Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
RAIS John Magufuli, amechukua fomu ya kuomba kusimamishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Rais Magufuli amechukua fomu ya kuwania urais Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma muda mfupi uliopita ambayo amekabidhiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally.
“Nimeishachukua fomu, kwa hiyo nitaanza kutafuta wadhamini wa hapa hapa Dodoma,” amesema Rais Magufuli wakati akizungumza na wana-CCM walijitokeza kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo.
Mara baada ya kuchukua fomu alipokuwa akiondoka, Rais Magufuli amekutana na makada wa Chama hicho waliokuwa wamejawa furaha, huku mmoja wao akimpa pole kwa kuuguliwa na mama yake.
Makada hao wa CCM wamemhakikishi Rais Magufuli kwamba ni makada wa Chama hicho na wapo tayari kumdhamini. Katika kinyang’anyiro hicho ndani ya CCM, Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, hatarajiwi kupata upinzani kutokana na mila na desturi za chama hicho kuachiana muda ili Rais anayekuwa madarakani amalize kipindi chake cha miaka kumi ya uongozi wake.
Rais Magufuli amechukua fomu ili kuomba kusimamishwa na CCM kuwania muhula wa pili wa uongozi wake ambao akiumaliza atakuwa amehitimisha ngwe ya miaka 10 ya Serikali ya Awamu ya Tano.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari