Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Wanawake wa kimasai wamekabidhiwa hundi ya pesa ya Kitanzania shilingi Milioni Ishirini na Mbili (22,000,000/=), itakayokwenda Kwa vikundi 11 vya wanawake kutoka kata ya Kimokouwa kama mtaji wa kuanzia.
Pia cherehani 11 zitakazotumika kutengenezea taulo za kike kwa ajili ya wasichana 1412 katika shule za Namanga sekondari na Lekule sekondari zilizoko Longido Arusha.
Uwezeshaji huo umefanywa na Shirika la Legal Services Facility (LSF) na Taasisi ya North – South Cooperation ambapo pia wamewawezesha wanawake 8 ambao ni wawakilishi wa vikundi vya wanawake katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi cha Mariale kwa ajili ya kupata ujuzi wa ushonaji nguo, mafunzo hayo yatafanyika kwa muda wa mwezi mmoja.
Akizungumza wakati wa hafla fupi iliyofanyika Longido, Mkoani Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa LSF imeamua kutekeleza mradi wa “Wanawake Tunaweza” kwa kushirikiana na wadau wengine ili kusaidia jamii ya kimasai hususani wanawake na watoto wa kike, ambao wamekuwa nyuma katika hatua za maamuzi, umiliki wa rasilimali ikiwemo ardhi na mifugo, pamoja na fursa sawa ya kwenda shule.
“Jamii ya kimasai ni ya kipekee nchini Tanzania kutokana na udumishaji wa mila na desturi zake kwa kipindi kirefu. Uchumi wa jamii ya kimasai unategemea zaidi shughuli za ufugaji kwa asilimia 85 ya shughuli zote za kiuchumi zinazoendeshwa na jamii hii. Njia kuu za uchumi pamoja na uzalishaji mali kwa jamii ya kimasai zinamilikiwa na kuendeshwa na wanaume, hali inayosababisha haki za wanawake na wasichana wa kimasai kukiukwa. Kuanzishwa mradi huu hapa Longido kutawezesha kutatua baadhi ya changamoto hizi na kuwawezesha wanawake wa kimasai kijamii na kiuchumi,” ameeleza Lulu Ng’wanakilala.
Sambamba na kuwawezesha wanawake kiuchumi LSF imezundua ujenzi wa Mabweni mawili ya Wasichana, ambapo bweni moja litakuwa katika Shule ya sekondari ya Wasichana ya Lekuke ujenzi wake utagharimu kiasi cha shilingi Milioni Mia Moja Arobaini za Kitanzania (140,000,000/=), na ujenzi mwingine wa Bweni utafanyika katika shule ya sekondari Namanga utakaogharimu kiasi cha Shilingi Milioni Mia Moja Ishirini za Kitanzania (120,000,000/=) ambapo kwa pamoja Ujenzi wa Mabweni yote mawili utagharimu kiasi cha Shilingi Milioni Mia Mbili na Sitini za Kitanzania (260,000,000/=).
Akitoa salamu fupi kwa niaba ya North- South Cooperation Mratibu wa Mradi, Roberto Marta ameeleza kufurahishwa kwake kutokana na matokeo chanya ya mradi wa “Wanawake Tunaweza” kadri siku zinavyozidi kusogea ambapo ameeleza kuwa ushirikiano wao na Shirika la LSF umekuja kutokana na uhitaji uliokuwepo wa kugusa maisha ya wakazi wa jamii ya kimasai.
“ Mradi huu tunaoutekeleza na LSF ni moja kati ya miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Luxembourg ambayo imejikita katika kujenga usawa wa Kijinsia na kukuza hali ya Maisha ya watu kwenye eneo la uchumi wao lakini pia kuhakikisha Ajenda ya mwaka 2030 inafikiwa ikiwemo kugusa na kusaidia makundi maalumu na hapa tunawasaidia zaidi Wanawake alieleza Ndugu Marta ”.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Longido Dominic Ruhamvya amewapongeza LSF pamoja na wadau wa maendeleo kutoka Luxembourg kwa kuona vyema na kuamua kushirikiana kutekeleza mradi huu na kuongeza kwamba, ujenzi wa mabweni ya watoto wa kike katika shule za sekondari za Lekule na Namanga utawezesha kutatua changamoto ya watoto kubanana na kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu utakaochochea ufaulu wa wanafunzi kuongezeka.
Aidha, amesisitiza kuwa kuviongezea nguvu vikundi hivi vya kina mama kutawaongezea nguvu ya kupambana na shughuli za uzalishaji na kuwainua kiuchumi, kutoa huduma bora na malezi kwa wototo na kukuza ustawi wa jamii nzima kwa ujumla.
‘Wanawake Tunaweza’ ni mradi unaotekelezwa wilayani Longido mkoani Arusha kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake na jamii ya kimasai nchini katika nyanja ya kiuchumi na kijamii.
Mradi huu umelenga kufanya kazi na wanawake kwa kupitia vikundi vya wanawake kwa kuwajengea uwezo katika masuala ya kibiashara na ujasiriamali, pamoja na kuwawezesha kupata soko la bidhaa mbalimbali watakazozizalisha. Aidha mradi huu pia unawawezesha watoto wa kike kupata elimu bora kwa kuwezesha ujenzi wa majengo.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam