April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LGTI imewaasa wanafunzi kuacha kukata tamaa wanapokosa alama zinazowaruhusu kuingia kidato cha tano

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline, Dodoma.

CHUO cha Serikali za Mitaa (LGTI),Hombolo-Dodoma kimewataka wazazi wenye watoto wanaomaliza kidato cha nne kuacha kuwakatisha tamaa wanapohitimu na kupata alama zisizoruhusu kuingia kidato cha tano bali wawapeleke chuoni hapo kujiunga na kozi zinazoendana na alama zao.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo na Afisa Udahili wa Chuo hicho Misu Chibona katika  Maonesho ya Elimu ya Sayansi na mafunzo ya ufundi stadi (TVET) yenye lengo la kuhasisha wanafunzi kujiunga na vyuo vya ufundi vya kati ambapo alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wazazi kuwavunja moyo watoto kuona kwamba hawezi kuendelea na masomo kutokana na alama zao kuwa ndogo.

“Kutokana na kuona matukio mengi mabaya  yanayofanywa na watoto waliokatishwa tamaa na alama zao za mitihani sisi kama chuo tuliona kuna haja ya kutembelea mashuleni kuhamasisha wanafunzi kutojisikia vibaya wanapopata alama hizo bali waangalie njia nyingine ya kujiendeleza ikiwemo kuja chuoni kwetu,

“Tulitembelea Shule zote za Sekondari Mkoa wa Dodoma na kueleza kozi tunazotoa lakini pia tuliwaambia sisi tunapokea hata mwanafunzi aliyefaulu kwa alama angalau D nne kusoma ngazi cheti,”amesema  Chibona.

Ametaja kozi zinazomruhusu mwanafunzi aliyefaulu kwa alama ya D nne kuwa ni utawala katika Serikali za Mitaa,Uhasibu na fedha,Maendeleo ya jamii,Kumbukumbu na nyaraka,Rasilimali watu na manunuzi.

“Ili kuokoa jamii wasijione wakosefu wanapopata alama zisizoruhusu kuingia kidato cha tano Chuo chetu tumejipanga kwenda shule za zote za Sekondari nchi nzima ilikuhamasisha wanafunzi kujiunga na chuo chetu,”amesema.

Amesema baadhi ya wazazi wamekua mstari wa mbele kuwarudisha nyuma watoto katika kipengele cha elimu kwa kuwakatisha tamaa kwamba wakisoma ngazi ya cheti elimu yao itakuwa ndogo kitendo ambacho siyo kweli kwani mwanafunzi wao akimaliza ngazi ya cheti anauwezo wa kuendelea kupata Diploma na kuendelea zaidi hadi degree.

“Nawasisitiza wazazi mtoto akishindwa kuchaguliwa mpeleke akapate elimu inayoendana na alama zake kwasababu anayoendelea ndivyo elimu yake inavyokuwa,

“Nasasa hivi ukisoma chuo chetu kinafaida kwasababu Serikali imetoa nafasi za ajira katika mikoa mbalimbali za watendaji wa vijiji na kata hivyo wanafunzi wakihitimu ajira zipo,”amesema.