December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kwa nini Rais Samia hafanani viongozi wengine maadui wa vyombo vya habari ?

Na Jackline Martin,Timesmajiraonline,Dar

DUNIANI kote historia inaonesha kuwa viongozi hasa wale wenye agenda za siri kwenye uongozi wao ni maadui wakubwa wa vyombo vya habari.

Miongoni mwa viongozi wasiopenda vyombo vya habari ni pamoja na Marais waliopo madarakani na waliomaliza muda wao. Wengi wanaviona vyombo vya habari kama adui kwao.

Mfano, Rais ambaye anatumia kiti hicho kufanya ufisadi wa mali za taifa lake, hawezi kuwa rafiki wa vyombo vya habar. Rais ambaye anatamani kubadilisha Katiba ya nchi yake ili abaki madarakani, hawezi kuwa mpenzi wa vyombo vya habari.

Kwa ufupi kiongozi anayefanya maovu dhidi ya Taifa lake, hawezi kupenda vyombo vya habari. Kwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa miongoni mwa marais wa Tanzania wanaotoa somo kwa viongozi wa mataifa mengine.

Amekuwa ni kiongozi anayependa vyombo vya habari akitaka vifanye kazi kwa uhuru bila kuingiliwa.

Hiyo inadhihirishwa maboresho makubwa yaliyofanywa na Rais Samia ambayo yameipandisha nchi chati kimataifa katika kuimarisha uhuru wa habari.

Hilo limethibitishwa na Ripoti ya World Press Freedom Index ya mwaka 2024 inayoonesha kuwa Tanzania imeongoza kwa nchi za Afrika Mashariki na duniani kushika nafasi ya 97 kutoka 143.

Anafanya hivyo, akitambua kwamba vyombo vya habari ni mdau mkubwa wa maendeleo.

Sifa hiyo imechochewa pia na mabadiliko ya mtanzamo wa waandishi wa habari kutokana na uzalendo mkubwa baina yao kwa kuwa katika utoaji taarifa zinazohusu nchi hiyo wametanguliza maslahi ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Juni 18, mwaka huu wakati akifungua Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari na Kakao kazi cha Maafisa Habari wa Serikali, Rais Samia anasema;

“Huko nyuma kipindi fulani vyombo vya habari na Serikali vilikuwa vinavutana.

Wao wamevuta na sisi tumevuta, lakini tuliona hatutofika pahali pazuri hivyo tuliamua kukaa sehemu moja, kuzungumza na kufanya kazi kwa pamoja.”

Kauli hiyo ya Rais Samia inadhihirisha wazi jinsi Serikali ilivyovipa uhuru mpana vyombo vya habari viweze kufanyakazi zake.

Rais Samia anasema vyombo vya habari si adui wa Serikali, bali ni mdau muhimu, hivyo Serikali haina budi kuweka sera nzuri na kudumisha uhuru wa vyombo vya habari.

Samia anasema vyombo vya habari vikiwa huru vinagusa kila pembe ya jamii kwa kuelemisha , kufichua maovu , kuchangia maendeleo ya kijamii na kukuza demokrasia.

Anawakumbusha waandishi kuandika habari zenye kuleta mawazo kinzani ya kuijenga nchi badala ya kuchochea migogoro na mipasuko ya kutishia amani ya nchi.

Ili kuvipa nguvu vyombo vya habari, Rais Samia anasema; “Serikali italipa madeni ya vyombo vya habari ifikapo Desemba, mwaka huu.

Anaagiza Wizara ya Fedha kufanya uhakiki wa madeni ya Serikali ili yanayolipika yalipwe huku akiahidi kusimamia suala hilo.

Lakini pia, anawakumbusha wamiliki wa vyombo vya habari wakati serikali inawalipa madeni hayo, wawalipe wafanyakazi wao mishahara yao.

Anasema kutowalipa kunapunguza ari ya kufanya kazi na kudhorotosha maendeleo ya sekta ya habari. Anawashangaa waandishi wa habari kuwa hodari kuandika mambo ya watu wengine wakati wao wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo kutolipwa mishahara na waajiri wao na hawasemi chochote.

Kadhalika, anasema sasa ni wakati wa vyombo vya habari kujiendesha kibiashara ili kuepuka madeni yasiyolipika yanaonekana kuwa mengi na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuwatia hasara.

Akizungumzia mabadiliko ya teknolojia, anasisitiza umuhimu wa kufikiria kuwekeza kwenye habari za mtandaoni kwa kuwa wasomaji wa magazeti ya kuchapisha wamepungua na pia malighafi za kuchapishia zimepungua kutokana na wazalishaji wakuu ambao ni nchi ya Ukraine kuathirika na vita, hali inayochangia kudorora kwa biashara zao.

Kuhusu uwajibikaji, Rais Samia anasema, amefanya juhudi kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na kusisitiza ni wajibu wao kuutumia kwa weledi na kuzingatia dhana ya uwajibikaji kwa sababu vina kazi muhimu ya kuunganisha Serikali na wananchi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Kwa upande wa kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani, anasema kalamu za waandishi wa habari zinahitajika kwa ajili ya kujenga na si kubomoa kwa kuleta migongano ya kisiasa.

