January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ludewa ilivyopania kupiga hatua kimaendeleo

Na David John, TimesMajira Online

LUDEWA ni miongoni mwa Wilaya kongwe hapa nchini, Wilaya hiyo inapatikana katika Mkoa wa Njombe huku ikipaka na mikoa ya Nyanda za juu Kusini. Wilaya ya Ludewa Kama zilivyo Wilaya nyingine, inahistoria yake, lakini pia inatamaduni zake mila na desturi kama ilivyo maeneo mengine.

Mbali na hivyo, Ludewa inamakabila mbalimbali madogo na makubwa ambayo yanapatikana wilayani humo wakiwemo Wamanda, Wapangwa napia na Wakisi kabila ambalo linapatikana pembezoni mwa Ziwa Nyasa.

Kwa mujibu wa wenyeji wa wilaya hiyo wanasema, wilaya hiyo inatamaduni zake mila na desturi zikiwemo Ngoma za kiutamaduni, pombe za kienyeji ambapo mara nyingi wananchi wakitoka kwenye shughuli zao za kilimo huketi pamoja na kupata kiburudisho.

Hata hivyo, ngoma yao kuu ya Kiutamdauni ni Mganda ambayo huchezwa zaidi na kabila la Wamanda na Wakisi kutoka pembezoni kabisa mwa ziwa nyasa.

Pia kuna Ngoma aina ya lindeku ambayo yenyewe wababa na wamama upenda kucheza katika sherehe mbalimbali hasa katika nyakati za msimu baada ya mavuno au shughuli za kisiasa.

Shughuli kubwa za uzalishaji zinazofanywa na wananchi wa Ludewa ni kilimo na uvuvi, lakini kuna rasilimali zingine kama vile Mali asili yakiwemo madini ya aina mbalimbali ambayo bado hayajaaza kuleta matunda kwa wananchi husika.

Kuhusu kilimo wananchi wanalima Mazao mchanganyiko kama vile Maharagwe, Chai, Mahindi pamoja na Mihogo hususani pembezoni mwa ziwa nyasa.

Lakin zao kubwa la Chakula katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa ni Mahindi huku zao la biashara likiwa Mahindi pamoja na Maharagwe licha ya kuwepo kwa mazao mengine mchanganyiko.

Mbali na kuwa na shughuli mbalimbali za uzalishaji, lakini Wilaya ya Ludewa kama ilivyo maeneo mengine lina Jimbo la uchaguzi ambapo tangu kuazishwa kwake wamepita viongozi mbalimbali .

Mwaka 1965 hadi mwaka 1970 alipita Mbunge wa jimbo hilo alikuwa Violet Baraka, mwaka 1970 hadi 1980 alipita Petrosimalenga lakini kuazia 1980 hadi 1995 alikuwa Mathias Kihaule .

Viongozi wengine ambao wamefanikiwa kuwa wawakilishi wa wananchi ni Horace Kolimba mwaka 1995 hadi 1996, kwa maana alidumu kwa muda wa mwaka mmoja na baadae kufariki dunia. Lakini mwaka 1996 hadi 2002 alikuwa Profesa Chrispin Haule.

Kuazia mwaka 2002 hadi 2005 alikuwa Stanley Kolimba ambaye alidumu Kwa miaka mitatu na ilipofika mwaka 2005 hadi 2010 alikuwa Profesa Raphael Mwalyosi, kuazia 2010 hadi 2015 alikuwa Deo Filikunjombe na kuazia 2015 hadi 2010 Mbunge wa Jimbo la Ludewa alikuwa Deo Ngalawa

Kwa sasa Jimbo hilo lipo Chini ya wakili Joseph Kamonga ambaye licha ya waliomtangulia wamefanya kazi kubwa ya kuijenga Wilaya hiyo lakini kuna mambo mbalimbali anapaswa kuyatekeleza kuhakikisha Ludewa inapiga hatua katika maendeleo.

Wananchi wa Wilaya hiyo, kwa nyakati tofauti wameonyeshwa kukerwa na tabia ya mabadilko ya wabunge kila miaka ya uchaguzi inapofika. Mbunge wa Sasa Joseph Kamonga akiwa katika Kampeni zake za uchaguzi wa mwaka huu, wananchi walionesha imani kubwa kwake huku wakisema wanatamani kuona Mbunge huyo anakuwa Mbunge wa kudumu katika Jimbo hilo.

Mara zote walikuwa wanamkumbusha makosa ambayo yalikuwa yanafanywa na watangulizi wake hasa kushindwa kuwatumikia wananchi ipasavyo huku wengi wao wakipoteza muda mwingi kukaa nje ya Jimbo.

Wananchi hao kubwa ambalo walikuwa wanalitaka kutoka kwa Mbunge huyoni kuwasemeya bungeni lakini pia kutatua kero za vijiji kama vile kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii.

Mbunge huyo mteule wa Jimbo la Ludewa wakili Joseph Kamonga anasema, anatambua kazi kubwa zilizofanywa na watangulizi wake na yeye atajitahidi kuendeleza mazuri yote yaliyo mbele yake.

Kamonga anasema, Jimbo la Ludewa lina rasilimali za kutosha lakini kwa bahati mbaya Wilaya hiyo imesahaulika licha ya jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali kwa kuijenga Ludewa.

Anasema, anatambua wananchi wa Ludewa wengi wao ni wakulima na Uvuvi huku vipato vyao ni vya kawaida lakini wanachangia kipato cha halmashauri kwa maana kukusanya kodi na mambo mengine.

Kamonga anasema, kuna haja sasa kuangalia upya fursa zingine za kupandisha mapato kwenye halmashauri hiyo na kwa bahati nzuri Wilaya ya Ludewa ina madini ya kutosha.

Anasema, katika kipindi chake cha ubunge kazi iliyombele yake ni kuishawishi Serikali kuona umuhimu Sasa wa kufanya uwekezaje mkubwa katika sekta ya madini wilayani humo.

“Mnajua Wilaya ya Ludewa ina mali nyingi hasa madini, hivyo kazi niliyonayo nikuona madini haya yananufaisha wananchi wa Ludewa lakini kubwa ni kuiomba Serikali kutuletea uwekezaji mkubwa ili ikiwezekana Ludewa pajengwe viwanda vya Chuma Kwa sababu madini ya Chuma yanapatikana hapa, “anasema Kamonga.

Nakuongeza kuwa ” Moja ya madini ambayo yapo ni madini ya Chuma ambayo yapo Liganga na Mchuchuma, pia kuna madini ya Makaa ya nawe ambayo yanatumika kuzalisha Sement pamoja na madini ya chokaa.

Anasema, kutokana na uwepo wa madini hayo na mengine mengi anaiomba Serikali hususani kupitia Waziri wa madini Dotto Biteko kuipa kipaumbele wilaya hiyo ili wananchi wa Ludewa waweze kunufaika na rasilimali zao.

Anasema kuwa kujengwa Kwa viwanda wilayani humo kutawezesha kuinua kipato cha halmashauri kwasababu itakuwa inakusanya mapato lakini wananchi watapata ajira kutokana na kuwepo kwa viwanda hivyo

Kamonga anasema, amejipanga vizuri na kikubwa anaomba ushirikiano mkubwa kwa wananchi, Madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri ili kwa pamoja waweze kuijenga Ludewa yao.

Anasema, anajua Ludewa bado kuna changamoto za miundombinu, huduma za Afya, lakini pia kwenye sekta ya elimu bado kuna tatizo hususani upungufu wa watumishi, lakini pia kuna baadhi ya maeneo changamoto ya maji na mambo mengine.

Amewataka wananchi wajimbo la Ludewa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali hasa Chini ya Rais Dkt. John Magufuli ambaye anania ya dhati ya kuivusha Tanzania na katika hilo, leo hii nchi imeingia uchumi wa Kati.