November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lukuvi awaonya watumishi wa Ardhi

Na Munir Shemweta, WANMM

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema watumishi wa sekta ya ardhi watakaohusika kwa namna moja ama nyingine kumilikisha kiwanja kimoja mara mbili (Double allocation) watachukuliwa hatua kali.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akisikiliza mgogoro wa mmoja wa wananchi aliyetembelea Banda la Wizara ya Ardhi katika Maonesho ya Sabasaba leo tarehe 7 Julai 2021.(Picha na Munir Shemweta-WANMM).

Ameyasema hayo leo Juni 7, 2021 baada ya kukagua shughuli za utendaji wa sekta ya ardhi kwenye banda la Wizara ya Ardhi katika maonesho ya biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.

Lukuvi amesema, ikibainika kuna umilikishaji mara mbili uliosababishwa na watumishi basi wote waliohusika kama ni afisa upimaji, upangaji na mmililishaji wote watachukuliwa hatua.

Amesema, awali sekta ya ardhi ilikuwa na migogoro mingi, lakini tangu mwaka 2015 kero nyingi za sekta hiyo hazipo ama zimepungua kwa kiasi kikubwa.

“Ni kweli huko nyuma tulikuwa na kero nyingi sana katika sekta ya ardhi na ninaamini tangu mwaka 2015 migogoro hakuna ama imepungua sana na nisisitize kama kuna utoaji hati mara mbili wote walioshiriki kuanzia wale wa kupima, kupanga na yule aliyemilikisha watachukuliwa hatua,”amesema Lukuvi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikagua fomu ya kuhifadhia Hati ya Kimila katika eneo la Chuo cha Ardhi Tabora kwenye Banda la Wizara ya Ardhi katika Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea viwanja vya Mwl Nyerere Dar es Salaam leo tarehe 7 Julai 2021.( Picha na Munir Shemweta-WANMM).

Kwa mujibu wa Lukuvi,Makamishna wa Ardhi Wasaidizi kwenye ofisi za ardhi za mikoa wanatakiwa kuhakikisha hakuna mgogoro mipya kwenye maeneo yao na kusisitiza kuwa ni marufuku ofisi hizo kushiriki ama kuchangia mgogoro wa ardhi.

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi amebainisha kuwa, kwa sasa wizara yake imeanza kubadilika ambapo uandaaji na utoaji hatimiliki za ardhi umetoka kwenye mfumo wa analogia kwenda digitali na kusisitiza kuwa hayo ni mageuzi makubwa.

Akielezea zaidi mfumo wa kidigitali, Waziri Lukuvi ambaye pia alikabidhi hati za kielektroniki za papo kwa hapo kwa baadhi ya wananchi waliotembelea banda la wizara alisema, mfumo huo umeasisiwa na vijana wazalendo wa Kitanzania na lengo lake ni kuzuia makosa ya kibinadamu na kuongeza kuwa, anaamini migogoro inayosababishwa na tamaa za kibinadamu za watumishi itapungua.

Waziri wa Ardhi pia ametembelea banda la Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC) na kusifu ubunifu wa shirika hilo katika ujenzi wa nyumba za kuuza na kupangisha mkoani Dodoma katika maeneo ya Iyumbu na Chamwino.

Hata hivyo, amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa kuhakikisha wananchi wanaolipa fedha kwa ajili ya kununua nyumba wanapatiwa nyumba hizo na kumilikishwa mara tu baada ya kulipa.