Judith Ferdinand
Ndoa za utotoni ni tatizo sugu katika maeneo mengi ya Tanzania, hasa katika jamii za wavuvi na wafugaji. Wasichana wengi huozeshwa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18, hali inayohatarisha maisha yao ya baadaye.
Aidha ndoa hizi ni ukatili dhidi ya watoto wa kike kwa kuwa wanakuwa hawajakomaa kimwili, kisaikolojia na kijamii kuweza kubeba majukumu ya uzazi na familia. Huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Tatizo hili linachochewa na sababu mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kimila ambazo zinahitaji kueleweka kwa kina ili kutafutiwa suluhisho.

Familia nyingi zinazojihusisha na uvuvi na ufugaji zinaelezwa kuwa katika umasikini mkubwa wa kipato, hivyo kuwa mojawapo ya sababu ya wazazi kuona kuwa kuwaoza watoto wa kike ni njia ya kupunguza mzigo wa kifamilia au kupata mahari. Wakati mwingine, familia huamini kuwa mtoto akiingia katika ndoa, atapata maisha bora zaidi kuliko anavyoyapata nyumbani.
Tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa ndoa za utotoni zinafanyika zaidi maeneo ya vijijini, katika jamii masikini na katika mikoa ya Magharibi, Kusini na Kaskazini – Magharibi mwa Tanzania. Inaelezwa kuwa wanawake wanne kati ya kumi sawa na asilimia 37, wenye umri wa miaka 15-49 wanaoishi Tanzania vijijini waliolewa wakiwa watoto, ikilinganishwa na wanawake wawili kati ya kumi sawa na asilimia 21 wanaoishi maeneo ya mijini.
Ndoa za utotoni pia ni hali ya kawaida na iliyozoeleka katika mikoa ya magharibi mwa nchi kwa asilimia 42, Ukanda wa Kusini asilimia 42 na Kanda ya Ziwa asilimia 39.
Wanawake wanaoishi katika kaya masikini asilimia 46 wana uwezekano mkubwa mara tatu zaidi wa kuolewa kwa mara ya kwanza wakiwa bado watoto kuliko wanaoishi katika kaya tajiri sawa na asilimia 16.
Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Kayenze na Bugogwa wilayani Ilemela mkoani Mwanza zilizopo kandokando mwa Ziwa Victoria, wanaeleza sababu zinazoweza kuchangia wasichana katika maeneo yanakofanyika shughuli za uvuvi kuolewa wakiwa wadogo.
Natumia saa mbili kutoka katikati ya Jiji la Mwanza hadi shule ya sekondari Kayenze iliopo wilayani Ilemela, napata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
Mazungumzo yanaanzia kwa Belina Antony, mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Kayenze ambaye anasema sababu ya watoto wa kike katika maeneo ya kandokando mwa Ziwa Victoria kuingia katika ndoa za mapema ni wazazi kuwaacha watoto wajilee wenyewe.
“Katika mazingira yetu ya uvuvi unakuta baba na mama wameenda visiwa vya mbali kwa ajili ya kutafuta mazao ya uvuvi, huku nyuma anaacha watoto chini ya uangalizi wa mtoto wa kike haijalishi umri wake na wengi wao wanakuwa na miaka chini ya 18.
“Hali hili inakuwa rahisi kwake kurubuniwa na hali inayochangia mabinti kujiingiza kwenye uhusiano, matokeo yake anapata ujauzito hali inayomlazimu kuolewa hata kama hataki ili kumuepusha muhusika aliyempa ujauzito huo kuingia matatizoni,” anasema Belina.
Kauli hiyo inaungwa mkono na mmoja wa wananchi wa Igombe Kata ya Bugogwa, Mariatabu Masumbuko, anasema hali ya watoto kujilea wenyewe ni ya kawaida sana katika jamii za uvuvi.
“Hii ni kutokana na wazazi kuwa mbali au kutokuwa makini, watoto hujikuta wakifanya maamuzi bila ushauri wa watu wazima. Wasichana hasa huingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na hatimaye ndoa za mapema kama njia ya kujikimu au kutafuta hifadhi,” anaeleza.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Pamela Kijazi, anasema changamoto kwa kazi ya wavuvi ni ile hali ya kuhamahama kutoka eneo moja kwenda jingine, kutafuta mazao ya uvuvi kama samaki na dagaa. Hivyo wazazi wanaweza kuondoka nyumbani miezi miwili hadi mitatu na kuwaacha watoto wao hawana ungalizi wa watu wazima.
