November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LJF yazindua mradi wa uendeshaji wa bajaji kwa wanawake

Na Mwandishi wetu, timesmajira

Shirika la Ladies Joint Forum (LJF)lazindua mradi wa She Drives to Change wenye lengo la kuwawezesha wanawake takribani 30 waliopo katika kundi la wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia,akinamama vijana ,wanawake wanaoishi na ulemavu na akina mama wanaolea watoto wenye ulemavu pekee yao katika malezi duni kupata ujuzi wa kina katika udereva wa bajaji.

Akizungumza hayo jana jijini Dar es Salaam ,Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ladies Joint Forum, Francisca Mboya wakati wa uzinduzi wa mradi mpya unaoendeshwa na shirika hilo wa She Drives to Change unaolenga kuwagusa wanawake wa makundi hayo alisema kutokana na changamoto mbalimbali wanzaokumbana nazo wanawake wa makundi hayo wameona ni vema kuhakikisha wanakuja na mradi utakaoweza kuwasaidia.

Amesema mradi wao ni wa miezi 12 unalenga kuwawezesha na kukuza uhuru wa kiuchumi wawanawake hao 30 wenye umri wa miaka kati ya 18 hadi 40 katika kata ya vingunguti wilayani ilala.

”She Drive to Change unaangazia kuwapa fursa wanawake hao kushiriki katika kuendesha bajaji na kufanya waweze kukuza uhuru wa kiuchumi ,usawa na uwezeshaji wa wanawake katika jamii,”amesema na kuongeza

”Mradi unalenga kutengeneza fursa za ajira kwa kuwapatia wasichana na wanawake walio katika mazingira magumu ujuzi wa kina unaowawezesha kujihusisha na udereva wa bajaji,kuweka mazingira shirikishi na kusaidia wasichana na wanawake walio katika mazingira magumu kujihusisha na udereva wa bajaji wa kitaalamu,”amesema.

Amesema pia taasisi hiyo inalenga kuanzisha mtandao wa madereva wa bajaji wanawake ambao wanatetea haki za wanawake ,usawa wa kijinsia na wasimamizi wa tamaduni za kijamii na wanaopinga aina zote za unyanyasaji dhidi ya wanawake.

Amesema wanaamini kuwa ujuzi ndio utakaomkomboa mwanamke kifikra hata kiuchumi na kumfanya ustawi wake kuwa imara.

Kwa Upande wake Afisa Maendeleo Kata ya Vingunguti Dominica Balama amesema katika kata yao inawatu wa kipato cha chini waliowengi hivyo mradi huu utaweza kuwasaidia wanawake wengi ambao wanalea familia pekee yao wakiwemo wakinamama wanaolewa watoto wenye ulemavu.

”Mradi huu utasaidia kuwainua wanawake wasichana ambao wanaowalea watoto wenye ulemavu ukizingatia wengi wanakimbiwa na wanaume zao pindi wanapojifungua,”amesema.

Naye Mmoja wa mnufaika wa mradi She hero kutoka JLF, Kijakazi Ibrahimu alisema miradi kama hii imekuwa ikiwasaidia wasichana wengi katika jamii katika kupiga hatua kwenye shughuli zao za kujiingizia kipato.