Judith Ferdinand
Imeelezwa kuwa zaidi ya asilimia 70 hadi 90 ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa Sikoseli(selimundu)hupoteza maisha ndani ya kipindi cha miaka mitano ya mwanzo ya maisha yao.
Hii ni kutokana na kutotambulika,unyanyapaa na kukosa elimu na uelewa juu ya ugonjwa huo pamoja na imani potofu ambayo imejengeka ndani ya jamii.
Wazazi na wananchi wanena
Mmoja wa wazazi wenye watoto wenye ugonjwa wa Sikoseli ambaye akutaka jina lake liandikwe ameeleza namna changamoto wanayopitia katika kuwahudumia watoto wenye ugonjwa.
Anes Shukuru siyo jina lake halisi ameeleza alipo mzaa mtoto wake alikuwa anaumwa mara kwa mara na ukuaji wake ulikuwa ni wa taratibu licha ya kuwa alikuwa anajitahidi kumpatia lishe lakini jamii iliokuwa inamzunguka iliamini katika Imani za kushirikiana na mara nyingi walimsisitiza ampeleke kwa Mganga wa kienyeji kuwa atakuwa amerogwa.
Hivyo kutokana na jamii pamoja na yeye kutokuwa na uelewa juu ya ugonjwa huo alichelewa kumpeleka hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
“Mtoto wangu aliteseka na ugonjwa huu kabla ya kifo chake kwani mara nyingi alikuwa anaumwa na kumpeleka hospitali hali iliyochangia kushindwa kuhudhuria masomo kwa wakati mpaka umauti umemfika lakini ameteseka,naomba elimu itolewe kama kuna namna ya kuweza kusaidia kutozaa watoto wenye changamoto hii,”anaeleza.
Naye Neema Emmanuel mmoja wa wakazi wa jijini Mwanza ameeleza kuwa aliwai kushuhudia mtoto wa jirani yake ambaye anasumbuliwa na ugonjwa huo lakini akujua kama ni sikoseli.
“Kutokana na kutokua na uelewa wa ugonjwa huu awali nilijua jirani yangu atakuwa ‘amembemenda’ ndio maana mtoto huyo alikuwa anaumwa mara kwa mara pia ata ukuaji wake haukua vizuri,”anaeleza Neema.
Hivyo anaiomba serikali na wadau wengine kuendelea kutoa elimu juu ya ugonjwa huo ili kuweza kuwakoa watoto wanaosumbuliwa na sikoseli kwa jamii kuwa na elimu ya kutosha na kuacha kukimbilia imani potofu ambazo zinaweza kusababisha mtoto akapoteza maisha.
Taasisi ya Mashujaa wa Sikoseli Tanzania yanena
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mashujaa wa Sikoseli Tanzania(Tasiwa) Priscilla Chassama,aneleza kuwa walianzisha taasisi hiyo mwaka 2018 kwa lengo la kutoa elimu kwenye jamii juu ya ugonjwa huo.
“Tuligundua kuwa ugonjwa huu wa sikoseli unaendele kwenye jamii kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya ukosefu wa elimu,elimu pekee ndio itatufanya tuweze kukata mnyororo wa sikoseli kwenye jamii na kupunguza ugonjwa huu kwenye kizazi chetu nchini,”anaeleza Chassama.
Sikoseli ni nini
Chassama anaeleza kuwa Sikoseli ni ugonjwa wa kurithi ambapo baba na mama wanachangia kumzaa mtoto mwenye ugonjwa huo.
Anaeleza kuwa kumekuwa na mifarakano kwenye familia kwa sababu ya kuzaliwa mtoto mwenye Sikoseli baba na mama wanagombana.
“Baba anasema huyu mtoto siyo wangu ,sisi kwetu hatuna matokeo yake mtoto analelewa na mzazi mmoja mama anaachiwa mzigo wa kulea pekee yake ndio maana tunatoa elimu ili jamii itambua kuwa sikoseli ni ugonjwa wa kurithi kutoka pande zote,”anaeleza Chassama.
