December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tundu Liss

Lissu ‘atinga’ ofisi ya RPC Dodoma kuchukua gari lake

Lissu atinga ofisi ya RPC
Dodoma kuchukua gari lake

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu, amefika kwenye Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuchukua gari lake ambalo limehifadhiwa na Jeshi la Polisi Mkoa huo tangu aliposhambuliwa na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka 2017.

Lissu ameenda ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma leo akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Salum Mwalimu na alipokelewa na Kamanda wa mkoa huo, SACP Giles Muroto.

Katika mazungumzo yake na SACP Muroto, Lissu amesema ameamua kwenda yeye mwenyewe baada ya utaratibu wa kulipata hilo kwa njia zingine kushindikana.

Kwa upande wake, SACP Muroto amemweleza Lissu kwamba Jeshi la Polisi mkoani hapo linahitaji muda zaidi ili kujiandaa kulikabidhi gari hilo kwake.

Aidha, SACP Muroto amemweleza Lissu kwamba Jeshi la Polisi linamhitaji atoe maelezo kwa Jeshi la Polisi kuhusu kushambuliwa kwake Septemba 7, 2017.

Lissu amejibu kwamba yeye yuko tayari kutoa maelezo polisi kwa tarehe na muda utakaokuwa muafaka kwa pande zote mbili. Lissu amesisitiza mshangao wake kwamba hadi sasa ni takriban miaka mitatu tangu kushambuliwa kwake, akidai Jeshi la Polisi halijafanya uchunguzi wowote, ikiwemo kumhoji yeye na dereva wake Adam Bakari Mohamed, licha ya kuahidi kwamba lingefanya hivyo akiwa hospitalini nchini Kenya.