March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Londo:TanTrade  mdau mkubwa katika kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini

Na Mwandishi wetu,Timesmajira 

Naibu Waziri wa Wizara ya Biashara na Viwanda, Dennis Londo, ameitaja Mamlaka ya Manedeleo ya Biashara (TanTrade),kuwa mdau muhimu katika kukuza maonesho ya biashara na kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipotembelea Mamlaka hiyo na kuzungumza na Menejimenti ya Tantrade, Londo amesema kuna viwanda vingi nchini  vinavyozalisha bidhaa bora ambazo Watanzania wengi hawajui kuwa ni za ndani.

“Tutasimama bega kwa bega na TanTrade kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinatambulika kitaifa na kimataifa. Wazalishaji wadogo wapate fursa ya bidhaa zao kujulikana, na zinapopenya kwenye masoko ya kimataifa zitambulike wazi kuwa zimetoka Tanzania,” amesema.

Amesema  TanTrade inajukumu la kukuza miundombinu ya maonesho ya biashara kwa kutangaza bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi ambazo  watanzania hawazijui.

Amesema ni vema kuboresha miundombinu hiyo ili watanzania kujua viwanda vilivyopo nchini ambavyo vinazalisha bidhaa mbalimbali.

” Matumaini yangu ni kuona nembo ya Made in Tanzania  itaenda kusaidia watanzania kuona na kujua bidhaa zinazozalishwa nchini.

”Matamanio na matarajio yangu kwamba watanzania watatanguliza mbele uzalendo wa kununua vya kwao,nawapongeza sana Tantrade kwa kubeba Tanzania katika maonesho mbalimbali ambapo mwaka jana tulishiriki nchini Iran,katika maonesho makubwa ya biashara na tuliona dhana ya biashara,”amesema

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, amesema kuwa katika utekelezaji wa Ilani ya Mwaka 2020–2025, wameweza kuunganisha kampuni 1,065 za Kitanzania na masoko ya kimataifa. Pia, kupitia programu za mafunzo, vijana na wanawake 14,045 wamejengewa uwezo wa kuendesha biashara kwa ushindani.

Amesema kupitia matukio ya kukuza biashara yanayoratibiwa na TanTrade, jumla ya mikataba 36 yenye thamani ya shilingi trilioni 17.35 ilisainiwa kwenye Expo 2020 Dubai, mikataba 8 yenye thamani ya shilingi bilioni 38 kwenye Expo 2025 Osaka – Japan, na mikataba 10 yenye thamani ya shilingi bilioni 176 ilisainiwa katika maonesho ya DITF Sabasaba.