Na Aveline Kitomary,TimesMajira online,Dar es Salaam.
MIONGONI mwa sintofahamu wanayokumbana nayo baadhi ya wanawake ni matumizi ya dawa za dharura za kuzuia mimba maarufu kama P2 kushindwa kufanya kazi yake kama ilivyokusudiwa.
Kadhia hii wanajikuta wakibeba ujauzito bila kuelewa nini kilitokea kwani waliamini matumizi ya vidonge hivyo vya dharura kuwakinga.
‘Vero’ sio jina lake halisi alipata ujauzito baada ya kufanya ngono isiyo salama na kutumia vidonge vya dharura (P2) akitarajia kuwa vitamsaidia lakini baada ya mwezi mmoja alijigundua kuwa ni mjamzito.
Sasa ana mimba ya miezi mitatu ameanza kupata huduma za afya na anajiandaa kupata mtoto bila kutarajia.
“Nilikuwa najua kuwa niko siku za hatari lakini hata nilivyomwambia mwenzi wangu tutumie kinga alisema naweza kutumia vidonge vikanisaidia lakini baada ya kutumia sikuona hedhi kwa wakati unaotakiwa nikajipa moyo kusuburi nikifikiri vidonge ndivyo vinachelesha.
“Lakini cha kushangaza baada ya mwezi mmoja nikaanza kupata mabadiliko na nilivyopima majibu yalionesha kuwa nimeshika mimba.
“Ilikuwa ngumu kidogo kupokea hali hiyo lakini ikabidi ni kubali kwa sababu ilishatokea ,”anaeleza Vero.
Anasema kuwa sio mara moja kutumia vidonge hivyo na kwa vipindi vya nyuma alivyotumia viliweza kumsaidia.
“Ni mara nyingi tu natumiaga P2 kama niko siku za hatari na nikafanya ngono lakini huwa vinanisaidia sasa sijui kwa kipindi hiki nini kilitoa.
Kwa mujibu wa habari ya BBC inakaridiwa kuwa asilimia 0.6 mpaka asilimia 2.6 ya wanawake wanaokunywa vidonge vya kuzuia mimba mara baada ya kushiriki kwenye tendo la ndoa ambayo sio salama wanaweza kupata ujauzito.
Mambo gani watu hawajui kuhusu vidonge hivyo vya dhararu vya kuzuia mimba.
KWANINI VIDONGE VINASHINDWA KUFANYA KAZI?
Mwandishi wa Jarida la Majira ya Afya alikutana na Mtaalam wa afya ya uzazi na elimu kwa vijana kutoka Hospitali ya Marie Stopes Mwenge, Dkt. Mashingo Lerise akamuuliza kwanini vidonge vya dharura vinashindwa kufanya kazi?
Akijibu swali hilo Dkt.Lerise anasema mzunguko wa hedhi unaweza kuwa kikwazo kwa dawa hizo kufanya kazi kutokana na jinsi dawa inavyofanya kazi kuchelewesha au kuzuia yai kutoka katika vifuko vya mayai na endapo yai litakuwa limepevuka na kutoka kwenye kifuko cha mayai, msaada wa dawa
hizo unapungua.
“Katika vitu vinavyosababisha isifanye kazi vizuri,ni pamoja na yai kupevuka na kuachiwa kutoka kwenye kifuko cha mayai (ovulation). Kama unajua siku zako ikiwa imetumika kabla ya yai kutoka kwenye mfuko
wa uzazi inakuwa na matokeo bora zaidi, ila baada ya ovulation kutokea uwezo wake unapungua”.
“Hivyo ni muhimu kufahamu mzungungo wa hedhi kwa muhusika ili dawa hizi ziweze kuwa na msaada”anasema Dkt. Lerise.
Kwa kawaida yai la mwanamke hupevuka siku ya 14 (kwa wale wenye mzunguko wa siku 28) kwa maana ya wiki mbili kabla ya kuingia kwenye hedhi.
