November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

????????????????????????????????????

Lipumba: Uchaguzi isivunje amani ya nchi

Na Allawi Kaboyo, TimesMajira Online, Karagwe.

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba, amesema uchaguzi huu usiwe chanzo cha uvunjifu wa amani ya Tanzania.

Akitoa kauli hiyo kwenye mkutano wake wa hadhara wa kuomba kura katika uwanja wa changalawe uliopo mjini Kayanga wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, Lipumba amesema Tanzania imekuwa kisiwa cha amani kwa kipindi kirefu, hivyo watanzania wanao wajibu wa kuhakikisha amani hiyo inadumu hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Amesema, vyama vya siasa vinatakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuhubiri amani huku akiomba tume ya uchaguzi nchini kuhakikisha inasimamia uchaguzi huu unakuwa wa huru na haki suala litakalopelekea nchi kudumu katika amani kwa kuwa haki itatendeka.

“Amani hii tuliyonayo tunapaswa kuilinda na kuhakikisha inadumu, niiombe tume yetu ya uchaguzi ihakikishe uchaguzi huu unakuwa wa huru na haki na ikifanya hivyo hakika amani yetu itastawi katika misingi ya tuliyoasisiwa, CUF tunaamini katika amani na sera yetu imejikita katika haki sawa kwa wote” Amesisitiza Prof. Lipumba.

Ameongeza kwa kusema, anatambua wananchi wa wilaya ya Karagwe wanazo changamoto nyingi ikiwemo kero sugu ya maji pamoja na migogoro ya ardhi inayowapelekea wengi wao kupoteza haki na hivyo kuwaomba wanankaragwe kumchagua ili kuweza kuwasaidia kutatua kero hizo kwa muda mfupi.

Hata hivyo mgombea udiwani kata ya Kihanga wilayani humo kupitia chama hicho Anastella Kibake, amemuomba mwenyekiti wake na mgombea urais endapo atapewa ridhaa na watanzania kuiongoza nchi hii kuwasaidia wakina mama wajane na watoto yatima kwakuwa wamekuwa wakidhurumiwa haki zao.

Anastella amesema, wananchi wa kata hiyo wanakabiliwa na changamoto ya huduma za afya hasa wakina mama wajawazito kwa kutozwa fedha nyingi wanapokwenda kujifungua hali inayowapelekea wanawake hao kuhatarisha maisha yao pamoja na watoto wao kwakuwa wamekuwa wakijifungulia majumbani kwa kuogopa gharama.

Nje ya kero hizo amesema, wanawake wamekuwa wakitaabika kwa kutembea mwendo mrefu kufata huduma ya maji ambapo wamekuwa wakishindwa kufanya shughuli nyingine za kuwaongezea kipato na wengine kuhatarisha ndoa zao.

%%%%%%%%%%%%