November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kwa nini hutakiwi kuondoa michango yako ya pensheni kabla ya kustaafu

Na Christian Gaya

WAFANYAKAZI wengi mara nyingi wamekuwa wakihama kutoka mwajiri mmoja hadi mwingine kwa ajili ya kupatia kipato zaidi na hatimaye kuwawezesha kuwapatia mkate wa kila siku familia zao.

Hivyo wafanyakazi wanatakiwa kuwa mwangalifu sana wakati wapo kwenye mpito wa namna hiyo wa kutoka kampuni moja na kujiunga na nyingine, na hapa mara nyingi wafanyakazi wengi wanashawishika kutaka kuondoa michango yao ya pensheni kabla ya wakati wake.

Na hapa ukiwa na mategemeo ya kuwa unakokwenda huko kwa mwajiri mpya utakuwa unaopata mshahara na marupurupu ya kutosha. Kinachotakiwa hapa ni kwenda kumwonesha mwajiri wako mpya kadi yako ya uanachama ili aendelee kuchangisha ili kutunisha pensheni yako ya baadaye.

Labda uwe umejipanga vizuri sana vinginevyo hiyo michango ya pensheni uliyochukua itaishia kutumika tu bila hata kuwekezwa kwenye kitega uchumi chochote.

Wakati mwingine unapochukua michango ya pensheni kabla ya wakati wake inaishia kukatwa faini kwa kuchukua kabla ya muda wake haujafika na kuanza kulalamika kwamba ni kidogo bila ya kujua ya kuwa huenda hata mahesabu yake yamelipuliwa na ndiyo inakuwa mwanzo ya magonjwa nyemelezi kama vile yanayotokana na msongo wa mawazo.

Kama mstaafu wakati wowote lazima unahitaji kuwa na fedha kwa ajili ya kukusaidia matumizi yako ya haraka. Kama vitega uchumi vyako vya kustaafu rasilimali ambazo zitachukua muda mrefu kuuzika au vinachukua gharama kubwa kubadilika kuwa fedha, itaharibu uwezo wako wa kupata fedha za kujikimu ili kulipa vitu muhimu kwa ajili ya maisha yako ya kila siku, kwa ajili ya matumizi yako ya siku za mapumnziko au kwa ajili ya mambo yasiyotabilika au hatarishi.

Kustaafu kunatakiwa kuwa ni wakati wa kukaa chini na kupumnzika na kuburudisha mwili na akili zako, ambapo kama una madeni hutaweza kuwa mtu wa kukaa chini tena kupumnzika na kujiburudisha kamwe. Na usipende kutegemea wana familia kukusaidia wewe na kuwa mzigo mtu tegemezi kwao badala ya watoto na wake zao. 

Anza kulipa madeni yako hasa yale makubwa kabla ya kustaafu kwako. Anza mapema kujiandaa na haya mambo kabla ya jua halijazama, usiaze wakati karibu unakaribia kustaafu, anza kubadilisha mtanzamo wako na kujiweka sawa kuanzia sasa.

Na unatakiwa kuwa makini na mwangalifu ikiwezekana anza kukwepa kuchukua madeni mapya na ukichukulia ya kuwa mapato yako yote yanategemea na kazi uliyoajiriwa nayo.

Tunatumia muda mwingi kwa ajili ya kufanya mipango ya baadaye, lakini tunajisahau juu ya maisha yetu yasiyotabilika. Je umesha andika Mirathi?  Kupanga mipango ya kufa ni mwiko kwa Afrika, na kwa watu wengi inaonesha ni kama unakaribisha kifo.

Ingawa, kuandika Mirathi ni njia mojawapo ya mwafaka ya kuwahakikishia kwa hao unaowajali sana katika maisha yako wakati wowote ya kwamba ndio watakaopatiwa endapo ukafikia mwisho wako hapa duniani.

Mirathi inakuhakikishia ya kwamba rasilimali zako hazitakaa hivi hivi wala kuoza wakati watu wanagombania mali zako. Anza na    mirathi rahisi kwanza ambayo unaweza ukawa unairekebisha au kuibadilisha kama madadiliko yeyote katika familia yako kama vile ya kuzaliwa, kifo au kuoa au kuolewa

Kuandaa mirathi inaweza kuonesha kama vile ni kitu kinachochukiza au kinachouzi, lakini hakuna kitachofanana wakati ambapo familia yako watakayopitia kama utakufa bila hata kuacha mirathi.

Hivyo kumbuka ya kuwa siku moja utastaafu, hutakuwa ukienda kazini kama ulivyozoea, hautakuwa na madaraka yeyote tena, hautakuwa na nguvu tena na pia utapungukiwa na nguvu ya ushawishi, na mzunguko wako wa pesa utapungua ghafla. Hivyo unatakiwa kuchunguza na fuatilia tarehe yako ya kustaafu kwenye risiti yako ya malipo ya mshahara na kwenye kumbukumbu zako mara kwa mara.

Unahitaji kutumia siku zako za likizo ya mwaka na kumbuka ya kuwa chochote utakachokifanya wakati uko likizo ndio utakachokifanya baada ya ukishastaafu.

Mfano kama unatumia likizo kulala au kuangalia luninga ndicho utakachokifanya baada ya kustaafu kwako. Unashauriwa kutumia vizuri wakati wako wa kustaafu hasa kwa kujishughulisha kwenye uzalishaji mali mara kwa mara. Unatakiwa kutumia wakati wako wa ziada kujifunza au kuboresha kipaji chako ambacho kitakuja kuwa na manufaa ukistaafu.

Unatakiwa kuwekeza kwa ajili ya pale utakapokuwa umestaafu tayari. Unashauriwa ya kuwa watoto wako sio uwekezaji kwa ajili ya kustaafu kwako kama ilivyokuwa wakati wa ujima, hivyo epuka kuwategemea watoto wala ndugu au marafiki kama benki yako ambayo inaweza kukupotezea heshima na utu wako katika jamii inayokuzunguka.

Jenga tabia ya kujitafutia shughuli unayoipenda au unayoifurahia kulingana na kipaji chako au ndoto zako wakati bado ungali kazini ili utakapofikia muda wa kustaafu ije ikusaidie kukuongezea kipato; kwa mfano unaweza kuanza kufuga kuku, au ukaanzisha biashara ya kumiliki duka. Hii itakusaidia kupata ujuzi unaojiuza na wala siyo vyeti visivyo na matumizi yeyote.

Kuongezeka kwa umaskini baada ya kustaafu kunamfanya mstaafu kufikiri kuwa kustaafu ni njia ya kuelekea kwenye hali ngumu ya kiuchumi, msongo wa mawazo, kutengwa na jamii, na kuumwa mara kwa mara na hatimaye kupoteza uhai kabla ya wakati wake.

kujiandaa kustaafu siyo kitu ambacho unaweza kuanza kufanya kabla ya wiki chache. Ni kitu ambacho unatakiwa kukifikiria kuanza kufanyia kazi mapema, inatakiwa mapema mara tu ya kuajiriwa na kuanza kufanya kazi kama ikiwezekana.

Hivyo kuustaafu ni moja ya nafasi ambayo inamwezesha mtu kutumia ujuzi wake, kuwa mjasiriamali na kuongeza kipato ili kuboresha maisha yake na ya watu wanaokuzunguka. Lakini wastaafu wengi huwa maskini zaidi kwa sababu kipato chao huisha mapema tu baada ya kustaafu.