanda vya pamba vilivyokuwa na sifa kubwa hadi nje ya nchi. 

Mbunge huyo alisisitiza kuwa baadhi ya wafanyabiashara kwa makusudi walizima viwanda hivyo ili Tanzania iendelee kutegemea bidhaa kutoka nje  jambo ambalo halikubaliki tena katika enzi hii ya mabadiliko.

Aliikumbusha Serikali juu ya viwanda vya nguo vya Urafiki, Mutex, Mwatex, Sunguratex, na Keytex vilivyokuwa uti wa mgongo wa ajira za vijana nchini. 

“Huu ulikuwa ni mpango wa makusudi kudhoofisha uchumi wa nchi hii,walitaka tuvae nguo mbovu ya kuagiza kutoka nje,hali hii haikubaliki,” alisisitiza.

Aidha  Lulida ametoa wito kwa Waziri wa Viwanda na Biashara Jafo kuhakikisha viwanda vilivyofungwa vinafufuliwa mara moja.

 Alisisitiza kuwa kufungwa kwa viwanda ni kuua ndoto za maelfu ya Watanzania, na kwamba Bunge lote linapaswa kushirikiana kuikomboa sekta ya viwanda kwa maslahi ya Taifa.

“Tumefika mwisho wa uvumilivu, tunataka mabadiliko ya kweli ya viwanda ,  kwa ajili ya kumkomboa Mtanzania masikini.”