Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Wanawake wa vitongoji 11,kijiji cha Kitumba Kata ya Kisesa, wilayani Magu mkoani Mwanza,wanatarajia kuondokana na changamoto ya ukatili waliokuwa wanakutana nayo wakati wa kutafuta nishati ya kuni porini kwa ajili ya kupikia.
Hiyo ni baada ya kampuni ya Chabri Energy,inayojihusisha na utengenezaji wa majiko banifu na kuni mbadala(kuni smart), kugawa majiko bunifu 250 kwa wanawake wa vitongoji 11, yenye thamani milioni 17.5, lengo ikiwa ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Wakizungumza katika kampeni hiyo ya utoaji wa majiko hayo iliofanyika Februari 28,2025, katika kiwanda hicho cha Chabri Energy Co.LDT,wanawake hao wameelezea adha waliokuwa wanaipata wakati wa kutafuta kuni na namna majiko hayo yatakavyo wasaidia.
Mkazi wa kitongoji cha Igudija ‘B’,Grace Mathias, amesema,”Athari tulizokuwa tunazipata kwa upande wa utafutaji wa kuni ni kubakwa.Unaweza kuingia kwenye pori kutafuta kuni ukajikuta unavamiwa na kundi la wanaume usiowajua na kuweza kukufanyia kitu kibaya,cha ajabu na kukuletea athari katika maisha yako,”.
Ofisa Mtendaji Kijiji cha Kitumba Leticia Missungwi, amesema,wanawake wengi walikatwa mapanga na kuuwawa kutokana na kutumia kuni,hivyo akiwa mzee akawa na macho mekundu jamii ilikuwa inamchukulia kama mchawi.
“Matokeo yake inamkata mapanga bila kupata maelezo rasmi kwamba aidha ni ugonjwa au vitu fulani vilisababisha yeye kuwa na macho mekundu,”.

Amesema,ujio wa ‘kuni smart’,utawasaidia wanawake kupikia kwa haraka,hivyo wanajivunia uwepo wa mradi wa majiko hayo katika eneo lao.Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Magu,Ofisa Tarafa Sanjo,Perpetua John,amesema,athari ni moshi unaotoka kwenye kuni unaweza kusababisha mtoto wa jicho na upo uwezekano wa kupofuka jicho,vile vile macho yanakuwa mekundu na kusababisha kuitwa mchawi,
Hata hivyo Mkazi wa kitongoji cha Igudija ‘B’,Sprina Kagose, amesema,atahamasisha wanawake wenzake kuacha kukata miti ovyo,kutunza uoto wa asili na misitu kwa ajili ya kupata mvua.
“Kinachosababisha kukata miti ovyo, ni kutokana na kipato kuwa duni,hivyo mazingira yanapokuwa magumu inabidi mama wa familia popote uhusike kutafuta kuni ili watoto waweze kula,hivyo watakapotumia majiko banifu na kuni mbadala hatuta kata tena miti,”amesema Sprina.
Ofisa Masoko kutoka kampuni ya Chabri Energy,Diana Godwin, amesema wanatengeneza ‘kuni smart’,kwa kutumia malighalifi za taka kavu, lengo ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Ni wakati sasa kila Mtanzania kutumia nishati mbadala ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.Tumetumia mkaa kwa muda mrefu,tumeharibu mazingira sana,ni wakati sasa wa kurudisha Tanzania yetu kuwa katika hali ya kijani,tumtumie nishati mbadala ili tuepuke kukata miti na kuharibu mazingira,”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Chabri Energy, Bernard Makachia, amesema,wanahamasisha watu juu ya matumizi ya nishati mbadala kwa kuwapa majiko,ili iwe chachu ya kutumia ‘kuni smart’,ambazo ni rafiki kwa mazingira na zinalinda afya za jamii.
Amesema kwa siku walikuwa wanazalisha tani tano za ‘kuni smart’ kupitia mashine ndogo ,na kwa sasa amefunga mashine kubwa ambayo itakuwa na uwezo wa kuzalisha tani kumi kwa siku na hivyo wanatarajia kuongeza uzalishaji na kufikia tani 15 kwa siku.
“Hatutegemei kukata miti kutengeneza kuni hizi,tunatumia taka kavu kama nyasi kavu,maranda,magunzi na vifuu vya nazi.Malighafi ni nyingi hatuwezi kuzimaliza na tunazichukua kuonesha watu kuwa taka ni nishati.lengo ni kuhamasisha watu kuwekeza na kutumia nishati safi,”.

Naye Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Mradi wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP), Jolson Masaki, amesema,shirika hilo limeiwezesha kampuni ya Chabri Energy,upande wa nishati safi ya kupikia ambapo wameweza kuja na ubunifu wa majiko hayo na kuni hizo,ambazo zinapunguzaa kiwango cha moshi uliokuwa una waathiri wanawake.
“Kuni smart, moja inauwezo wa kupika chakula cha watu kumi,tutakuwa tumeokoa miti hivyo kupunguza ongezeko la joto lililopo sasa.Tumtumie mbadala wa nishati ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kutimiza lengo la Serikali la kufikia asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,”.

Ofisa kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Collin Lwanga, amesema,Mei mwaka 2024,ulizinduliwa mkakati wa miaka 10(2024-2034),wa nishati safi ya kupikia wenye lengo kufikia asilimia 80, kwani kipindi hicho ilikuwa chini ya asilimia 10,ambapo Chabri Energy wamekuwa miongoni mwa kufanikisha mkakati.

More Stories
Zaidi ya bilioni 1.1 kunufaisha vikundi 60 Ilemela
WMA wawakamata watu wawili kwa tuhuma za kutumia mizani isiyo sahihi
Serikali:ARVs zipo za kutosha watanzania msiwe na hofu