Hivyo jamii inapaswa kutambua kuwa familia inatakiwa kushirikiana kumlea mtoto huyo kwasababu wote wamechangia akazaliwa akiwa na sikoseli.
Pia anaeleza ugonjwa huo ni ulemavu wa damu kwani ile itilafu ambayo ipo kwenye damu yao ndio tunapata jina la selimundu.
“Ile damu yao badala ya kuwa na umbo la duara inakuwa na umbo kama nusu mwezi ndio maana tunaita sikoseli yani seli iliyojikunja na kwa Kiswahili tunaita selimundu,” anaeleza Chassama.
Sababu ya wagonjwa wa sikoseli kupunungiwa damu na madahara yake
Anaeleza kuwa kutokana na seli kujikunja . ndio inaleta madhara kwa wenye ugonjwa huo ikiwemo kusababisha upungufu wa damu kwa sababu inavunjwa sana kitu ambacho siyo sawa mwilini.
Pia inasababisha maumivu makali ya viungo na sehemu mbalimbali za mwili kwa sababu zile seli zinatabia ya kukwama kwenye mishipa ya damu.
“ Siyo kama seli ya kawaida ambayo inaweza kujiminya kwaio inaweza kumsababishia maumivu tunaona mtu mwingine anapata maumivu ya miguu,mikono na maeneo mengine na hiyo seli ikikwama kwenye mishipa ya kichwani inaweza kusababisha mwenye ugonjwa huo kupata kiarusi,”anaeleza Chassama.
Lakini pia anaeleza seli hiyo ikikwama kwenye mapafu mtu anaweza kupata lemonia ya sikoseli pia ugonjwa huo unasababisha ukuaji duni kwa watoto kwasababu haibebi oksijeni ya kutosha kupeleka sehemu mbalimbali za mwili ili kufanya mtoto aweze kukua vizuri.
“Hayo yote ni madhara ambayo anayapata mtu mwenye sikoseli kutokana na ile seli jinsi ilivyo,”anaeleza.
Jamii inazungumziaje ugonjwa wa sikoseli
Chasama anaeleza kuwa ndani ya jamii kuna mambo mengi ambayo wamekuwa wakisema juu ya mtu mwenye ugonjwa huo ikiwemo kuwa hawezi kuishi siku nyingi kwamba akifikisha miaka 18 anafariki.
Ambapo ameeleza kuwa hayo yote ni Imani potofu kwani ukweli ni kuwa mtu mwenye sikoseli anaweza kuishi miaka mingi isipokuwa familia husika na jamii iwe na tabia ya kufuata huduma za afya wanapogundua kuwa wana mtu mwenye ugonjwa huo.
Kwa kumpeleka hospitali kwa muda muafaka na kwa kufanya hivyo watakuwa wamempunguzia maumivu na madhara yanayotokana na ugonjwa huo na kuongeza kiasi cha maisha yake.
“Umeisha jua kuwa mwanangu mimi ana sikoseli anaumwa macho ya njano,anaishiwa damu unampeleka kwa mganga wa kienyeji hawezi kuishi na hotofika umri fulani kwa sababu haumtafutii matibabu sahihi,tunashauri kufuata matibabu sahihi ya hospitali,”anaeleza.
Aidha anaeleza kuwa hospitali mtoto anapimwa na kupewa vidonge vya folic acid kila siku hiyo ni kwa watoto na watu wazima,vitamin D kwa ajili ya kuwasaidia katika vitu mbalimbali kama mifupa.
Pia anaeleza kuwa kuna dawa nyingine ya hydroxyurea ambayo ni nzuri na inawasaidia watoto wenye sikoseli pia watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanapewa penicillin v ambayo pia inawasaidia na maumivu ya kifua.
“Wanapimwa ini,figo hivyo vyote vinawasaidia kuendelea kuishi vyema tukigundua kuwa figo inashida tayari jambo hilo litapatiwa ufumbuzi haraka kuliko kuwa nyumbani tayari hawezi hata kutembea,”anaeleza na kuongeza kuwa
“Au bandama imevimba mlete hospitali angefanyiwa upasuaji na ikatolewa na angeendelea na maisha ila wewe umekaa naye tu nyumbani,hiyo imani ambayo kwenye jamii walikuwa wanasema watoto wenye sikoseli hawaishi siku nyingi ni kwasababu walikuwa hawawapi matibabu sahihi,”.
