Na Yusuph Mussa,Timesmajira Online,Lushoto
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Japhari Kubecha amewataka Madiwani kusimamia miradi na kuona thamani ya fedha inaonekana badala ya kusubiri viongozi wa kimkoa ama kitaifa ndiyo waeleze changamoto za miradi hiyo.
Na ili Madiwani waweze kufanikiwa kwenye hilo ni lazima waujue mradi tangu mwanzo, hivyo ametaka miradi yote inayopelekwa kwenye kata wajulishwe ili waweze kufuatilia utekelezaji wake.
Ameyasema hayo Mei 25, 2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto robo ya tatu, huku akiweka mkazo miradi ikamilike kwa wakati na thamani ya fedha ionekane.
“Madiwani tushiriki kikamilifu usimamizi wa miradi iliyopo kwenye kata zenu,hapa mnajadili lakini ikija kwenye kata mkazo na msukumo wa kwenu ninyi ya kwenda kuisimamia unakuwa mdogo,mnaacha mpaka akija kiongozi wa chama ama Mkuu wa Wilaya ndiyo mnasema. Ile miradi sio ya Mkuu wa Wilaya, ile miradi sio ya chama, ile miradi ni ya kwenu Madiwani sababu hata bajeti mnapitisha ninyi,”
“Hivyo, inapokuja katika suala la kusimamia, bado ni jukumu letu kuona bajeti yenu inatekelezwa, na value for money (thamani ya fedha) inaonekana kwa miradi kusimamiwa vizuri sababu ni miradi ya halmashauri. Lakini nimuagize Mkurugenzi (Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge), barua ziende kwa Madiwani kuwajulisha miradi inayokuja kwenye kata zao… mradi gani unakuja, waweze kusimamia,”.
Kubecha amesema na mradi huo ueleze unaanza lini na kumalizika lini lakini thamani ya mradi, na nani ama kampuni ipi inatekeleza mradi huo, kwani mambo hayo yatasaidia hata madiwani kufuatilia na kujua utekekezaji wake, na kukiwa na changamoto, taarifa zitolewe mapema kwa wahusika, na sio kusubiri viongozi wa ngazi za juu.
Kubecha, pia amewataka madiwani waache kujihusisha na zabuni zinazotolewa na halmashauri hiyo, na kutolea mfano usambazaji wa vifaa vya Serikali, kwani kufanya hivyo wakati mwingine kunawachafua madiwani, kwani katika miradi hiyo, wakati mwingine inashindwa kukamilika kwa wakati, ukimuuliza mtendaji wa halmashauri, anashindwa kutoa majibu sahihi kwa vile mhusika ni diwani.
“Ni kweli tuna miradi mingi, lakini hii ya Serikali tuachane nayo ili tupate muda wa kuisimamia, na maelezo haya sio ya kwangu, ni maelekezo ya chama. Juzi amepita hapa Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, na ameyatoa kule Bumbuli, na kunitaka mimi nisisitize kwenye vikao vya madiwani.
“Tujiepushe na kukimbilia tender (zabuni) kwenye miradi ya Serikali ili tupate nafasi nzuri ya kuisimamia Serikali kwa maana ya watendaji wa Serikali, kuwe na check and balance, vinginevyo tutabaki tunalalamika miradi haiishi miradi inahujumiwa, kumbe na sisi ni sehemu ya ushirika huo” amesema Kubecha.
Kubecha ametaka miradi ikamilike kwa wakati na kwa ubora, kwani baadhi ya miradi, pamoja na fedha kuwepo, lakini bado haijakamilika, na kutolea mfano bweni la Shule ya Sekondari Magamba.
Lakini pia amesisitiza lishe shuleni, wanafunzi wapate chakula cha mchana wakiwa shuleni, tena chenye lishe, jambo hilo litasaidia kuwafanya watoto waweze kusoma na kufaulu kwa weledi tofauti na wale waliokosa lishe.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mathew Mbaruku amesema suala la wanafunzi kula shuleni, huo ni mwongozo wa Serikali, na sio hiari tena, na mzazi sio lazima atoe fedha, akiweza kutoa hata nafaka iwe mahindi ama maharage inatosha.
Diwani wa Kata ya Kwai, Omari Kipande amesema kuwe na sheria ya kuwabana wazazi wanaoshindwa kuchangia chakula shuleni, kwani kwa sasa hakuna sheria ya kumfunga mzazi anaeshindwa kuchangia chakula shuleni.
Diwani wa Viti Maalumu Sarah Chai, ametaka kuwe na msisitizo kwa kuona mzazi anachangia chakula, sababu mtoto anaweza kwenda shuleni, wenzake wanakula yeye amelala tu kwa njaa kwa vile tu mzazi wake hajachangia chakula .
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa