January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Songea-Namtumbo wajivunia fursa za kiuchumi kupitia mradi wa barabara

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WATAALAM wa masuala ya uchumi na fedha wanasema barabara ni kati ya nyenzo muhimu za kupunguza umasikini na kuongeze kipato cha mwananchi kuanzia wa shambani anayelima mazao mpaka wa kiwandani zinakozalishwa bidhaa.

Ripoti iliyochapishwa na Shirika la fedha Duniani (IMF), Juni mwaka huu, inaonyesha ubora wa barabara ni kati ya vitu vyenye mchango mkubwa kwenye kipato cha mtu mmojammoja hata uchumi wa Taifa.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni kuendelea kukua na kuimarika kwa uchumi ambao unachochewa na jitihada za Serikali za kuwekeza kwenye miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja, reli, viwanja vya ndege sanjari na kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme.

Hivyo barabara zinazoruhusu magari kutembea kwa kasi kubwa huwezesha abiria na bidhaa kufika masoko ya mbali haraka hivyo kuongeza tija, kupunguza umasikini na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo na uchumi.

Tathmini hiyo, wanasema inaweza kutumika pia kuboresha kasi ya barabara ndogo ambazo ni muhimu katika baadhi ya maeneo.

Utaratibu huo, ripoti inasema utazisaidia nchi zinazoendelea kuondoa vikwazo vilivyopo barabarani, hivyo kuongeza ushindani wao katika kusafirisha bidhaa na abiria.

Hata hivyo, utafiti huo unasema tathmini ya kasi iliyofanywa haijahusisha usalama barabarani, uwepo wa namna nyingine za usafiri mfano reli na meli, wala msongamano.

Hata changamoto za uhandisi wa ujenzi wake nazo hazijazingatiwa pia.Kwa mujibu wa takwimu za NBS,zinaonyesha kuna idadi kubwa ya masikini kwenye mikoa ya kanda ya ziwa na ile ya kanda ya magharibi, sababu kubwa ikielezwa kuwa ni ukuaji mdogo wa sekta zinazoajiri watu wengi, hasa kilimo, uvuvi na mifugo tofauti na wanaopatikana mikoa ya mashariki kwenye sekta za viwanda, huduma na usafirishaji zinazokua zaidi.

NBS inasema umasikini nchini unachangiwa na ujinga wa wananchi na ukosefu wa fursa za kiuchumi kwenye maeneo yao.

“Umasikini na elimu ndogo ya wazazi unawaathiri hata watoto kuajiriwa kwenye nafasi zinazolipa vizuri, hivyo kuchelewesha mabadiliko yao ya kiuchumi hivyo wengi kuendelea kuishi kwenye ufukara,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Barabara ya Namtumbo-Songea kabla ya ujenzi ilikuwa ni barabara kero na iliyokuwa ikichangia kudumaza maendeleo kwani mbali ya kuwepo kwa nauli kubwa lakini pia ilikuwa haipitiki kirahisi.

Barabara Namtumbo-Songea yenye Km 61 ni kati ya barabara ambazo ujenzi wake umetokana na msaada kutoka Shirika la Changamoto za MileniA (MCC) ambapo jumla ya dola milioni 46.2 zimetumika kwa ujenzi wa barabara hiyo.

Ujenzi wa barabara hiyo ulianza Juni 14,2010 na kukamilika Septemba 16,2013tangu kukamilikwa kwa ujenzi wa barabara hiyo kumekuwa na mwamko mkubwa wa ujenzi wa makazi lakini pia uanzishwaji wa biashara mbalimbali, wakulima kusafirisha mazao bila ya vikwazo na kufika sokoni kwa wakati.

Laurent Denis ambaye ni mkulima wa korosho na mkazi wa Songea, anasema kuwa ubora wa barabara huchochea maendeleo ya haraka.

Anasema kuwa kabla ya kujengwa kwa barabara hiyo ilikuwa kero kubwa kwa wananchi na kuchangia kudumza maendeleo kutokana na kupitika kwa shida sana.

“Nakumbuka Aprili 17,2008 nyakati za saa 2 usiku mke wangu (Neema Nyakomba) ambaye alikuwa ni mjamzito wa miezi 7 na matarajio yake ya kujifungua ilikuwa Juni na alitakiwa kwenda kwa wazazi wake waishio Songea mjini.”

Tulikubaliana ndani mwishoni mwa wezi huo wa Aprili aondoke na ilipofika Aprili 17 asubuhi nilimsindikiza kwenda Songea cha kushangaza njiani aliniambia anajisikia vibaya kwamba mgongo ulikuwa ukimuuma sana hata kukaa kwake ikashida” anasema .

Anasema kuwa barabara hiyo ilikuwa kero kubwa sana kutokana na kutokuwa na lami hivyo gari walilopanda aina ya landrover lilikuwa likipita kwa shida kutoka na kipindi hicho kuwa na mvua na pia kukwama mara kwa mara.

Denis anasema kuwa wakati wakielekea Songea njia katika kijiji cha Ndonde mkewe alizidiwa hivyo waliamua kutoendelea na safari kwa kuwa alikuwa na dalili ya kujifungua.

“Kwa kweli sitousahau mwaka 2008 kwani mke wangu aliumwa sana na hata hatujiandaa kwa kuwa muda wa kujifungua ulikuwa bado hivyo niliomba msaada kwa wanakijiji ambapo kulikuwa na mkunga ndiye aliyetusaidia na ilipofika saa 5 usiku alijifungua mtoto wa kiume nyumbani hata hivyo nusura nikose mke na mtoto kwa jinsi ambavyo wakati anajifungua kupata tatizo ambaye jina lake nilimwita Israel Denis Laurent na sasa ana miaka 14 anasoma kidato cha pili,” anasema.

MFANYABIASHARA MAAFURU NAMTUMBO

Hashaz Saidi ni mfanyabiashara maarufu Namtumbo Mjini tangu mwaka 2003, anasema kuwa kuna mafanikio ambayo yanaonekana tangu kupatikana kwa ufadhili wa barabara ya Songea -Namtumbo chini ya ufadhili wa MCC kwani usafirishaji wa bidhaa hivi sasa umekuwa ni rahisi.

“Hakuna aliyekuwa anataka kuleta gari lake huku na ndio maana gharama ya usafiri ilikuwa juu lakini hivi sasa kutoka Songea kwenda Namtumbo unatumia sh,6500 pamoja na hayo mjini kuna benki za NMB,CRDB na pia kuna Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya na hata kituo cha Polisi haya ni maendeleo tuliyokuwa tukiyataka kwa muda mrefu,” anasema.

DC NAMTUMBO ANENA

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt.Julius Ningu anasema kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mkoa wa Ruvuma ya kuhakikisha kuwa miundombinu ya barabara na madaraja inaimarishwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa kwa lengo la kuinua uchumi na kuchangia kasi ya maendeleo zinaendelea.

Anasema kuwa ujenzi wa barabara Songea-Namtumbo kilometa uliojengwa chini ya ufadhili wa Millenium Challenge Corporation(MCC),umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kutokana kuongezeka kwa mafanikio katika sekta elimu, kilimo, biashara na hata afya.

UPANDE WA SEKTA ELIMU

Dkt. Ningu anasema kuwa tangu kukamilika kwa barabara hiyo kumekuwa na mwamko wa ujenzi wa makazi lakini pia kujengwa kwa Chuo cha Uhasibu tawi la Arusha lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 400.

“Pembezoni wa mwa barabara hiyo ya ufadhili wa Watu wa Marekani imesaidia kuchochea maendeleo katika nyanja mbalimbali kwani hata kujengwa kwa Chuo cha Uhasibu kumetokana na kukamilikwa kwa barabara hiyo na pia kumekuwa na maombi ya ujenzi wa shule za watu binafsi kwani itasaidia kuongeza ari katika sekta ya elimu.

“Tulikuwa hakuna chuo lakini kukamilika kwa barabara hii kuchangia kuanzishwa kwa chuo ambao kinachochea sekta ya elimu na hata uchumi naamini kuwa katika sekta ya elimu itakuwa kutokana na kuongezeka kwa uwezekaji,” anasema.

BIASHARA

Akizungumzia kuhusiana na biashara hiyo anasema kuwa kumekuwa usafirishaji wa makaa ya mawe yanayotoka Mbinga-Songea-Namtumbo na kuelekea bandari ya Mtwara jambo ambalo limechochea kuanzishwa kwa biashara nyingine kama baa,nyumba za kulala wageni na hata miji na vijiji.

“Kuna mambo mengi yameongezeka lakini yote hayo yametokana na kukamilika kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami lakini pia kuna kituo kidogo cha mabasi yatokayo mikoani kuanzishwa cha Seedfarm ambacho kimekuwa msaada mkubwa sana kwa abiria.Mpiga debe wa kituo hicho, ambaye alijitambulisha kwa jina la Mapunda, anasema kuwa ni vozuri Serikali ikaomba ufadhili kwa Watu wa Marekani wawasaidia pia kujenga barabara zingine hapa Ruvuma ambazo kama zikikamilika zitakuwa na fursa kubwa kwa wananchi na hata Serikali,” anasema.

“Tangu kukamilika kwa ujenzi huu kumechochea kuanzishwa kwa kituo kidogo cha mabasi hakika kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi, hata hivyo tumechelewa haya yote yalitakiwa kufanyiwa huko nyuma naamini na sisi tungekuwa mbele zaidi,’ anasema.

UMOJA WA WASAFIRISHAJI MAZAO RUVUMA

Akizungumzia mafanikio mwenyekiti wa Umoja wa Usafirishaji Abiria Mkoa wa Ruvuma (TWAUMARU),Jaribuni Mangoma,anasema kuwa tangu kukamilika kwa barabara hiyo kumewapunguzia ugumu wa maisha kutokana na kupungua kwa gharama za usafirishaji mazao lakini pia usafirishaji abiria.

Mangoma anasema kuwa awali walikuwa wakitumia masaa mengi kutoka Songea kwenda Namtumbo kutokana na barabara kupitika kwa shida sana na matajiri wengi kukataa kupeleka magari yao yao.

“Nauli ilikuwa juu ambapo sh,20,000 abiria alikuwa akitoka Songea kwenda Tunduru lakini kwa sasa nauli sh.10,000 ambapo imechangia kuunganisha kirahisi kwa maeneo mengine kutokana na kufikika kirahisi.”

“Pia kumekuwa na mabadiliko kwa Wilaya ya Tunduru ambayo awali ilikuwa nyuma kimaendeleo sasa kuwa mara mbili na kuonekana kukimbia kiuchumi ambapo hivi sasa unaweza kutumia masaa 3 kutoka Tunduru badala ya masaa 12 ya mwanzo,” anasema Mangoma.

Anasema kuwa pia wakulima wa nyanya,viazi, mahindi mabichi hivi sasa wanasafirisha bidhaa zao kwa urahisi tofauti na awali ambapo walikuwa wakikaa barabarani muda mrefu kusubiri usafiri na hata kufikia hatua ya kulala barabarani na huku bidhaa zikiharibika.

OFISI YA MKUU WA MKOA

Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Steven Mashauri Ndaki akizungumnza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Kanali Laban Thomas,anasema kuwa Mkoa wa Ruvuma hivi sasa unafanya jitihada za kuhakikisha kuwa barabara zinazounganisha miji zikarabatiwe na kuweza kufika kirahisi mjini.

Anasema kuwa pia imeongezeka kwa nyumba za kulala wageni,vijiji hivyo kuonekana kuhitajika kwa ukarabati wa barabara ili kusaidia kufikika katika maeneo mengine kirahisi.

Ndaki anasema kuwa ili kupata mafanikio kuna barabara ambazo zinahitaji kupata ufadhili ni kama barabara ya Tanzania-Msumbiji ambapo wananchi wa pande zote hutumia barabara hii kuingia yenye Km 124 hivyo inahitajika sh.bilioni 248 ili kujenga barabara yenye kiwango cha lami.

Pia inahitajika sh.bil.224.8 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Luanda-Nyasa -Lutohi kujenga barabara ya lami ili kuwarahisishia wananchi kwenda ziwa Nyasa na kufanya shughuli za uvuvi.

“Kwa ujenzi wa barabara hizo pamoja na ile ya Kidatu-Ifakara,Lupilo-Londo,Namtumbo-Rumecha ambayo inatokea Mikumi itasaidia uwekezaji na hata usafiri wa kwenda Iringa ambapo ni Km 512,” anasema.

Anasema kuwa bado inahitajika misaada zaidi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kuwa mji unazidi kukua na idadi ya wananchi inaongezeka hivyo katika kukuza utalii ni vyema barabara hizo zikajenga.

TANROADS YAELEZA FAIDA ZA BARABARA ZA LAMI

Anasema,kukamilika kwa barabara hiyo ya Songea-Namtumbo iliyojengwa kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kumesaidia hata makazi hasa ardhi kuwa na thamani kubwa na kuongezeka kwa idadi ya watu watakaokuwa wanaitumia kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Meneja wa TANROADS mkoani Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi anasema kukosekana kwa barabara ya lami ni chanzo cha kusuasua kwa maendeleo kwenye maeneo mbalimbali,hali hii imechangia sana hata usafiri kwenda kuwa ngumu siyo wakati wa masika tu bali hata muda wa kiangazi, na madereva wanatumia nafasi hiyo kupandisha nauli.

“Katika kuhakikisha kuwa barabara zetu zinapitaka kirahisi kumekuwa na jitihada mbalimbali zinazofanyika ambapo hivi sasa tana ujenzi wa barabara ya mchepuko (Songea ByPass)maarufu kama (Mtwara Corridor)yenye urefu wa km 14.3. umeanza,” anasema Mlavi.

Anasema kuwa bado kunahitajika wafadhili ili kufanikisha ujenzi mbalimbali kwani kuna maeneo wananchi wanafika mjini kwa shinda kutokana na barabara hizo kupitika kwa shida hasa kipindi cha mvua.

TAHADHARI KWA WANANCHI

Anasema kuwa ni vizuri jamii na taifa kwa ujumla Mkuu huyo wa mkoa anasema kuwa ni muhimu wananchi wakaelimika vya kutosha ili waone umuhimu wa kulinda miundombinu ya barabara na mawasiliano kwa ujumla ili isihujumiwe hata kusababisha usumbufu kwa jamii na taifa kwa ujumla.

“Lindeni miundombinu ili idumu kwa muda mrefu hasa barabara zinazojengwa kwa fedha nyingi na kuhujumiwa na wananchi wasiopenda maendeleo mara kwa mara hivyo kuisababishia Serikali hasara kubwa ,”anasema Mwambungu.