November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lissu hatarini kushitakiwa Kwa uongo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wanasiasa waliosambaza taarifa za uongo kupitia mikutano yao, wakidanganya kwamba kampuni ya Uwekezaji kwenye utalii na ranchi za wanyama, Mwiba Holdings Ltd (na mmiliki wake Thomas Dan Friedkin) imepewa umiliki wa ekari milioni 6 za eneo la hifadhi ya wanyama wilayani Meatu mkoani Simiyu, wametishiwa kuchukuliwa hatua Kali za kisheria.

Kupitia mikutano ya hadhara ya kisiasa inayoendelea huko Kanda ya Ziwa, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, amenukuliwa akitoa tuhuma hizo, ambazo sasa zimeelezwa kuwa uongo mtupu.

Katika taarifa yake kwa umma, Mwiba Holdings Ltd imesema haimiliki ardhi yoyote kwenye maeneo ya hifadhi nchini Tanzania na kwamba wilayani Meatu kampuni hii inafanya kazi kwa mikataba ya uwekezaji na upangishaji ambayo imeingia na Halamshauri za Vijiji ambazo ndizo zinazomiliki maeneo hayo. Jumla ya maeneo yote haya yaliyopangishwa ni ekari 171,604 – na si ekari milioni 6 kama ambavyo Lissu amekua akidai.

Kwa mujibu wa takwimu za Mkoa wa Simiyu, mkoa mzima una eneo la kilomita za mraba 23,807 sawa na takribani ekari milioni 2.4. Eneo la Wilaya ya Meatu lililoko kwenye hifadhi ni kilomita za mraba takribani 4,253 sawa na ekari 425,000.

Kwa takwimu hizi, ina maana maelezo ya Lissu yanamaanisha Mwiba imepewa eneo ambalo ni mara 14 ya eneo lote la hifadhi wilayani Meatu, na mara tatu ya ukubwa wa mkoa wote wa Simiyu – jambo ambalo linaonyesha dhahiri taarifa hizi si sahihi.

Aidha, kampuni hiyo (Mwiba Holdings) imeeleza kwamba haijaingia mkataba wowote na Serikali ya Awamu ya Sita kama inavyoelezwa na wapotoshaji, bali mikataba yake ya upangaji na uwekezaji kwenye maeneo haya imekuwepo kwa muda mrefu na iliongezewa muda mwaka 2018 na 2019 wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.