June 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kwanini kila taasisi inapaswa kuchangia mapato yasiyo ya kodi

Na Penina Malundo,Timesmajira

Katika safari ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, mchango wa taasisi za umma kupitia gawio na mapato mengine yasiyo ya kodi, ni chachu ya ustawi wa taifa.

Serikali imewekeza jumla ya Sh86.3 trilioni katika taasisi za umma na kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache. 

Uwekezaji huu mkubwa unaipa Serikali msingi wa kisheria na kiutendaji wa kudai mapato kutoka kwa taasisi hizo kama sehemu ya kurejesha thamani ya uwekezaji wa umma.

Katika kutambua umuhimu huo, Serikali imeanzisha Siku ya Gawio – itakayoadhimishwa Jumanne, Juni 10, 2025 – kama sehemu ya kuenzi na kuhamasisha ushiriki wa mashirika ya umma na kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache katika kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, gawio na michango mingine ya mapato yasiyo ya kodi huchangia moja kwa moja kwenye bajeti ya Serikali. 

Fedha hizi husaidia kugharamia huduma za msingi kama afya, elimu, maji safi na salama, pamoja na ujenzi wa miundombinu muhimu inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja. 

Mapato haya, yanayokusanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, huwasilishwa moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa Serikali ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya maendeleo.

 Kwa kufanya hivyo, Serikali hupunguza utegemezi wa misaada kutoka kwa wahisani na mikopo kutoka nje, hivyo kuimarisha uhuru wa kifedha na kuwezesha maamuzi ya kisera yaliyojikita katika vipaumbele vya kitaifa.

Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina yameongezeka kutoka shilingi bilioni 637.67 mwaka 2020/21 hadi kufikia shilingi bilioni 767.2 mwaka 2023/24. 

Hili ni ongezeko la asilimia 20.3, linalothibitisha mafanikio ya juhudi za Serikali katika kusimamia rasilimali za umma kwa weledi na kuongeza mchango wake katika bajeti ya taifa.

Mchechu amesema mwaka huu makubwa zaidi yategemewe, huku akisisitiza kuwa maandalizi yamefanyika kikamilifu na taasisi nyingi tayari zimeonesha utayari wa kuchangia zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Ili kufikia lengo la mwaka huu wa fedha, ambalo ni kukusanya Sh1.113 trilioni. amehimiza kampuni, taasisi na mashirika yote ya umma kuendelea kuwasilisha gawio na michango yao.

“Taasisi ambazo bado hazijakamilisha kuwasilisha gawio na michango mingine zinatakiwa kufanya hivyo kabla ya tarehe 30 Juni 2025,” ameagiza Mchechu.

“Ushirikiano wa kila taasisi ni muhimu katika kuijenga Tanzania yenye uchumi imara, huduma bora kwa wananchi, na maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, utaratibu huu wa uchangiaji huongeza uwajibikaji kwa mashirika ya umma, kwani unawalazimu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kuimarisha utendaji wa ndani, na kuhakikisha kuwa wanapata faida inayoweza kurejeshwa kwa umma kupitia gawio.

Amesema  Idadi ya mashirika yanayotoa gawio na kiasi kinachochangwa kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka, jambo linaloonesha dhamira ya kweli ya taasisi hizi katika kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa upande wa kijamii, mapato haya huwezesha utekelezaji wa miradi yenye tija kwa wananchi kama vile ujenzi wa vituo vya afya vijijini, madarasa, pamoja na huduma nyingine za kijamii zinazoboreshwa kila mwaka kwa kutumia fedha zinazotokana na gawio na michango mingine. 

Kwa upande wake,Lightness Mauki, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini – Mashirika ya Kibiashara, Ofisi ya Msajili wa Hazina, amesema Kupitia uwazi katika ukusanyaji na matumizi ya fedha, wananchi hujenga imani kwa taasisi za umma na kupata ujasiri wa kufuatilia kwa karibu jinsi rasilimali za umma zinavyotumika kwa manufaa ya wote. 

Hali hii, ameongeza, huongeza ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya maendeleo na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Ili kuimarisha zaidi ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeweka mikakati ya kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato kwa kutumia mifumo ya TEHAMA kama PlanRep na mifumo ya malipo ya kielektroniki. 

Ameongeza kuwa Serikali pia imekuwa ikifanya tathmini za mara kwa mara za vyanzo vya mapato ili kubaini fursa mpya za kuongeza mapato na kuhakikisha kuwa kila rasilimali inatumika ipasavyo.

Vyanzo vya mapato yasiyo ya kodi vinajumuisha gawio, ambalo hutokana na faida za mashirika na taasisi za umma zinazofanya biashara. 

Gawio hili hukusanywa kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni na Sheria ya Mashirika ya Umma. 

Aidha,amesema taasisi ambazo hazimo kwenye kundi la gawio zinatakiwa kuwasilisha asilimia 15 ya mapato yao ghafi kila mwaka kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma.

 Pia, zipo taasisi zinazopaswa kuwasilisha mapato ya ziada kila mwisho wa mwaka wa fedha, ambapo hulazimika kuwasilisha asilimia 70 ya ziada hiyo kwa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina. 

Vyanzo vingine ni pamoja na marejesho ya mikopo na riba kutoka mashirika ya umma, pamoja na mapato yanayotokana na matumizi ya mtambo wa TTMS unaosimamia mawasiliano ya kielektroniki kati ya Tanzania na mataifa mengine.

Kwa upande wake Neema Musomba, Mkurugenzi wa Huduma za Kimenejimenti amesema makusanyo yasiyo ya kodi ni mhimili muhimu wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali na miradi ya maendeleo ya taifa. 

Kwa kutambua hilo, alisema, usimamizi wa mashirika ya umma umeimarishwa kwa kuhakikisha kuwa kila taasisi inatekeleza wajibu wake wa kutoa gawio na michango mingine kwa mujibu wa sheria.

“Ni wajibu wa kila taasisi ya serikali, na kampuni ambayo serikali ina umiliki wa hisa, kuhakikisha inashiriki katika kufanikisha ustawi wa taifa letu,” amesema Musomba.

Kupitia kampeni ya Siku ya Gawio 2025, Serikali inasisitiza umuhimu wa usimamizi bora wa rasilimali za umma, uwajibikaji wa taasisi, na ushiriki wa kila shirika katika kuchangia maendeleo ya taifa.