“Wanajilea wenyewe muda wote na wakati mwingine wanaishiwa mahitaji, unakuta kuna watu ambao siyo waaminifu wanawalaghai watoto wa kike na matokeo yake anapata ujauzito na kisha kulazimika kuolewa akiwa katika umri mdogo, au wengine wanarubuniwa na kuingia kwenye ndoa katika umri huo, licha ya kuwa elimu tumepeleka katika jamii hiyo ya kuhakikisha malezi ya watoto wao yanakuwa mazuri,” anasema Kijazi.
Ofisa Elimu Watu Wazima Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Redemptor Kibiti, anasema ndoa za utotoni zipo ingawa siyo kwa kiasi kikubwa. Anaeleza kuwa mwaka juzi walipata kesi mbili za ndoa hizo. Anasisiza kuwa kwa asilimia kubwa zinafanyika maeneo yanakofanyika shughuli za uvuvi huku sababu ikiwa ni watoto kujilea wenyewe kwa muda mrefu.
Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Sekondari Bugogwa, Tumaini Kabila, anasisitiza kuwa shughuli ya uvuvi inaweza kuchangia ndoa za utotoni. Anaeleza kuwa kwanza watoto kujilea huku wazazi wakijikita kutafuta mazao ya uvuvi kwa ajili ya kipato na kusahau wajibu wao wa msingi wa malezi. Pia wavuvi kutumia kipato chao cha msimu kuwalaghai mabinti ambao kimsingi wengi wao wanatoka kwenye familia duni.

Kutelekeza familia kichocheo kingine
Neema Mwita mwanafunzi wa shule ya sekondari Kayenze anasema uvuvi na hali duni ya maisha vinachangia wasichana kuangukia katika ndoa za utotoni kwani wazazi hushindwa kumudu mahitaji ya familia zao, hali inayochangia watoto wa kike kutumika kama kitega uchumi.
“Kwa mfano sisi watoto wa kike, mzazi anaposhindwa kututimizia mahitaji ya msingi kama taulo za kike na vitu vingine, kunaweza kusababisha binti kujiingizia katika mambo hatari ili aweze kupata kifaa hicho kwa ajili ya kujisitiri, ikiwemo kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi ambao ni kichocheo cha kuingia kwenye ndoa za mapema,” anaeleza Neema.
Kauli hii inajidhirisha kupitia kisa cha binti mmoja wilayani Kwimba ambaye alijikuta ameingia katika uhusiano wa kimapenzi akiwa darasa la saba, baada ya kuvunja ungo na mama yake kushindwa kumpatia huduma ya taulo za kike. Hivyo aliona njia rahisi ya kupata mahitaji hayo ni kujiingiza katika mapenzi jambo ambalo lilikuwa hatari na kama hasingeokolewa na uongozi wa Wilaya hiyo wa kipindi hicho angeweza kutumbukia katika ndoa na mimba za utotoni.
Diwani wa Kata ya Kayenze, Issa Mwalukila, anasema tabia ya baadhi ya wazazi kutelekeza familia katika maeneo ya uvuvi, ni mojawapo ya vichocheo vya ndoa za utotoni. Pia kuna sababu nyingine kama vile migogoro, kutokuelewana ndani ya familia, wazazi hasa akina baba kutafuta maisha mbali na nyumbani, kwa ujumla wake hali hizo huwafanya watoto kukosa malezi ya karibu na kutumbukia kwenye tabia hatarishi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini, Ali Yassin, akizungumza na Majira hivi karibuni alisema katika maeneo ya uvuvi shinikizo kubwa ni wanaume (baba) kutelekeza familia kutokana na ukatili na umaskini kwa kushindwa kulea familia.
Alisema hali hiyo huacha jukumu la kulea familia kwa wanawake (mama) ambao huwatuma watoto wadogo wa kike kwenda kwenye mialo kufuata samaki akiwa na fedha ndogo. Pia wanawake nao wanatelekeza watoto na kuwaachia watoto wa kike wenye umri mdogo majukumu ya kuhakikisha mahitaji ya nyumbani yanapatikana.
Tabia hiyo kwa ujumla wake inaelezwa kuchangia mabinti kujikuta kwenye shinikizo la kukubali kufanya ngono isiyo salama ili apewe samaki na ile fedha ndogo aambiwe nenda akanunulie kitu kingine kwa sababu yeye ni rahisi na hana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.
Kwenye mazingira hayo, watoto hao katika kutimiza mahitaji ya kutafuta chakula wanajikuta wameingia kwenye mtego wa ndoa za utotoni na mimba za utotoni kutokana na vishawishi na shinikizo la kupata mahitaji ya nyumbani.
“Tumefanya kazi kwenye baadhi ya kata ambako kunafanyika shughuli za uvuvi ikiwemo Kayenze na Igombe unaweza kukuta kwenye familia kuna binti mwenye umri wa miaka 18 hatumwi kwenda kununua samaki, bali atatumwa binti wa miaka 14 ambaye akienda yeye ndio atakuja na samaki wengi, hapo unapata picha gani? kwani ana akili zaidi ya dada yake mwenye umri wa miaka 18,” anahoji Yassin.
Mwalimu wa Taaluma wa shule ya sekondari Bugogwa, Tumaini Kabila, anasema ndoa za utotoni kwenye maeneo ambayo shughuli za uvuvi hufanyika husababishwa na wasichana kujiingiza katika masuala ya mapenzi wakiwa katika umri mdogo, ushirikiano duni kutoka kwa wazazi huku jamii ikifanya siri kwa kushindwa kutoa taarifa kwani ndoa hizo zinaanzia ndani ya familia.
Suala hilo la usiri linaungwa mkono na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Pamela Kijazi, anasema moja ya changamoto ya kubaini ndoa za utotoni ni kuwa jamii kuendekeza usiri, hivyo kupata taarifa inawawia ugumu na wakati mwingine hazipatikani kabisa.
Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kayenze, Mwalimu Noeli Zaidi, anasema sababu ya kuwepo kwa ndoa za utoto ni wazazi kumalizana wenyewe na alieoa au kubebesha mimba binti ambaye ni mwanafunzi, hali hiyo inachangia jamii kuona suala la kumkatisha binti na kumuoza ni jambo la kawaida.
“Mwaka jana tulipata kesi ya binti mmoja ambaye alikuwa ni mwanafunzi wetu, ambaye aliolewa katika umri mdogo na kesi yake ilifika polisi, lakini changamoto ilikuwa ushirikiano wa wazazi haukuwepo. Maana wewe unaweza kufuatilia, lakini huku nyuma mzazi akawa ameshamalizana na muhusika, kwani sisi kazi yetu ni kupeleka barua na mahudhuriao ya kuthibitisha binti fulani kama ni mwanafunzi kweli basi,” anaeleza Noel.
Nenetwa Ngedele mwanafunzi wa shule ya sekondari Bugogwa anasema baadhi ya mabinti wanalazimika kuingia kwenye ndoa za utotoni baada ya kupata ujauzito katika umri mdogo, hivyo wazazi hulazimika kukubaliana na aliyempa ujauzito kwa kumuoa.
Hata hivyo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Pamela Kijazi, anasema ndoa za utotoni wanazipata kupitia binti akiwa mjamzito anavyokwenda kliniki katika vituo vya afya.
“Mtu anajua sheria inataka mtoto aendelee na masomo hivyo mzazi anafanya siri endapo mtoto atapata ujauzito, wanaamua kumuozesha kimya kimya, taarifa hazisemwi watu wanamalizana nyumbani. Hivyo, wito wangu kwa jamii watoe taarifa hizo na waache mabinti wasome na watimize ndoto zao,” anasema Pamela.
Mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Bugogwa Fibi Ilelema, anasema kutokana na mazingira ya kandokando mwa ziwa, watoto wa kike wanakabiliwa na ushawishi kutoka kwa wanaume wenye tamaa, ambao huwarubuni na kujikuta wameanzisha uhusiano nao kisha kuangukia kwenye ndoa za utotoni.
“Si rahisi kwa binti mdogo kuweza kukwepa vishawishi hivyo kwa muda mrefu na ukizingatia asilimia kubwa ya maisha yetu ni duni. Mfano binti mmoja tulikuwa tunakaa mtaa mmoja ila sasa amehama, alishindwa kuepuka vishawishi kwani walijiingiza kwenye mapenzi kwa sababu ya tamaa ya fedha za kula wakati akiwa shuleni, mwisho amejikuta amepata ujauzito na hatimaye kuolewa katika umri mdogo,” anasema Fibi.
Mzigo mzito wa kulea familia, mfumo dume
Naye Mtaalamu wa Mafunzo mradi ‘Hapana marefu yasio na mwisho’ Mchungaji wa KKKT Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria, Julia Gabriel, anaeleza kuwa ndoa za utotoni zinachangiwa na umaskini wa wazazi kwani uwezo wao wa kumudu familia upo chini. Hivyo, njia nyepesi wanayoamini inaweza kupunguza mzigo wa malezi kwa familia ni kuwaozesha watoto wa kike wakiwa bado na umri mdogo.