Anasema sababu zingine za dawa hizo kushindwa kufanya kazi ni matumizi ya nje ya muda unaotakiwa ambao ni saa 72 kwa maana ya siku tatu.
“Matumizi ya hii dawa kwa jinsi inavyofanya kazi inashauriwa kumezwa ndani ya saa 72 baada ya kukutana na mweza wake.Baadhi wanasubiri saa 72 ndio anameza,hapa anakuwa ameshachelewa kama endapo itatumika kwa usahihi inazuia mimba kwa asilimia kati ya 52 mpaka 100.
“Unatakiwa kumeza mapema sana ili kuwa na ufanisi wa kufanya kazi kwa haraka kwani kwa kadiri unavyochelewa uwezo wa dawa unapungua na kwa sababu ya kusababisha kichefuchefu inashauriwa nkumezwa baada chakula,”anaeleza.
Anasema sababu nyingine ni uzito mkubwa “Tafiti zinaonesha kuwa watu walio na uzito zaidi ya kilogram 70 wanahatari ya mara mbili hadi nne ya dawa hiyo kushindwa kufanya kazi katika miili yao.
“Kingine ni mwingiliano wa dawa.Kuna dawa ambazo mtumiaji akiwa anatumia kwa wakati mmoja na vidonge vya dharura, vinapunguza uwezo wa vidonge hivi vya majira kufanya kazi.
Mfano wa dawa hizi ni pamoja na dawa za fangasi,saratani,dawa za kifafa,” anafafanua Dkt.Lerise.
Kwa Vero hili ni suala geni kwake ,hakulijua hilo mapema,sasa anaendelea kulea mimba yake kwa kuhudhuria kliniki hadi hapo atakapojifungua.
“Inawezekana yai kupevuka na kutoka nje ya mfuko wa uzazi ndio chanzo cha dawa kushindwa kufanya kazi kwa sababu nakumbuka nilitumia mapema wala sina tatizo la kutumia dawa zingine lakini nilikuwa sijui kabisa kuhusu yai kupevuka .
“Hili limekuwa nje ya mpango wangu lakini sasa nitafanya nini? nimeamua kulea lakini nashauri kuwe na elimu kama hii kwa wanawake ili kuepuka haya yaliyonikuta mimi,”anashauri kwa msisitizo.
WANAOPASWA KUTUMIA NJIA YA DHARURA
Dkt.Lerise anasema njia hiyo ni ya dharura kwa mwanamke inapaswa itumike endapo anahisi yuko kwenye hatari ya kupata ujauzito baada ya kufanya ngono na wala sio kupanga kutumia.
“Kwa mfano mtu aliyetumia kondom halafu ikapasuka au ikavuka na akajua haijamsaidia anatakiwa kutumia vidonge vya dharura.
Vivyo hivyo kwa mtu anayetumia kalenda na kwa bahati mbaya akachanganya tarehe,au anayetumia kitanzi halafu kikachomoka,au mwanaume kushindwa kumwaga mbegu nje (Withdrawal method) kwa wakati vidonge hivi vinaweza kutumika ili kuzuia ujauzito ambao haukutarajiwa.
“Lakini pia kwa mwanamke ambaye amebakwa au kushinikizwa kushiriki tendo la ndoa bila ridhaa yake, licha ya kutumia anashauriwa kwenda kupima magonjwa ya zinaa kama Hiv,”anafafanua.
MADHARA YA KUTUMIA KIHOLELA
Dkt.Lerise anasema dawa za dharura zinavichochezi ambavyo kazi yake ni kuchelewesha au kuzuia yai kutoka kwenye mfuko wa uzazi kwenda kurutubishwa.
Vichocheo hivyo pia hubadilisha wepesi wa ute na hufanya kuwa nzito ili mbegu zisiweze kuwa na urahisi wa kusafiri.
Pamoja na utendaji kazi huo,vidonge hivyo havitakiwi kutumika mara kwa mara kama njia ya uzazi wa mpango.
“Kama zilivyo dawa zingine, vidonge hivi pia vina maudhi madogo madogo mfano maumivu ya tumbo chini ya kitovu, kutoka na damu kusiko kwa kawaida, kichefuchefu na kutapika, maziwa kuvimba na kuambatana na maumivu. Hivyo basi matumizi yake ya mara kwa mara hufanya maudhi kuwa makubwa
zaidi hasa kutokwa na damu katika uke kuliko kawaida wakati wa hedh”.
“Na Kwa sababu inabadilisha mfumo wa hedhi,mzunguko unaweza kuwahi, kuchelewa au usiweze kuona kabisa kwa mwezi wote.Kiutaratibu ni vyema kupata ushauri wa wataalamu wa afya ili kuweza kupata dawa inayofaa,”anasema.
Anasema kumaliza dozi ni njia nzuri ya dawa hizo kufanya kazi kwa ufasaha “Kuna dawa ina vidonge viwili na kimoja na vyote vinaufanisi sawa. Ikiwa dawa ina vidonge viwili,lakini ukameza kimoja, dawa haitafanya kazi.
“Kikubwa tunasisitiza kwa wale wanaotumia mara kwa mara wakati wanapowaza kutumia dawa hizo vizuri wakakumbuka kuna magonjwa mengine kama homa ya ini, saratani ya mlango wa kizazi na HIV ambayo ni hatari zaidi kuliko ujauzito ambayo vijidudu vinavyosababisha huenezwa kwa kufanya ngono
zembe”.
“Wakati unafikiri vidonge vya dharura kuwa njia ya kujikinga lakini pia fikiria namna unvyoweza kupata magonjwa na kupoteza maisha kwahiyo mtumiaji afikirie na haya magonjwa. Na pia dawa za uzazi wa mpango zinatolewa bure katika vituo vya Marie Stopes kama ilivyo kwenye vituo vya serikali na binafsi,inakuwa rahisi kuliko kutumia hizo ambazo ni gharama kwani bei ya chini ni Sh 5000 kwa dozi moja”,anaeleza Dk Lerise.
NJIA ZA UZAZI WA MPANGO
Kwa mujibu wa Dkt.Lerise kuna makundi manne ya njia zinazoweza kukukinga na ujauzito usiotarajiwa.
“Kundi la kwanza ni njia ya vidonge vya dharura, la pili ni za muda mfupi zipo za vidonge na sindano. Pia kuna za muda mrefu kama kijiti au kipandikizi na kitanzi na zipo njia kudumu yani kufunga uzazi.
ELIMU NI MUHIMU
Daktari huyo anaitaka jamii kutafuta taarifa sahihi kutoka kwa wataalamu wa afya katika vituo vya afya ili kuweza kuwa na maamuzi sahihi .
“Watu wanatakiwa kuuliza na kudadisi vitu wanavyotumia.Wengine wanapoenda kununua vidonge hivi vya dharura, almaarufu P2 wanakuwa hawajiamini,wanaenda kwa kujificha na kujihukumu hivyo wanaenda na kuchukua haraka bila kusubiri maelekezo. Ni vizuri waende kituo cha afya wapate maelezo mazuri.
“Kama hutaki kubeba ujauzito ni bora kutafuta njia nzuri ya kujikinga usipate mimba. nenda kwa muhudumu wa afya akusaidie kwa ushauri. Watoa huduma za dawa washuri watu wanaoenda kununua dawa ili waweze kuwa na taarifa sahihi, mfano ukitapika ndani ya masaa 2 tangu kumeza dawa hii
inashauriwa urudie tena kumeza. Kwa taarifa kama hii, ni muhimu muuzaji kuongea na mteja kabla ya kuanza kutumika,” anashauri Dkt.Lerise.
mwisho
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika