November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kwaheri Maradona nyuma umeacha alama ya mshindi

Na Philemon Muhanuzi, TimesMajira Online

MSIBANI ni mara chache sana kuona watu wakichekeshwa na bashasha ya maneno ya waombolezaji wanaopewa nafasi ya kumuenzi marehemu. Hata kama maneno ni ya kuchekesha waombolezaji hupiga makofi kama ishara ya kuguswa na ujumbe wa mzungumzaji.

Ameondoka gwiji wa soka wa Argentina, Diego Armando Maradona. Enzi za uhai wake alijawa na vituko vya kila aina. Alikuwa ni mwingi wa uchangamfu wa mbele za watu akiwa hajali kabisa kamera zilizomzunguka kila aendapo.

Siku ya msiba wake pamoja na uchangamfu aliojaliwa na Muumba akiwa hai, hakutatokea mchekeshaji atakayeweza kupeleka tabasamu kwenye nyuso za waombolezaji.

Marehemu huheshimiwa na Diego Maradona hatapunguziwa heshima anayoistahili. Zimekuwa ni wiki chache zenye habari za misiba ya wanasoka wa zamani.

Wamefariki wachezaji wa zamani wa Uingereza waliocheza kombe la dunia mwaka 1966 wakati Maradona akiwa ni mtoto wa miaka sita. Umri wao ni miaka zaidi ya 75, wameishi ukizingatia hii dunia yenye maradhi mengi yasiyo na huruma hata kidogo.

Pengine Maradona alikuwa amebakiza miaka 15 au 20 aweze kuufikia umri wa Pele na wakongwe wengine. Afya yake haikuwa nzuri na hakuonekana kujali sana katika suala la kujinyima starehe nyingi za kidunia.

Kwa kawaida ukishafikisha miaka kuanzia 60 kwenda juu inakubidi ufunge breki kwa maana ya kupunguza mambo ambayo mwili unaanza kuyakataa. Na haswa kama mhusika ni mchezaji aliyetumia nguvu nyingi ujanani mwake.

Maradona alichezewa rafu nyingi mno na mabeki wa timu za mataifa na wale wa vilabu. Alikuwa ni sugu sana, mfupi na mwenye stamina ya kutosha.

Sunday Oliseh wakati akihojiwa kuhusiana na ushiriki wa Nigeria katika mechi za kombe la dunia la mwaka 1994 alisema kuwa wao mabeki walimpiga sana viatu Maradona lakini kila mara alikuwa akiamka.

Walicheza rafu mpaka wakachoka lakini baada ya dakika tisini kumalizika huyo waliyetaka kumkomoa bado akawa na uwezo wa kusimama na kuondoka uwanjani. Na hao mabeki wa Nigeria ni vipande vya watu, kina Oliseh, Uche Ikechukwu,

Mike Emenalo na Marehemu Uche Okafor. Hapo hatujazungumzia rafu nyingine za kibabe alizochezewa na mabeki wa timu za ligi kuu ya Italia miaka ile akichezea Napoli.

Maradona alikuwa fundi haswa mwenye kuweza kuwa mwalimu wa hawa namba kumi wa kisasa. Wenye kulindwa sana na filimbi za waamuzi mpaka mtazamaji wa mechi anajikuta akitamani kubadilisha channel na kuangalia vipindi vingine.

Hawa namba kumi wanaoguswa tu na ghafla inasikika filimbi ya faulo wakati ukiangalia marudio ni kama vile hakuna walichofanyiwa. Mchezo umempoteza mtaalam aliyecheza mpira mgumu wa kutoonewa huruma na waamuzi pamoja na mabeki.

Maradona atakumbukwa sana na Waingereza haswa wale wakongwe wa kizazi chake. John Barnes na wenzake wote wa kikosi cha mwaka 1986 kule Mexico watamkumbuka gwiji huyu.

Aliwakera kwanza kwa kufunga goli la mkono halafu ndani ya mechi hiyo hiyo akawafunga goli lisilo na ubishi kwa kuwatesa kwa chenga mpaka kipa wao Peter Shilton nae akapokea zawadi ya kunyanyaswa kabla goli halijafungwa.

Hii itakuwa ni wiki ya Makala za wanasoka wa zamani wa Uingereza, wakiwakumbusha wale wa kizazi cha mwaka 1984 na wadogo zao wenye kuitwa watoto wa Milenia kwamba mwaka 1986 timu yao ilifungwa na Argentina iliyokuwa na mchezaji bora sana.

Mchezaji ambaye ni wa kiwango cha Pele wa Brazil, wakitoka hao wawili ndio wanakuja wengine kama Zidane. Halafu ndio wanakuja hawa kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wa kundi lile lile la watoto wa Milenia.

Ni msiba kwa familia ya wapenda soka. Haswa kwa wale waliokuwa wafuatiliaji wa miaka ile ya ujana wa Maradona. Na kama ilivyo kawaida ya misiba yote kila kitakachofanyika kitaambatana na upole wa waombolezaji.

Vile vituko vyote vya Marehemu Maradona vitawachekesha watu wakiwa katika uchache wao wakimuongelea. Wakati akiagwa yatapigwa makofi pale wasifu wake utakapokuwa ukisomwa. Pole maalum ziwafikie raia wote wa Argentina ambao wazazi wote wawili wa Maradona ni wenzao.

Pole zimfikie kila mpenda soka haswa mfuatiliaji wa uwezo wa kipekee wa Maradoka kama namba kumi atakayechukua miaka mingi kuja kupata wa aina yake. Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi.

%%%%