Julia Gabriel anasema sababu nyingine ya ndoa za utotoni, ambazo wamebaini kupitia mradi huo hususani kwenye jamii za ufugaji ni uelewa mdogo wa jamii hasa maeneo ya vijijini kutofautisha mila na tamaduni na masuala ya haki na sheria kwani wamejikita zaidi katika tamaduni hivyo hawazingatii sheria.
Alitaja mfume dume uliopo kwa jamii nyingi hususani za vijijini ambazo sauti za wanawake hazipewi umuhimu huchangia wimbi la ndoa za utotoni. Anasema kuwa maeneo ambayo mradi umefanya kazi wapo wanawake wengi waliozungumza nao ambao hawakutaka watoto wao kuozeshwa, lakini kwa sababu ya mfumo dume hawana mamlaka juu ya watoto kwani mwanamume (baba) anafanya maamuzi.
“Wapo wamama amabao walipambana kuhakikisha watoto wao hawaolewi wakiwa wadogo na ndoa zikavunjika, mfano mabinti tulionao hapa walifika hapa kwa jitihada ya mama zao ambao hawakutaka waozeshwe,” anaeleza.
Hii imedhihirisha kupitia kisa cha Furaha Matumaini mwenye umri wa miaka 19, siyo jina lake halisi, akiwa ni mtoto wa nne kati ya watano kutoka kwenye familia na jamii ya kifugaji, ambaye amenusurika kuolewa katika umri mdogo baada ya kuokolewa na KKKT na sasa ana soma kwa ajili ya kurudia mtihani wa kidato cha nne mwaka huu ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa askari wa usalama barabarani (trafki).
“Nilimaliza kidato cha nne mwaka 2023 nikiwa na miaka 17, lakini nilipata ufaulu wa chini ambao sikuweza kuendelea kielimu, ikanilazimu kukaa nyumbani, akajitokeza mtu kutaka kunichumbia na akatoa kishika uchumba cha ng’ombe mmoja, lakini mimi muolewaji nilikuwa sijui. Mama yangu mzazi alikuwa hataki mimi nitolewe mahari wala kuolewa, lakini kutokana na mfume dume hakuwa na sauti na asingeweza kuzuia kwani aliyekuwa anashinikiza mimi niolewe ni baba yangu mdogo kwani baba yangu mzazi amekwisha kufariki,”anaeleza binti huyo.
Pia Mchungaji Julia anasema changamoto nyingine ni mila na tamaduni, ambapo wanakabilina nazo kwa kunatoa mafunzo shuleni wakati wa likizo kwenye jamii za kifugaji, wakiwauliza watoto wa kike ni mambo gani wanafikiri yanaweza kusababisha wasifikie ndoto zao, wanawataja baba zao kuwa ni vikwazo, huku wakisema mama zao hawana shida.
“Mila na tamaduni kwamba mtoto ni mali ya mwanaume, maamuzi juu ya nini kifanyike kwa mtoto ni ya mwanaume, wanaona moja ya changamoto ni baba zao, pia wamezuilia mahitaji ya shule kwa baadhi ya watoto ambao wamefanya vizuri. Hawawapi mahitaji ya shule ili washindwe kusoma, warudi nyumbani wakae na wafikie malengo ya kuwaozesha katika umri mdogo,” anasema Julia.
Achanja mbuga kutoroka kuolewa, hakuhofu wanyama wakali
Hata hivyo hapa kuna simulizi ya Subira Mafanikio, siyo jina lake halisi, binti mwenye umri wa miaka 19 kutoka kwenye familia na jamii ya kifugaji alinusurika kuingia kwenye ndoa za utotoni baada ya kufanikiwa kukimbia waoaji. Alitumia dakika 30 kupita kwenye pori lililojaa wanyama hatari kama tembo na hatimaye kupitia mradi wa ‘Hapana Marefu Yasiyo na Mwisho ameweza kuendelea na masomo na anatarajia kurudia mtihani wa wa kidato cha nne mwaka huu ili kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanasheria.
Binti huyo anasema mila na tamaduni za jamii yao ya kifugaji ndio ilitaka aolewe katika umri mdogo, aidha baba yake hakutaka aendelee na masomo kwani hapendi watoto wa kike wasome akiamini ni kupoteza muda na anaweza kuleta aibu nyumbani.
“Mimi ni mtoto wa nne kuzaliwa kati ya watoto sita, nina miaka 19, nilivyomaliza kidato cha nne nilipata ufaulu wa chini, sikuweza kuendelea na kidato cha tano, watu ambao walikuwa wananiunga mkono kusoma ni mama yangu, hivyo uwezo wa kunilipia ada ya mimi kwenda chuo hakuwa nao, ikabidi sasa nikae tu nyumbani anasimulia Subira.
