Na Penina Malundo, Timesmajira
Methane ni mojawapo ya gesi za Hydrocarbon ambayo ni gesi inayochangia ongezeko la joto duniani na huzalishwa katika usafirishaji na uzalishaji wa makaa ya mawe, gesi asilia na mafuta. Mifugo, maeneo ya kutupa taka na tabia za kilimo .
Sifa mbaya ya gesi ya methane ni gesi chafu yenye uwezo wa kuongezeka kwa joto dunian kama tafiti mbalimbali zinavyosema , gesi hii ya methane inasambaa dunia mara 23 kuliko gesi ya Kaboni dioksidi.
Katika Mkutano wa COP26 huko Glasgow ,Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, alisema Methane (CH4) ni mojawapo ya gesi ambazo tunaweza kupunguza na ikipunguzwa itapunguza mara moja ongezeko la joto duniani.
Pia alikumbusha kuwa gesi hii inahusijka kwa karibu asilimia 30 ya ongezeko la joto duniani tangu Mapinduzi ya Viwanda.
Umoja wa Ulaya na Marekani wamekuwa wakifanya kazi juu ya makubaliano haya ya kupunguza uzalishaji wa Methane ambapo nchi nyingi zimejiunga na juhudi hizi kama vile Canada, Korea Kusini, Vietnam, Colombia na Argentina.
Aidha Watanzania nao wameonekana kuunga mkono kwa kiasi kikubwa mipango inayolenga kupunguza uzalishaji wa gesi ya methane na kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa.
Hatua hii imekuja baada ya utafiti uliofanywa na Global Methane Hub, Shirika la Kibinadamu linalojitolea Kupunguza Uzalishaji wa Methane Duniani ambapo ni utafiti ulijumuisha nchi 17 katika mabara sita, umetoa ufahamu wa jinsi jamii inavyoiona hali ya mazingira na njia za kisheria za kurekebisha hali hiyo.
Matokeo ya utafiti huo yanaonesha kwamba asilimia 83 ya washiriki kutoka Tanzania wanapendelea sera zinazolenga kupunguza uzalishaji hatari wa methane, na kati yao, asilimia 49 wanatoa uungaji mkono mkubwa, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuliko nchi nyingine zilizofanyiwa utafiti.
Zaidi ya hayo, asilimia 87 ya Watanzania wanaamini kwamba shughuli za binadamu ndio sababu kuu ya mabadiliko ya hali ya hewa, ikionesha ufahamu mkubwa wa umuhimu wa kuchukua hatua za kupunguza athari hizo.
Utafiti huo pia unaonesha kwamba asilimia 88 ya washiriki kutoka Tanzania wanapendelea sheria zinazolenga kupunguza upotevu wa chakula na utupaji sahihi wa taka za kikaboni, ambazo ni moja ya vyanzo vikuu vya uzalishaji wa methane.
Marcelo Mena, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Methane Hub,anasema kupunguza uzalishaji wa methane ni njia ya haraka zaidi ya kupunguza ongezeko la joto duniani na kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Anasema utafiti walioufanya unaonesha kwamba wale wanaoathiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa ndio wanaotoa uungaji mkono mkubwa kwa jitihada za kupunguza methane.
‘’Utafiti huo unathibitisha kwamba uungaji mkono wa mikakati ya kupunguza gesi ya methane umebaki imara licha ya tofauti katika ufahamu wa awali wa gesi hiyo katika nchi zilizofanyiwa utafiti.
‘’ Hata hivyo, wasiwasi mkubwa umeelekezwa kwa suala la ubora wa maji, ambapo asilimia 76 ya washiriki kutoka Tanzania wameripoti wasiwasi mkubwa kuhusu hilo,’’anasema.
Anasema utafiti huo uliwafikia watu katika nchi 17 kote ulimwenguni ambao wanatoka katika mabara sita, ukikusanya data kutoka kwa watu wazima 12,976, takriban 750 kutoka kila nchi.
Makamu wa Rais wa kampuni ya BSG,Natalie Lupiani, anasema kwamba takwimu hizo ni ishara nzuri kwamba watu wanaunga mkono serikali zao katika kuchukua hatua za kuwalinda dhidi ya ongezeko la joto duniani.
Anasema Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi tatu zilizoathiriwa zaidi, pamoja na Brazil na Kenya, huku karibu nusu ya washiriki wakiripoti athari kali katika maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jopo la Kitaalam la Sayansi la Hali ya Hewa na Hewa Safi (The Climate and Clean Air Coalition Scientific Advisory Panel), Drew Shindell, anasisitiza umuhimu wa kupunguza uzalishaji wa methane mara moja ili kuzuia jamii dhidi ya athari mbaya za uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Anasema ripoti hiyo ya utafiti inaonesha kuwa kupungua kwa kiasi kikubwa cha ongezeko la joto kunaweza kutokea kupitia juhudi za kupunguza methane kwa asilimia 45, ambayo itasaidia kuleta mustakabali bora na kufikia malengo ya kimataifa ya hali ya hewa.
‘’Utafiti huo unaonesha kwamba watu duniani kote wanaona serikali za kitaifa, biashara, na watu binafsi kuwa wajibu wa uharibifu wa mazingira, lakini kuna imani kubwa kwamba biashara kubwa na serikali zinaweza kuleta mabadiliko muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa,’’anasisitiza.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika