Na Mwandishi wetu, timesmajira
ZAIDI ya wachezaji 80 wakiwemo 16 wa kulipwa wamejitokeza katika michuano ya Gofu inayoitwa Lina PG Tour ambayo imeanza kurindima katika Viwanja vya TPC Moshi.
Shindano hilo limeandaliwa na familia ya Said Nkya kwa kushirikiana na Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU) kwa lengo la kumuenzi mchezaji wa zamani wa timu ya taifa anayeitwa Lina Nkya.
Akizungumza jana wakati wa usajili wa wachezaji hao Makamu wa Rais wa TLGU Ayne Magombe alisema ushiriki umekuwa mkubwa kuonesha namna watu walikuwa wakimkubali mchezaji huyo wa zamani hivyo kutegemea ushindani kuwa mkubwa.
“Wachezaji wengi wameshawasili na wako tayari kupambana, tunategemea ushindani utakuwa mkubwa na vipaji vitakuwa vingi, tunawahimiza mashabiki wa mchezo huu kujitokeza kwa wingi kushuhudia mastaa wakichuana,”amesema.
Naye Katibu wa Chama cha Gofu nchini,Enock Magire alisema chama kiliona umuhimu wa kushiriki katika shindano hilo hasa kwenye kusaidia kupata washindi wengi zaidi watakaoiwakilisha nchi katika mshindano mbalimbali ya kimataifa.
Kwa upande wa wachezaji wa gofu wa kulipwa wanaoshindana katika mashindano hayo, Brison Nyenza alisema ni jambo jema na zuri kwa Tanzania kuwa na mashindano ya Tour(ziara) kwani yatasaidia kuwaleta pamoja wachezaji na kujipatia kipato kwa wale watakaoibuka washindi.
“Kiasi ambacho kimewekwa kama zawadi ni kikubwa hivyo ni fursa kwangu kama mchezaji wa gofu wa kulipwa kutengeza pesa zaidi na kunipa motisha ya kuendelea kucheza mchezo huu,” amesema
Mashindano hayo yanatarajiwa kumalizika siku ya Jumaapili Machi 3,2024 na baada ya hapo yatafanyika katika mikoa mingine ambayo ni Arusha, Zanzibar na Dar es salaam.
Lina Nkya alikuwa ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Gofu na miongoni mwa wachezaji waliopeperusha vyema bendera ya Tanzania mwaka 2011 walipotwaa taji la Afrika Mashariki na Kati katika mashindano ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Dar es Salaam.
More Stories
Madiwani Korogwe TC wahakikishiwa maji ya uhakika
CHADEMA wampongeza Mkurugenzi Mpanda
Ukosefu wa maji wasababisha wanafunzi kujisaidia vichakani