“Watu wakawa wanakuja nyumbani kuja kunioa, lakini walishindwa. Ila siku moja jioni walikuja watu wengi nyumbani kwa ajili ya kunibeba, kwa taratibu za mila na tamaduni za kwetu mtu akitaka kuja kukuoa anakuja kwenu anakubeba kwa lazima, hata kama hutaki, lakini wanakuwa wamekwisha kubaliana na wazazi wako, hivyo baada ya kuona kundi hilo ndipo nilipokimbia,”.
“Kwa sababu ilikuwa ni usiku nilikimbia mpaka kwenye pori kisha nikamfua na rafiki yangu tukakimbilia kwa mjomba ambaye yeye alikuwa mwenyekiti, nilitumia dakika 30 kujiokoa ili nisiolewe licha ya kuwa porini kuna wanyama wakali, sikuogopa bali nilijiamini na hatimaye niliweza kuwasilina na Mchungaji Julia ambaye aliniambia hapa Mwanza kuna nafasi, hivyo nipo ninaendelea na masomo ninaimani nitafanya vizuri,” anasimulia kwa kujiamini.

Kadhalika Mchungaji Julia anasema sababu nyingine ni ujinga kwani jamii hizo hazioni faida ya kusomesha watoto wa kike, wanaona bora aolewe mapema wajipatie chao mapema. Aidha, wazazi na walezi wana hofu kwamba mtoto wa kike hawezi kusoma akarejjea salama nyumbani bila kupata ujauzito angali masomoni, hivyo kuwa aibu kwa familia.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa shirika la Kivulini, Yassin Ali, anaeleza kuwa chimbuko la ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni ni hali ya chini aliyopewa mwanamke na mtoto wa kike kutokana na mila na desturi kandamizi. Anasema kutokana na tamaa ya mali – mahari, watoto wa kike huozeshwa katika umri mdogo na mikoa inayoongoza kwa vitendo hivyo Shinyanga na Mara.
Wazazi wataka mabinti wajifelishe
Aidha anasema upo ushahidi wa wazazi kuwatishia watoto wa kike siku za mitihani wakiwataka wafanye vibaya ili wasifaulu kuendelea na masomo nia ikiwa ni kuwaozesha mapema.
“Kuna kauli ya kuwa nenda ukachore jovijo yaani ni kuchora madudu, aidha kwenye mtihani wa taifa wa darasa la saba, kidato cha pili au cha nne, kwa hiyo kama ulitoka kwenye kitovu cha tumbo langu uhakikishe haufaulu ole wako ujifanye una akili,” anaeleza Yassin kuwa hizo ndizo kauli wanazotumia baadhi ya wazazi kuwatisha watoto wao.
Yassin anaeleza kuwa wazazi wanajua akishindwa (akishafeli) kwenye mtihani wa darasa la saba, kidato cha pili au cha nne itakuwa ni rahisi kutimiza azima yao ya kupata mahari na kumuozesha binti.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Mchungaji Julia ambaye anaeleza kuwa amekutana na tabia moja Bariadi ambako binti wanafundishwa na wazazi kwenda kuchora chora kwenye mitihani ya mwisho, ili wasifaulu kuendelea na masomo.
Anasema wazazi hao wamekuwa wakitoa vitisho kwa kutandika shuka na kumwambia binti wa kike, kuwa kama wewe unaweza kupambana na tamaduni zetu ruka shuka hili, kutokuruka maana yake anakubaliana nao kuwa ataenda kuchorachora kwenye mtihani.
Mbinu hizi zinatumiwa na wazazi kukwepa mkondo wa sheria kwani mtoto akifaulu lazima aendelee na masomo, hivyo ili waweze kumpeleka kwenye mambo yao ya kumuozesha wanamlazimisha afayanye vibaya kwa kuchora chora ili asifaulu.
“Kuna binti aliambiwa kwenye mtihani wa darasa la saba akachore, lakini hakufanya hivyo akafaulu kuingia kidato cha kwanza, walimnyimwa mahitaji ya kwenda kidato cha kwanza,” anasema.
Aidha anaeleza sababu nyingine ya mimba za utotoni na ndoa za ni watoto wengi kutokuwa na elimu ya afya ya uzazi ambayo ingewasaidia katika kujitambua na kujilinda.
More Stories
Mhandisi Samamba ahimiza uaminifu kwa watoa huduma migodini
Mwanasheria Mkuu wa Serikali awataka wananchi kujitokeza kujiandikisha daftari la wapiga kura
Dkt.Mpango azindua shule ya sekondari itakayojengwa na CRDB Dar