“Kwa maneno mengine msitoboe dau tunalosafiria, ndani ya hilo dau tupo wote, ukitoboa yakiingia maji tunazama wote, msiingie kwenye mtego wa kurarua nyuzi zinazounganisha kitambaa cha taifa letu,” anasema.

Anasema uhuru wa vyombo vya habari haumaanishi kutoa lugha ya matusi, kashfa wala kejeli bali kutoa mawazo kinzani yenye lengo la kuboresha na kuijenga nchi ili kuleta maendeleo.

Anavitaka vyombo hivyo kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia huku vikijua wajibu wao wa kulinda mila, desturi na utamaduni na usalama wa kisiasa wa taifa hilo na si kuyahamasisha kwa kisingizio cha biashara.

Anawakumbusha kutumia kalamu zao kuandika mambo yanayojenga nchi kwa kuwa yakiandikwa mambo mabaya yakasomwa nje ya nchi sifa ya nchi nzima inaharibika na si ya mtu mmoja.

Anasema kongamano hilo litumike kujitathmini ni wapi wanafanya vyema na wapi hawafanyi vizuri na kupanga mikakati ya namna ya kujiboresha kwa manufaa ya vyombo vyao na nchi kwa ujumla.

Anasisitiza vyombo vya habari kufanya uchambuzi wa kina taarifa wanazozipokea kabla ya kuziandika kwa kuwa nyingi zimekuwa zikiandikwa kama zilivyo na wakati mwingine kuleta taharuki.

Anawahimiza wanahabari kuandika habari zinazokubalika na jamii badala ya kupata umaarufu na matokeo yake kuharibu hadhi ya mwandishi na chombo cha habari.

Anasema kuna baadhi ya waandishi wanachukua habari zilizoandikwa na mataifa mengine kuhusu nchi hiyo na kuziandika kama zilivyo bila ya kuzifanyia uchambuzi na kuwasihi kuwa wafafanuzi wa hoja kwa ajili ya kulinda hadhi zao wenyewe na nchi yao.

Anasema serikali haina budi kuweka mifumo ya kisera, kisheria na taasisi inayolenga kuimarisha uhuru wa mazingira kwa waandishi wa habari.

Anavishukuru vyombo hivyo kwa jinsi vinavyoshirikiana na serikali kutoa habari kwa umma kuhusu mambo yanayoendelea kwenye jamii ikiwamo harakati za maendeleo na hata majanga kama vile maporomoko ya Hanang’ na athari za mvua za El-nino zilitokea miezi michache iliyopita.

Kuhusu habari za vijijini, anasisitiza habari za vijijini ziripotiwe na vyombo vya habari vya jamii, wananchi wa maeneo hayo wapate kuzisikia, kwa kuwa taarifa nyingi zinaandikwa na vyombo vya kitaifa .

Anawaagiza wadau wa habari kuipelekea Serikali mapendekezo ya kuundwa kwa mkakati wa mawasiliano nchini ili kuboresha sekta hiyo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRi), Ernest Sungura, anataja changamoto zinazowakabili waandishi wa habari kuwa ni kufanya kazi bila mikataba na takwimu zikionesha kuwa ni asilimia 80 wanaishi katika hali hiyo tofauti na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.

Aidha, aliiomba serikali kupanua uhuru wa vyombo vya habari nchini ili kumpa uhuru kila mwandishi wa kutoa maudhui huku wakiimarisha misingi kusimamia maadili ya weledi katika kazi.

Akisoma Taarifa ya Hali ya Waandishi wa Habari, Utendaji na Uchumi wa Vyombo vya Habari nchini, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Tido Muhando, aliainisha mambo waliyoyaona kuwa ni changamoto katika vyombo vya habari ikiwamo kuidai serikali na sekta binafsi madeni makubwa na ya muda mrefu.

Anasema hali hiyo imesababisha vyombo hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati ikiwamo kuwalipa wafanyakazi mishahara na kulipa Kodi .

Aidha, anasema kutokana na hofu ya usalama wao, waandishi wa habari wameacha kuandika maudhui yanayolenga uwajibikaji na kudhoofisha waandishi kuzingatia uwajibikaji wa umma na kuwa na kizazi kisichofikiria sawa sawa, wengi wamebobea kwenye habari za burudani, vichekesho.

Kamati hiyo ilipendekeza pamoja na mambo mengine kuboreshwa kwa sera ya habari ili kuruhusu wawekezaji wa nje kumiliki hisa kwa asilimia 75, kwa sasa sera hiyo inaonyesha wawekezaji hao wanaweza kuwekeza chini ya asilimia 50. Ilipendekeza kuwapo na mfuko wa mafunzo kwa vyombo vya habari yatakayowezesha kuletwa kwa kampuni za nje za teknolojia kwa ajili ya mafunzo pamoja akili bandia itumike katika vyombo vya habari.