Na Philemon Muhanuzi, Times Majira Online
BENARD Morrison ni raia wa Ghana anayecheza soka Tanzania kwa sasa. Kabla ya kuja hapa kucheza mpira alikuwa akichezea klabu ya Orlando Pirates ya kule Afrika ya Kusini. Ni mmojawapo wa wanasoka wa Ghana wanaocheza nje ya nchi yao kwa mafanikio.
Huko kwao sidhani kama wanamuona ni nyota mkubwa wa kupewa nafasi ya kutamba katika vichwa vya magazeti na runinga. Wanaopewa vipaumbele ni wale wanasoka wao wanaochezea ligi kuu za Italia, Hispania, Uingereza na Ujerumani.
Kwao wachezaji wa maana ni kina Thomas Partey wanaozungumzwa katika kipindi hiki cha msimu wa usajili cha Ulaya. Morrison huko kwao ni mchezaji wa kawaida sana.
Iwapo Black Stars inapocheza na Tunisia, Nigeria au Misri inaweza kuwa na wachezaji kumi na moja mpaka wale wa akiba pasipo mchezaji hata mmoja wa ligi ya Afrika kuwemo, huyu Morrison kwao ni wa kawaida mno.
Tatizo letu lenye kusitikisha halina uhusiano wa moja kwa moja na hizi habari za Simba na Yanga kuwa na vikao vya siku tatu kujadili hatima ya mchezaji wa kigeni kutoka Ghana.
Tunalo tatizo la kushindwa kuwa na kina Morrison wa kwetu, watakaogombewa huko Namibia, Zimbabwe au Malawi, na timu mbili maarufu huku mashirikisho ya soka yakiwa ni sehemu ya maamuzi ya suluhisho.
Farid Mussa kuja kuichezea Yanga akitokea Hispania wakati akiwa na umri mdogo ni habari mbaya lakini yenye sababu ya kuwa sehemu ya mijadala ya wapenda soka. Ni habari mbaya kumuona akikubali kushindwa wakati alishaanza kutazamwa na makocha wa Hispania.
Hata kama alikuwa anachezea timu ya daraja la pili. Kwanini arudi yeye na wanasoka wengine wa mataifa kama Ghana, Nigeria, Cameroon na mengine ya afrika magharibi hawarudi makwao mapema?.
Morrison kaja kimaslahi, amekuja kutafuta riziki na nguvu zake za kucheza soka zikianza kupungua atafikiria kurudi kwao. Morrison ni mpita njia tu, hajafikia ule ukaribu wake kwa nafsi zetu kama alivyo Farid Mussa.
Anaposhindwa kucheza soka lenye kutoka hatua moja kwenda nyingine akiwa huko Ulaya, maswali mengi wanayojiuliza wapenda soka yanakuwa ni ya msingi.
Na uzoefu unaonyesha kuwa utetezi wa kushindwa kwa Farid utakuwa sawa na utetezi wa kushindwa kwa Abdallah Shaibu.
Wote wawili watatetewa kwa kusema kwamba ipo mipango ya miezi michache ijayo ya wachezaji hao kurudi tena huko walipokuwa.
Hazitakosekana siasa za utetezi zenye kuhalalisha ujumbe kwamba wachezaji wetu hawajaonyesha kukua kiuwezo licha ya kupata muda wa kutosha wa kuwaridhisha makocha. Shaibu alishindwa Marekani na akaenda Ulaya Mashariki na kwenyewe akashindwa tena!.
Nauona umuhimu wa makocha wa kigeni wanaokuja kuwa ni wataalam wenye kutakiwa kuulizwa ni kipi tunatakiwa tufanye ili wanasoka wetu wasiendelee kushindwa kutoka hatua moja kwenda nyingine wakiwa huko nje.
Kwamba mpira wetu unawafaa sana makocha wa hapa hapa kwani wanawajua wachezaji wetu, wakati mwingine ni uhalalishaji wa kushindwa huko nje kwa hawa kina Shaibu na Mussa.
Wachezaji wetu wanazo hamu za kufika alipofika Mbwana Samatta, kusema kwamba waendelee kucheza katika mazingira ya kwetu tu ni kuahirisha utatuzi wa tatizo linaloendelea kuwepo mwaka baada ya mwaka.
Mwaka huu Farid Mussa anarudi nyumbani akiwa bado ni kijana kiumri na kimuonekano, miaka michache ijayo atakwenda Ulaya kijana mwingine na kurudi nyumbani akiwa bado hajafanikisha jambo lolote la uwanjani na katika maisha yake binafsi.
Habari ya Morrison kugombewa na timu mbili za Kariakoo kwangu ni ya kawaida kulinganisha na ile ya wanasoka wetu wanaokwenda Ulaya kushindwa na kurudi nyumbani tena wakiwa vijana wadogo.
Kwanini wanashindwa kusonga mbele?. Kigezo kipi ambacho hawana ili kifanyiwe kazi na wao waweze kuwa sawa na vijana wa mataifa mengine ya Afrika?.
More Stories
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship
Mnzava apania kuwapeleka vijana Simba na Yanga