Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Mlazindizi
ALIYEKUWA mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Amina Ally Kurupe, amesema hajakasirika kuondolewa kwenye mpango huo, kwani ameachiwa mradi wa kumuingizia kipato.
Aidha, amesema hawezi kukasirika, kwani hatua hiyo inatoa nafasi kwa watu wengine kufaidika kupitia TASAF.
Kurupe mkazi wa Mlandizi, Kata ya Mtongani, mkoani Pwani ni miongoni mwa waliohitimu wa mpango huo baada ya hali zao za kiuchumi kuimarika, hivyo kuwa na uwezo wa kujiingizia kipato cha kuendesha maisha yao.
Akizungumza wiki hii, Kurupe ambaye ni mama mwenye ulemavu alisema ruzuku aliyokuwa akipata kutoka TASAF ikiwemo ya uzalishaji imemuwezesha kuanzisha mradi wa kuzalisha batiki.
Alisema kabla ya kujiunga kwenye mpango wa TASAF, alikuwa anafanya biashara ndogo ndogo ya kuuza karanga mbichi na kavu pamoja na ubuyu na kwenda kuuza maeneo ya vijiweni.
“Baada ya kuingizwa kwenye mpango wa TASAF nilianza kupata ruzuku na niliweza kuanzisha mradi wa kutengeneza batiki, huku nikiendelea mradi wangu karanga kwa ajili ya kuendeleza maisha yangu,” alisema Kurupe na kuongeza;
“TASAF imenisaidia kwa sababu nilikuwa napata ruzuku kila mwezi na ilinisaidia kukidhi mahitaji yangu na kama nilikuwa na madeni madogo madogo, niliweza kuyalipa.”
Alisema mradi huo wa batiki, umemwezesha kuwa na akiba. “Nashukuru kwani ruzuku ya uzalishaji ndiyo imeniwezesha kuanzisha mradi ya batiki.
Mtaji wangu jumla yake ni kiasi cha sh. 500,000 na ruzuku ya mwisho ya uzalishaji niliyopata nilinunulia vifaa kwa ajili ya uzalishaji batiki, kuanzia kununua vitambaa hadi vitendea kazi vyake,” alisema.
Kuhusu kuondolewa kwake TASAF, alisema hajakasirika, kwani ameachiwa mradi, japo changamoto anayokabiliana nayo ni kukosa wateja wa uhakika.
More Stories
LGTI yaunga mkono juhudi za Dkt.Samia matumizi nishati safi nchini
Wawili wadakwa na polisi tuhuma za kumuua Mwenyekiti UVCCM
Uganda yafurahishwa utendaji kazi,maabara ya GST na Masoko ya Madini