January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KUWASA kutekeleza miradi ya maji ya Bilioni 49.7

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Kigoma

Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) inatekeleza miradi mbalimbali ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 49.7 .

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma na Ufuatiliaji wa Wizara ya Maji, Mhandisi Lyidia Joseph wakati akizindua Bodi mpya ya muhula wa saba ya KUWASA baada ya ile ya awali iliyoanza kazi Julai 2016 muda wake kumalizika Juni 2019.

Akizindua Bodi hiyo mpya, Mhandisi Lyidia amesema kuwa, zipo changamoto zinazohitaji utatuzi na kuitaka bodi hiyo mpya kujipanga na kuendeleza jitihada zilizofikiwa na bodi iliyopita ili kuhakikisha misingi ya uendeshaji wa mamlaka inaimarika.

Amesema, Serikali imejipanga kumaliza changamoto ya huduma ya maji mkoani Kigoma ambapo ipo miradi inayotarajiwa kuanza ambayo itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.8, ikiwemo ujenzi wa kitekeo kipya cha maji katika eneo la ufukwe la Amani, ukarabati wa
miundombinu ya mradi wa maji Mwandiga na mradi wa uondoaji majitaka Manispaa ya Kigoma.

Pia Bodi mpya ya KUWASA imetakiwa kutumia nyenzo iliyokabidhiwa kuwa kichocheo katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu, ikiwemo Sheria ya Maji Na. 5 ya mwaka 2019, na Mpango wa Biashara wa Mamlaka kwa mwaka 2019/2020-2021.