Hivyo anaeleza kuwa kikubwa jamii inapaswa kumtia moyo mtoto mwenye sikoseli na kumpatia matibabu sahihi ili aweze kutimiza ndoto zake pia wanaweza kupata watoto na kuwa watu fulani katika jamii.
“Wenye sikoseli wanazaa vizuri isipo kuwa akiwa na ujauzito na anajua ana changamoto ya ugonjwa huo muda wowote anaweza kupungukiwa damu kuwa karibu na kituo cha afya na daktari ambaye anaujua ugonjwa huo vizuri,”anaeleza.
Sanjari na hayo anaeleza kuwa kutokana na changamoto hizo na imani potofu iliyojengeka katika jamii dhidi ya ugonjwa huo ndio maana wameamua kutoa elimu ili kupunguza vifo vya watoto wenye sikoseli.
Anaeleza kuwa mpaka sasa wanatoa huduma kwa watu zaidi ya 300 hivyo serikali itafute namna ya kufanya kampeni kwenye jamii hasa vijijini na kuhakikisha elimu juu ya sikoseli inawafikia ipasavyo .
“Tumewafikia watu wa vijini kwa baadhi ya Wilaya tatizo ni kubwa mfano tulienda Busega tuliwapima watu 365 kati yao nusu yake walibainika kuwa na ugonjwa ya sikoseli wengine wana chembechembe na wachache wao wakiwa hawana chembechembe wala sikoseli hapo utaona jinsi gani ugonjwa huu ulivyo mkali hivyo tunaendelea kutafuta fedha ili kuyafikia maeneo mengine ya vijijini,”anaeleza.
Je ni kwa namna gani mtoto anarithi sikoseli
Chassama anaeleza kuwa ili mtoto azaliwe na chembechembe za sikoseli au ugonjwa wenyewe lazima wazazi wawe na ugonjwa huo au mmoja akiwa na vinasaba vyenye vimelea vya ugonjwa huo.
Anafafanua kuwa mtu mwenye vinasaba vya Hb AA maana yake ni mzima hana sikoseli wala vimelea lakini wa Hb AS-ana vimelea au vinasaba vya sikoseli na mwenye Hb SS ana sikoseli.
Hivyo mzazi mmoja akiwa na vimelea vya ugonjwa huo na mwingine hana wanaweza kuzaa mtoto mwenye vinasaba vya ugonjwa wa sikoseli lakini kama wazazi wote wamebeba chembechembe za ugonjwa wa sikoseli mtoto atazaliwa akiwa na ugonjwa huo.
Pia anaeleza kuwa kutoka na jamii kutokuwa na tabia ya kupima kujua kama ana vinasaba vya sikoseli ndio chanzo cha kuibua migogoro ndani ya ndoa baada ya kuzaliwa mtoto mwenye ugonjwa huo.
Ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo Chasama anaeleza kuwa elimu juu ya ugonjwa sikoseli inapsawa kutolewa zaidi huku iwe na tabia za kupima afya zao kabla ya kuingia katika ndoa ili wajue hali ya vinasaba vyao.
“Usiolewe au kuoa tu kabla ujajua hali ya vinasaba vyako na hata yule ambaye utaingia naye kwenye ndoa apime ili kujua kama vinasaba vyake vipoje kabla hamjapata mtoto, elimu pekee yake ndio itapunguza au kumaliza tatizo la sikoseli kwani watu watakuwa na uelewa na kujua umuhimu wa kupima afya zetu,”anaeleza Chassama.
Dakitari aeleza ukubwa wa tatizo.
Akizungumza na Timesmajira Online Daktari Bigwa wa Magojwa ya Watoto Hospitali ya Rufaaa ya Kanda Bugando Emmanuela Ambrose anaeleza kuwa tatizo la ugonjwa huo ni kubwa.
