Na Nathaniel Limu,TimesMajira Online. Singida
WATANZANIA wamehimizwa kujenga utamaduni wa kutumia vyakula vya mtama, kwani pamoja na faida zake nyingi lakini pia unaweze kupunguza kasi ya kuzeeka.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na mtafiti wa kilimo kutoka Kituo cha Utafiti (TARI) Ilonga Kilosa, Franck Reuben wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye viwanja vya Social vinavyomilikiwa na Kanisa la Roman Katoliki mjini hapa.
Akizungumza na Majira mtafiti huyo, amesema mtama pamoja na kurefusha maisha ya binadamu pia unapunguza makali ya maradhi ya kisukari na kansa.
“Watu wengi wenye umri mkubwa, ukiwauliza ni kitu gani ambacho kimechangia afikishe umri huo mkubwa. Kwanza atakuambia ni kazi ya Mungu na kisha atakuambia imetokana na kula vyakula vya mtama,” amesema.
Reuben amesema pamoja na mtama kuwa na virutubisho mbalimbali, mtama ukichanganya na ngano utatengeneza maandazi, mkate, biskuti, pizza, pilau, wali, kande, bisi, togwa na chakula cha ‘kulikiza’.
Amesema chakula cha kulikiza, hupewa watoto wadogo wenye umri wa miezi sita na kuendelea. Pia wagonjwa na watu wengine wanaopendelea kunywa kwa ajili ya afya zao.
Mtafiti huyo amesema mtu mwenye ugonjwa wa kisukari au presha, akienda hospitalini atashauriwa kutumia vyakula vya mtama kwa kuwa huongeza nguvu ya mwili.
Kuhusu kilimo cha mtama, amesema mtama ni zao lenye uwezo mkubwa wa kustahimili ukame ikilinganishwa na mazao mengine ya nafaka.
Amesema mtama una fursa kubwa ya kuzalishwa kwa wingi zaidi kama zao la chakula kwa vile, haliathiriwi na ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa sasa mtama ni zao la tatu katika mazao ya nafaka kuzalishwa kwa wingi hapa nchini. Mtama vile vile ni zao linalotumiwa kama mali ghafi katika viwanda vya kutengeneza vyakula vya mifugo na vinywaji mbalimbali hivyo kulifanya kuwa zao la kibiashara,” amesema.
Kwa upande wake mkazi wa Kijiji cha Ihanja Wilaya ya Ikungi, Samsoni Sangida (69) amesema kabla ya uhuru zao la mtama ndilo lilikuwa zao pekee kwa kwa makabila mengi wakiwemo Wanyaturu.
“Enzi hizo kabla ya uhuru, miili ya watu ambao walikua wanategemea zao la mtama kwa chakula chao, miili yao ilikuwa mikubwa na yenye nguvu nyingi baada ya zao la mahindi na mengi mapya kuingia nchini, miili ya watu imekuwa myepesi na haina nguvu. Upepo mkali ukivuma, mtu anapepesuka,” amesema.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto