Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
LSF kwa kushirikiana na S4C wamezindua jezi mpya kwa ajili ya mbio za ‘Run for Binti Marathon 2023 zenye lengo la kukusanya rasilimali fedha kwa ajili ya kuwezesha watoto wa kike kupata taulo za kike ili kuboresha upatikanaji wa haki ya afya ya uzazi hususani hedhi salama na safi pamoja na kuboresha mazingira bora na rafiki katika sekta ya elimu kwa mtoto wa kike yatakayomuwezesha kupata hedhi iliyo salama kupitia ujenzi wa miundombinu bora hususani vyoo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa jezi hizo, Mkurugenzi Mkuu wa S4C, Flora Njelekela amesema Mbio hizo zinafanyika kwa mara ya tatu (3) hapa nchini, chini ya usimamizi na uratibu wa LSF na S4C, ambapo takribani washiriki 1,500 watakimbia.
Amesema Mbio hizo sasa zitafanyika mnamo tarehe 30 Julai 2023 badala ya tarehe 02 Julai 2023 kama ilivyokuwa imepangwa awali. Mabadiliko haya ya tarehe yanalenga kuboresha zaidi maandalizi ya mbio hizi na kuhamasisha ushiriki mkubwa.
“Mabadiliko ya terehe yamekuja kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mrejesho wa wadau mbalimbali wanaotaka kuwa sehemu ya tukio hili la hisani. Tunaamini kuwa kusogeza mbele kwa tarehe za mbio hizi mpaka tarehe 30 Julai 2023 itawezesha kujenga mazingira rafiki zaidi kwa washiriki mbalimbali kujiandaa kwa tukio hili la kijamii ambalo pia ni muhimu kwa utimamu wa mwili na afya kwa aujumla.”
“Mikoa itakayonufaika na mbio hizi ni Mtwara na Lindi, ambapo watoto wa kike kwenye shule za sekondari watanufaika kwa kupatiwa bidhaa za hedhi salama, uboreshwaji wa miundo mbinu hususani vyoo salama. Sambamba na hilo vikundi vya wanawake vya kiuchumi katika ngazi ya jamii vitawezesha kwa kupatiwa mashine na vitambaa maalumu vitakavyowawezesha kushona sodo (taulo za kike) na kuziuza kwa bei nafuu kwenye shule mbalimbali na hivyo kujiinua kichumi.
“Njelekela amewashukuru wadau wote kwa kuunga mkono mbio hizi kupitia uwezeshaji wao pamoja na kujitolea kwa hali na mali ili kuchangia matokeo chanya katika jamii.Kwa upande wake Meneja Rasilimali na Mawasiliano kutoka LSF, Jane Matinde amewashukuru pia wadau ambao wameweza kuona umuhimu wa mbio hizo na kuweza kujitolea ili kuendelea kufanikisha tukio hilo la kijamii.
“Naomba tujumike pamoja kama jamii na tuhamasishe wengine na tuonyeshe nguvu ya pamoja katika kujitolea. Kwa michango yenu tunaweza kuleta matokeo chanya kwa mustakabali wa watoto wa kike nchini. Tukielekea tarehe 30 Julai 2023 nawaomba wadau wote kushiriki mbio hizi kwa ajili ya kumuinua mtoto wa kike,” amesema Jane Matinde.
More Stories
Watumishi wa Mahakama waonywa
CCM ilivyotambua mchango wa wanahabari Mkutano Mkuu Maalum
Wasira :Uamuzi Mkutano Mkuu umezingatia katiba