Na Nasra Bakari, TimesMajira Online
WIZARA ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Shirika la Legal Services Facility (LSF) wamezindua kongamano la siku mbili la msaada wa kisheria lililoanzishwa tarehe 30-31 Machi 2022.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma wakati wa tukio la uzinduzi wa kongamano hilo, Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene alisema, kongamano hilo ni sehemu muhimu itakayowaleta pamoja wadau wa sekta ya msaada wa kisheria nchini ili kujadili utekelezaji wake na namna ya kuboresha zaidi ili kuleta ufanisi mzuri.
Alisema, Kongamamo hilo lenye kauli mbiu inayosema kuwa, “Msaada wa Sheria kwa Jamii yenye Haki na Jumuishi” linalenga kuangazia utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya Mwaka 2017 kwa kuangalia mafanikio na changamoto ya utekelezaji wa sheria hiyo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Aidha, kongamano hilo litaendesha mijadala mbalimbali yenye lengo la kubadilishana uzoefu miongoni mwa wadau wa sekta ya msaada wa kisheria nchini ili kujenga mifumo na taasisi imara na endelevu ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria na kuwezesha upatikanaji wa haki nchini Tanzania.
“Halikadhalika, kongamano hilo linafanyika sambamba na maonyesho ya wazi kutoka kwa watoa huduma za msaada wa kisheria waliokaa pamoja (one-stop centre) ili kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa watu mbalimbali wanaotembelea maonyesho hayo,” alisema.
Waziri huyo alisema, huduma za msaada wa kisheria kupitia kituo cha pamoja (one-stop centre) zinatolewa bure chini ya dawati la kijinsia la polisi, wasaidizi wa kisheria (paralegals), wanasheria kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) na Maofisa ustawi wa jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii nchini Tanzania, Sambamba na huduma za wanawake wajasiriamali wanaonyesha na kuuza bidhaa zao ikiwa ni hatua mojawapo ya shughuli za uwezeshaji.
Alisema, Kabla ya kutungwa na kupitishwa kwa Sheria ya Msaada ya Mwaka 2017, wadau wa sekta hii hasa watoa huduma na wasaidizi wa kisheria walikuwa wakikumbana na changamoto nyingi kubwa ikiwa ni kutokutambuliwa katika taasisi mbalimbali za mifumo ya utoaji haki, Tunatarajia kusikia uzoefu wa wadau hawa na wengine baada ya sheria hii kuanza kutekelezwa
Waziri huyo ameongeza kuwa, kongamano hilo linalenga kupata uzoefu wa utekelezaji sheria za msaada wa kisheria kwa kuangalia maeneo mengine ya nchi jirani kama vile Kenya, Uganda na Malawi huku lengo kuu likiwa ni kupata uzoefu na kujifunza kutoka kwa kila mmoja namna bora ya kukuza sekta hii muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu kutoka Shirika la Legal Services Facility, Lulu Ng’wanakilala alisema, kongamano la mwaka huu ni sehemu kubwa ya mafanikio ambayo LSF inajivua kwa kushirikiana na wadau wengine hasa serikali katika kuwezesha upatikanaji wa haki.
Ng’wanakilala alisema, kongamano hilo ni muhimu sana katika kuinua sekta ya huduma za msaada wa kisheria kwani litatusaidia kufahamu kwa undani mafanikio, changamoto na fursa ya kukutoka na maazimio ambayo yataboresha upatikanaji wa haki nchini kwa ujumla hivyo tunafurahi sana kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria katika kuliandaa.
“Tangu mwanzo LSF imekuwa mdau mkuu wa serikali katika kuhakikisha tunaendelea kufanya kazi kwa karibu katika kuwezesha upatikanaji wa haki ikiwemo kuchangia katika kuwezesha sheria ya msaada wa kisheria nchini Tanzania inapatikana. LSF kama shirika lisilo la kiserikali tumekuwa tukifanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kupitia uwezeshaji wa kisheria. Uwepo wa sheria hii umekuwa nyenzo muhimu kwetu katika kuongeza upatikanaji wa haki kupitia wadau wetu wakubwa ambao wamekuwa wakitoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria kwa watu wote hasa wanawake na wasichana” alisema Afisa huyo.
Nae Msajili wa Msaada wa Kisheria, Felistas Mushi alisema, katika kipindi cha miaka mitano changamoto kubwa imekuwa ada ya usajili wa wasaidizi wa kisheria lakini hata hivyo serikali imeamua kufuta ada hiyo ili kuruhusu wasaidizi wa kisheria kujisajili kwa wingi zaidi.
Alisema, Mpaka sasa tuna wasaidizi wa kisheria 757 ambao wamejisajili katika mfumo wa serikali kama watoa huduma za msaada wa kisheria,Vilevile tuna mashirika 202 tu ya wasaidizi wa kisheria yaliyosajiliwa baada ya kukidhi vigezo, Kuanzia mwezi wa pili ada hizo ambazo zilionekana ni kikwazo zimefutwa kabisa.
“Leo pia kulifanyika uzinduzi wa ripoti maalumu ya Wadau wa Upatikanaji Haki nchini Tanzania (LSF Access to Justice Stakeholders Mapping Report). Meneja Programu wa LSF, Deogratias Bwire alizungumzia ripoti hiyo ambayo imezinduliwa na Waziri Simbachawene jana alisema, kuna zaidi ya wadau 30 kwenye sekta ya msaada wa kisheria ambao wana umuhimu mkubwa katika kuhakikisha haki za wananchi zinafikiwa. Wadau hawa wameonekana wana umhimu katika kuboresha na kuunganisha nguvu katika upatikanaji wa haki nchini alisema.
“LSF tumefanya utafiti na kuja na ripoti hii muhimu kwa wadau wa upatikanaji wa haki nchini. Ripoti imebainisha ya kuwa miongoni mwa wadau wakubwa katika utoaji huduma za msaada wa kisheria ni wasaidizi wa kisheria, mahakama, polisi, viongozi wa serikali, viongozi wa dini bila kusahau viongozi wa kimila,Ripoti hii inaonyesha kama wadau wote wataunganisha nguvu ya pamoja kuna uwezekano mkubwa wa kuboresha zaidi upatikanaji wa haki kwa wananchi,” alisema Wakili Bwire
John Nginga ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Msaada wa Kisheria Wilaya ya Tunduru na ni mdau wa sekta ya msaada wa kisheria nchini alisema, sekta ya msaada wa kisheria kwa kushirikiana na serikali imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha mfumo wa utoaji haki kupitia huduma za msaada wa sheria inawekewa mazingira mazuri kwa kutungiwa sheria ambayo imesimamia vyema kwa miaka hii mitano iliyopita.
“Serikali pamoja na Asasi za kiraia nchini tulifanya kazi kubwa kuhakikisha sheria hii inakuwepo. Kupitia kongamano hili, ni matumaini wadau watajadili vyema na kutoa michango bora yenye lengo la kuboresha sekta hiyo kupitia utekelezaji wa sheria.” alisema Nginga
Alisema kongamano hili limewaleta pamoja Taasisi za Serikali, Asasi zisizo za kiserikali (CSO) ,Wadau wa maendeleo na wadau mbalimbali takribani 120 wanaojihusisha na utoaji wa msaada wa sheria kutoka Tanzania bara na Zanzibar, kujadili na kutathmini utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Sheria ya Mwaka 2017
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato