December 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KWATAARIFA YAKO: Kuliwahi kutokea janga la mziki, watu zaidi ya 400 walicheza mpaka kufa

Na Mwandishi Wetu

HISTORIA inaonyesha kuwa, katika mwezi Julai, mwaka 1518, wakazi wa Jiji la Strasbourg (wakati huo ikiwa chini ua utawala wa Roma siku hizi Ufaransa) walikumbwa na hisia ambazo zilishindwa kuzuilika za kucheza mziki.

Kwa mujibu wa jarida maarufu la History, tatizo hili lilianza pale mwanamke aliyejulikana kama Frau Troffea, alipoingia mitaani na kuanza kusakata mziki kimya kwa kukatika na kucheza.

Mwanamke huyo alicheza mziki kwa wiki nzima, kabla ya watu wasiopungua 50 kuungana naye kulisakata densi kimya kimya.

Ilipofika mwezi Agosti,1518 janga hilo la mziki lilikumba zaidi ya watu 400, bila maelezo ya kina kuhusu janga hilo, wanasayansi walielekeza lawama zao katika kile walicokiita “damu inachemka” na kupendekeza kuwa wenye hali hiyo kutibiwa.

Hivyo liliundwa jukwaa na wabobezi wa kucheza mziki waliletwa. Manispaa ya Jiji hilo pia ilikodisha bendi ya muziki ili kutumbuiza wakati watu wakiendelea kucheza, hata hivyo haikuchukua muda kabla ya vifo kuanza kutokea.

Wachezaji wengi walianza kuanguka na kuzimia kutokana na uchovu mwingi. Wengine walipoteza maisha kutokana na shinikizo la damu pamoja na miili yao kupooza.

Tukio hilo la ajabu kuwahi kutokea halikuisha mpaka mwezi Septemba, ambapo kutokana na hali kuendelea kuwa mbaya wachezaji hao walikusanywa na kupelekwa katika maombi. Janga la Strasbourg (siku hizi Ufaransa) laweza kuonekana kama jambo lililopitwa, lakini lilirekodiwa vizuri na kuingizwa katika historia karne ya 16.

Pamoja na janga hilo pia kumekuwa na matukio kama hayo nchini Switzerland, Ujerumani na Uholanzi japo hayakuwa makubwa kama janga la mwaka 1518.

Kwa mujibu wa Mhistoria, John Waller, inaaminika kuwa palikuwa na Mtakatifu Vitus wa Kanisa Katoliki, aliyetambulika barani Ulaya karne ya 16 kuwa alilaani na kusababisha msongo wa mawazo ambao ulisababisha janga hilo la kucheza mziki.

Pamoja na kuwa kulikuwa na tishio la magonjwa na janga la njaa, mambo ambayo kwa pamoja yaliiathiri sana Strasbourg katika karne ya 1518, Mtakatifu Vitus alidaiwa kusababisha msongo mkubwa katika jiji hilo.
Wengine wanadai kuwa, wachezaji hao walikuwa ni waumini wa dini mpya, au walilishwa bila kujua mmea wenye sumu ambao huamsha hisia za kutojitambua.

Hata hivyo, rekodi ya tukio hilo unaweza kuiona kwa kina kupitia Strasbourg’s Musée de l’Oeuvre Notre-Dame pamoja na andiko la mwandishi wa Ufaransa, Jean Teulé, au kufuatilia mtiririko wa kumbukizi za maDJs waliolipatia tukio hilo jina la “1518”.