November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KWA TAARIFA YAKO: Mtoto anayeongopa hufanikiwa zaidi maishani

Na Mwandishi Wetu

Mwanao anaongopa au kufanya michezo ya uongo?Usiogope, kwa kawaida watu waongo huwa hawaaminiki, lakini ikifika kwa watoto, yaweza kuwa sio jambo baya.

Utafiti umekuja na jawabu. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Toronto (University of Toronto) nchini Canada, umebaini jinsi mtoto anavyoanza mapema kuongopa ndio jinsi anavyokuwa mjanja na kuishia kuwa na mafanikio maishani.

Watafiti walichunguza watoto zaidi ya 2,000 ili kuelewa kwa nini watoto hupindisha ukweli. Katika uchunguzi huo, kila mtoto aliwekwa katika chumba chenye kamera zilizofichwa na kuwekewa mdoli nyuma yake.

Watafiti waliwaeleza watoto wasigeuke kuangalia midoli ile, kati ya watoto 10, tisa walishindwa kujizuia na kuchungulia midoli ile. Baadaye walipoulizwa kama walichungulia ile midoli, karibu watoto wote walikataa, lakini walijikuta wakitoa maelezo walipoulizwa wanahisi midoli hiyo ikoje.

Asilimia 80 ya watoto wa umri wa miaka minne huongopa.Mtafiti Mkuu, Dkt.Kang Lee anasema, asilimia 30 ya watoto wa umri wa miaka miwili huongopa, nusu ya watoto wenye umri wa miaka mitatu hutengeneza maelezo ya uongo kwa wazazi wao na mpaka asilimia 80 ya watoto wa miaka minne hutunga uongo.

Mtu akidanganya, husababisha sehemu ya ubongo inayosaidia kufikiri kufanya kazi haraka ili kuziba mapengo, hiyo humaanisha kuwa mtoto anayeongopa mapema amepiga hatua ya haraka kuweza kushawishi kwa kutumia uongo wake.

Wazazi wasistushwe na uongo wa watoto wao, wataalam wanasema, “karibu watoto wote huongopa. Wenye uelewa zaidi hufanikiwa zaidi sababu wanaweza kushawishi kwa kutetea uongo,”anasema Dkt.Lee.

Wataalam waligundua hakuna uhusiano kati ya watoto kudanganya wakati wa utotoni na kukua kuwa wezi, matapeli (wapigaji) wakiwa watu wazima. Hivyo, haimaanishi uunge mkono mtoto kuongopa, wataalamu wanasisitiza kuwa ni muhimu sana kuwafundisha watoto umuhimu wa kuwa wakweli katika kipindi chote cha utotoni.

“Watoto waliofungwa jela au kutuhumiwa uhalifu, sio waongo wazuri,”anasema Dkt. Lee alipokuwa anahojiwa katika chaneli a televisheni ya CBC News.

“Watoto wanaoongopa mapema, na kudanganya vizuri, ni watoto watakao kuwa na makuzi ya kawaida. Wakiwa na umri wa miaka 7-8, sio uamuzi wao bali ni maneno watakayochagua kuongea ndio yatawaongoza, japo uongo wao unaweza ukawa haujapangika vya kutosha kumshawishi mtu mzima.

”Lakini jinsi mtoto anavyozidi kukua na kuvuka umri wa miaka 7-8, bila kujali uzoefu wake au amepitia mazingira gani, maelezo yake huanza kuwa magumu kwa mtu mzima kutambua uongo.

Japo hatupendi kukuza taifa la waongo, ni muhimu kujua kwamba watoto wetu wanapopindisha ukweli yaweza kuwa sio jambo baya,”anaongeza.

Wataalam wa masuala ya malezi kwa watoto wameieleza tovuti ya TimesMajira Online kuwa, wazazi au walezi wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wao wanawaongoza katika malezi ambayo yanazingatia miongozo ya vitabu vitakatifu ikiwemo Quaran takatifu na Biblia ili wakue katika misingi ya hofu ya Mungu, ambayo ni nguzo muhimu katika maisha ya binadamu yeyote.