Ambapo tafiti zinaonyesha dunia nzima tatizo kubwa lipo Afrika asilimia 75 ya watoto wanaozaliwa na sikoseli wamenukuliwa kuzaliwa barani Afrika na Tanzania ni nchi ya tano.
Anaeleza vkuwa japo imeshika nafasi ya tano bado taarifa zinasema ina wagonjwa wenye sikoseli mpaka sasa zaidi ya watoto 14000 uzaliwa na ugonjwa huo nchini wengi wao wakitokea Kanda ya Ziwa.
Anaeleza kuwa katika hospitali hiyo ina zaidi ya watoto 1000 ambao wanahudhuria kliniki kwa mwaka.
Ambapo kila siku ya Jumatatu wanawaona watoto 30 hadi 50 huku Ijumaa wakiwaona watoto 50 hadi 80.
Pia wanatoa ushauri na kuongea na wazazi jinsi ya wao kuwa ndio chanzo cha watoto hao kupata ugonjwa huo na nini wakifanye ili kuepuka kupata mtoto mwingine mwenye tatizo hilo.
Anaeleza kuwa bado utafiti mkubwa unahitajika ili kueleza bayana ukubwa wa tatizo hilo kwani ugonjwa huo kwa sasa umekuwa ni mada kubwa kwa sababu watoto wengi wanazaliwa wakiwa na shida hiyo.
Pia Ambrose anaeleza kuwa ukubwa wa tatizo hilo unachangiwa na watu kutokuelewa kama wamebeba chembechembe za ugonjwa huo wanatambua tu pale wanapopata mtoto.
Hivyo kusubili mpaka upate mtoto ni kuchelewa wanapaswa watambue hali zao kabla ya kubeba ujauzito kama ana chembechembe aolewe na mtu asiye na chembechembe.
“Ni vyema wakapima kabla ya kuingia kwenye ndoa lakini mtoto anapozaliwa akapimwa akakutwa na tatizo hilo anaanzishwa kliniki na matibabu mapema ambayo yatamsaidia kutibu matatizo yote yanayotokana na ugonjwa huo hivyo kumfanya kuishi muda mrefu,”anaeleza.
Akizungumzia suala la matibabu anaeleza kuwa ni ghali inamlazimu mzazi awe na fedha hasa kwa wale walio juu ya miaka mitano japokuwa serikali inatoa dawa aina ya Hydroxyurea inayosaidia kuwapunguzia shida zinazotokana na sikoseli ikiwemo maumivu.
Pamoja na kulazwa mara kwa mara damu yao kubaki juu na kuzuia kupata kiharusi(kupooza)pia kipindi mtoto anapozaliwa akiwa na shida anaanzishiwa Folic Acid inayosaidia uzalishaji wa damu, au Penicillin V inayozuia vifo hasa chini ya umri wa miaka mitano na akifikisha miezi tisa anaanza kutumia Hydroxyurea inasaidia kulainisha damu kuwa nyepesi.
“ Kupandikiza uroto ndio tiba lakini ni gharama sana pia lazima uroto huo utoke kwa ndugu yako unayeendana naye hapa nchini ni watoto wanne tu wamefanyiwa na wote walitoka salama lakini na imani wengi zaidi watafanyiwa endapo serikali itapunguza gharama,”anaeleza Dkt.Ambrose na kuongeza kuwa
“Ni vyema somo la sikoseli likaingizwa kama somo kwenye elimu ya afya itaongeza tija pia upimaji ufanyike shuleni ili watoto wajue hali yao na elimu hiyo itawasaidia kutambua hatari iliyopo mbele yao na watakuwa makini,”.
Pia anaeleza njia nyingine ya kukabiliana na ugonjwa huo mama mjamzito aanzapo kilinki apimwe hali yake akionekana amebeba chembechembe iandikwe kwenye kadi yake AS (ana chembechembe za sikoseli), SS ( ana sikoseli) na AA( mtu asiyekuwa na chembechembe wala sikoseli).
“Watoto wote watakaozaliwa na mama mwenye SS au AS lazima wapimwe hali zao itasaidia,” anaeleza.
