December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afya bora ya mtoto msingi mzuri wa ukuaji wake

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZAZI wametakiwa kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa ili kuhakikisha ubongo wao hauathiriwi na magonjwa hali ambayo itaathiri ukuaji wao kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya inayojishughulisha na masuala ya utoaji wa elimu kuhusu masuala ya lishe (ANUE) Mengo Chikoma ambaye pia taasisi yake inashirikiana na timu ya Mkoa wa Dodoma katika utekelezaji wa Mradi wa Mtoto Kwanza unaopelekea mafanikio ya utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM-2021/22-2025/26).

Amesema,moja ya mambo ya kuzingatia kwa mtoto  ili awe  na afya bora na bila kuathiriwa na magonjwa mzazi anapaswa kuhakikisha pamoja na mambo mengine mtoto anapata lishe ya kutosha.

“Na kwa kuzingatia suala la malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto haswa wenye umri wa miaka sifuri mpaka nane kwa ajili kuhakikisha ukuaji wake,huwa tunatoa  elimu kwa kina mama kwa kuzingatia chakula cha kuwapa ili kuwakinga na magonjwa pia tunatoa elimu ya lishe ya mama mjamzito ili kumnusuru mtoto atakayezaliwa , na tunatoa elimu hiyo kupita kwenye vituo vya afya na kuongea na jamii.

Daktari Bingwa wa Watoto hosptali ya Mkoa wa Dodoma Halima Kassim amesema,mtoto anaweza kupata magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe ya kutosha tangu akiwa tumboni na mama yake kwa kupungukiwa damu tangu akiwa tumboni kwa mama yake mpaka anapozaliwa.

“Upungufu huu wa damu unaweza kupoteza uhai wake kwani mtoto anapozaliwa anakuwa amebeba akiba ya madini ya chuma ambayo ni stoo ya damu kwa mtoto ,hiyo inafanya hata mama akiwa hana damu ya kutosha pia inaweza kumpelekea mtoto kutokuwa na damu ya kutosha hivyo kutokuwa na akiba yoyote na hivyo kuhatarisha uhai wake kama hatapata matibabu mapema.”

Kwa mujibu wa Tafiti za Tanzania Demographics Health Survey (TDHS 2015) zinaonesha kuna uhusiano wa karibu sana kati ya tatizo la upungufuwa damu kwa wanawake kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa miaka 15 hadi 49 ,kwa wanawake wajawazito .

Kitakwimu asilimia 44 ya wanawake wenye umri wa kuzaa wana upungufu wa damu huku asilimia 57.1 ya wanawake wajawazito nao wakiwa upungufu wa damu.

Aidha Takwimu za Tanzania National Nutrition Survey (TNNS 2018) mikoa inayoongoza kwa upungufu wa damu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni  Shinyanga asilimia 70.9,Geita asilimia 68.1,Kigoma asilimia 67.2,Morogoro asilimia 65.7 na Mwanza asilimia 62.6.

Dkt.Halima amesema lakini pia  mtoto anaweza kupata utapiamlo kwa sababu ya mama mjamzito kukosa lishe na hivyo akazaliwa mdogo kuliko umri wake na hivyo kushindwa kukua vizuri.

Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Makole jijini Dodoma Josephine Dikoko ametaja athari za magonjwa hayo kuwa ni pamoja na kuathiri ukuaji wa mtoto  kwa sababu ili mtoto akue vizuri ni lazima awe na afya njema.

Jacquline Joseph na Andrea Charles wote wakazi wa Dodoma mjini  wameiomba Serikali iendelee kuelimisha jamii umuhimu wa malezi ya watoto kwani bado jamii haizingatii mambo muhimu yatakayomuwezesha mtoto kukua vizuri.