November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lina PG Tour yafufua gofu Moshi

Na Mwandishi wetu, Moshi

KUWEPO kwa mashindano ya gofu ya Lina PG Tour katika viwanja vya gofu vya klabu ya Moshi Gymkhana, kumesaidia kufufua mchezo huo na kuboresha viwanja hivyo ambavyo awali vilikuwa na hali mbaya kutokana na kutokuwepo kwa michuano kwa miaka mingi.Imeelezwa viwanja hivyo ambavyo vilikuwa havina nyasi siku ya kwanza ya michuano ya Lina PG Tour viligeuka vya kijani siku inayofuatia kuamkia Ijumaa Septemba 27, 2024 wakati michuano hiyo ikiingia siku yake ya pili.

Hayo yote yalibainishwa na Mkurugenzi wa mashindano hayo ya Lina PG Tour wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema anaamini kuwepo kwa michuano hiy katika viwanja vya Moshi Club ni baraka kubwa kwa sababu ni viwanja ambavyo Lina Nkya, ambaye alikuwa muasisi wa maendeleo ya gofu ya wanawake nchini, alianzia kucheza hapo.

Amesema michuano hiyo inafanyika kwa kuwaleta wachezaji wa gofu pamoja kwa lengo la kumuenzi Lina Nkya ambaye alikuwa mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya gofu.

“Siamini ninachokiona leo, naona ghafla nyasi zimeota na viwanja vimekuwa kijani sasa. Viwanja vinavutia sana tofauti na siku ya kwanza tulipoanza michuano hii,” amesema

Kwa mujibu wa Challi, alisema viwanja vya gofu vya Moshi Gymkhana vilikuwa kama vimetelekezwa au vimekufa kabisa kwa sababu hakukuwepo na mashindano yoyote makubwa kwa miaka mingi.

“Kuwepo kwa Lina PG Tour hapa kumefufua viwanja na mchezo wa gofu, na mashindano haya tofauti na siku za nyuma, yameweza kuvuta hata wachezaji kutoka Kenya,” alifafanua Challi.

Raundi ya kwanza ya mashindano hayo ilianzia katika viwanja vya TPC mwezi Februari mwaka huu ambako washindi wake wa kwanza walikuwa Nuru Mollel kwa upande wa gofu ya kulipwa na Ally Isanzu kwa upande wa gofu ya ridhaa.

Viwanja vya gofu vya Morogoro Gymkhana vilikuwa ni mashuhuda wa raundi ya pili ya Lina Tour ambako Hassan Kadio aliibuka mshindi wa kitengo cha gofu ya kulipwa na Ally Isanzu tena akishinda gofu ya ridhaa.

Mambo yalikuwa tofauti jijini Arusha ambako raundi ya tatu ya Lina Tour ilichezwa.Nuru Mollel tena alishinda kwa upande wa gofu ya kulipwa lakini mambo yaikuwa tofauti katika gofu ya ridhaa ambayo mshindio wake alikuwa Jay Nathwani wa Arusha.

Raundi ya nne ya michuano ya Lina PG Tour inachezwa mjini Moshi baada ya raundi tatu za mafanikio katika viwanuja vya klabu za TPC, Morogoro Gymkhana na Arusha Gymkhana.Yasiyokuwa ya kawaida katika viwanja vya Moshi ni washindi wengi ambao hawakuonekana katika raundi tatu zilizopita.

Miongoni mwa majina yaliyoshangaza katika raundi ya nne ni Karim Ismail aliyerudisha mikwaju 75, Jumanne Mbunda aliyeleta mikwaju 76 akiwa mbele ya Ally Isanzu ambaye alishinda raundi mbili za kwanza kwa mikwaju mitano.