Siri ya sikoseli Kanda ya Ziwa
Dkt.Ambrose anaeleza kwa kusimulia sababu ya Kanda ya Ziwa kuwa na sikoseli ni kuwa zamani hakukuwa na ugonjwa wa maralia duniani.
Ulivyokuja uliua watu wengi kwa sababu dawa mara nyingi ugundulika baada ya ugonjwa na uchukuwa muda hivyo vifo vilivyotokana na maralia vilikuwa vingi hasa nchi za Kitropikia ndizo zilikuwa na ugonjwa huo.
Katika kipindi hicho mwili ulitengeneza kinga ya kupingana na maralia na ndipo mwili ulitengeneza hitilafu kwenye damu.
Anaeleza kuwa malaria ilikuwa inavunjavunja damu na hitilafu iliyojitokeza mara ya kwanza hawakujua kama ni sikoseli lakini wale watu waliokuwa wamepata hiyo hitilafu na wakaja kuoana ndipo kuliibuka kesi za sikoseli .
Pia anaeleza sababu za kuongezeka kwa ugonjwa huo ni kwamba wale watu walikuwa na hitilafu waliweza kupingana na malaria ata wenye chembechembe lakini wale ambao hawajathiriwa walipoteza maisha sana.
Hivyo ongezeko la watu wenye chembechembe na sikoseli ikakuwa na wakaanza kuoana na tatizo ilo likaendelea kuwepo.
Akisimulia chanzo cha tatizo hilo kuenea katika maeneo mengine anaeleza kuwa zamani mtu akiwa Mwanza anaoa Mwanza na ukioa sehemu nyingine unakataliwa tofauti na sasa mtu anaweza kuoa sehemu yoyote.
Hiyo inatokana mtu anatoka Kanda ya Ziwa anaenda kufanya kazi Iringa au Mbeya kumbe ana sikoseli akioa huko na wakipata mtoto anakuwa na shida hiyo ,hivyo ndio maana ugonjwa huo umeenea nchini.
“Ndoa za mitala ndizo zinaleta sikoseli na ukanda wa Kitropikia hasa Mwanza ina malaria sana na mtu mwenye sikoseli kamwa hawezi kuumwa ugonjwa huo kitu cha muhimu ni kufanya vipimo kabla ya kuoana,”anaeleza na kuongeza kuwa
“Ikibainika mna sikoseli bora msioane ni bora mkaendelea kuwa marafiki kuliko kuja kukitesa kiumbe kitakacho kuja inashauriwa mtu mweye sikoseli ama chembechembe ni vyema akaolewa na mtu asiyekuwa na sikoseli ama chembechembe hizo,”.
Hatua za serikali katika kudhibiti ugonjwa wa sikoseli
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu anazitaka akizindua kampeni ya kuelimisha jamii juu ya Magonjwa Yasiyoambukiza iliyofanyika Oktoba 2,2023 katika Hospitali ya Sinza – Palestina jijini Dar es Salaam alizitaka hospitali zote za Halmashauri nchini kuwapima ugonjwa wa Sikoseli watoto wote wanaozaliwa katika Hospitali hizo ili kujua hali zao mapema na kuanza matibabu.
“Waganga Wakuu wa Mikoa mkalisimamie hili nataka Hospitali zote za Halmashauri nchini ndani ya Miezi Sita zipime ugonjwa wa Sikoseli kwa watoto wanaozaliwa katika Hospitali hizo kabla sijashuka vituo vya Afya”. Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 70 hadi 90 ya watoto wanaozaliwa na Sikoseli hupoteza maisha ndani ya kipindi cha miaka mitano ya mwanzo wa maisha yao kutokana na kutotambulika au kwa sababu ya unyanyapaa na kukosa elimu.
“Hali hii haikubaliki ni lazima tuchukue hatua za haraka ili kuokoa maisha ya watoto wachanga wenye ugonjwa wa Sikoseli kwa kuwatambua mapema ili kuhakikisha wanapata matibabu kwa wakati.
Waziri Ummy anasema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa fedha za dawa kwa asilimia 100 kila mwezi, fedha hizo wanaruhusiwa kuzitumia kwa ajili ya kununua mashine za kupima ugonjwa wa Sikoseli.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika