December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TOST ni kielelezo Rais Samia kukataa kodi za dhuluma

Na Mwandishi Wetu,TimesMajiraOnline

JUMANNE, Aprili 6, 2021 akiwa anaelekea kutimiza miezi mitatu kamili baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kushika wadhifa huuo, alitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akisema;

“Kodi za dhuluma hapana.” Kauli hiyo ya Rais Samia ilibeba ujumbe mzito kwa TRA na aliielekeza kuwarejesha wafanyabiashara waliofunga biashara.

Rais Samia aliitaka TRA kuangalia namna bora ya kuwarudisha wafanyabiashara waliofunga biashara zao kutokana na mabavu yaliyokuwa yakitumika kwenye ukusanyaji kodi.

Alisema ukusanyaji wa kodi kwa kutumia nguvu na mabavu hausaidii, umesababisha wafanyabiashara wengi kufunga biashara zao kwa kuhofia kubambikiwa kesi.

Alitoa maelekezo hayo kwa TRA baada ya kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu wao Ikulu, jijini Dar es Salaam na kumtaka aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, kuhakikisha taasisi hiyo inakusanya kodi kwa haki, bila kuwaumiza wafanyabiashara.

Pamoja na maelekezo hayo, katika uongozi wake, Rais Samia, ameweka msisitizo wa ulipaji wa kodi unaolenga kusimamiwa kwa haki.

Baadhi ya Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya Habari wakifuatilia hotuba iliyokua inatolewa na Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Tanzania, Robert Manyama (hayupo pichani), wakati wa Kikao Kazi cha Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (Tax Ombudsman Service of Tanzania – TOST) iliyopo chini ya Wizara ya Fedha na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kimelenga kuwajengea uwezo kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo ili wawe na uwezo wa kuwahabarisha wananchi kwa ufasaha.

Amekuwa akisisitiza hilo na uongozi wake umejitaidi kuweka mazingira mazuri zaidi ya kufanya biashara nchini.

Kwa kudhihirisha hilo, Serikali imeunda Taasisi ya Usuluhuhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (Tax Ombudsman Service of Tanzania TOST) ikiwa ni taasisi huru ya usuluhuhishi na malalamiko ya taarifa za kodi.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika ukumbi wa Hazina Ndogo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuitambulisha Ofisi hiyo pamoja na malengo na wajukumu ya kuundwa kwa Taasisi hiyo huru ya Usuluhishi, Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Robert Manyama, anasema;

“Taasisi hii inafanya shughuli zake kwa ufanisi na tumetoa fursa hii kuwajulisha wananchi kuhusu taasisi hii na majukumu yake,” anasema Manyama.

Anasema kuundwa kwa TOST kunatokana na nia nje ya Serikali na Bunge kwa pamoja kuridhia kuanzishwa kwa ofisi huru yenye mamlaka ya kisheria kushughulikia malalamiko ya walipa kodi yanayotokana na taratibu, huduma au maamuzi yanayotokea kwa usimamizi wa sheria ya kodi unaofanywa na TRA.

Anasema Ofisi ya TOST imeanzishwa chini ya sheria iliiyounda taasisi hiyo.

Anasema ilianzishwa mwaka 2019 kwa marekebisho yaliyofanywa katika Sheria ya Usimamizi wa Kodi, 2015: Sura ya 438 kwa kuongeza sehemu ya 11A yenye vifungu vya 28A hadi 28F.

Baadhi ya Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya Habari wakifuatilia hotuba iliyokua inatolewa na Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Tanzania, Bw. Robert Manyama (hayupo pichani), wakati wa Kikao Kazi cha Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (Tax Ombudsman Service of Tanzania – TOST) iliyopo chini ya Wizara ya Fedha na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kimelenga kuwajengea uwezo kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo ili wawe na uwezo wa kuwahabarisha wananchi kwa ufasaha

Anasema ujenzi wa taasisi na mifumo yake ulianza Februali 2023 baada ya Waziri wa Fedha kutengeneza kanuni zilizochapishwa katika gazeti la Serikali, GN 105 na GN 106.

Anasema tayari Serikali imehamishia watumishi jijini Dodoma na kuunda taasisi chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha. Kwa mujibu wa Manyama taasisi inaendelea kujiimarisha na sasa iko tayari kutoa huduma kwa jamii kwa kupokea malalamiko yaliyopo yatokanayo na maamuzi yasiyoridhisha au taratibu zisizokubalika za kutoza kodi.

Manyama anasema mambo hayo matatu yanatokana na usimamizi wa sheria ambazo zinasimamiwa na TRA.

Anafafanua kuwa TOST na TRA ni taasisi mbili huru za Serikali, zilizohundwa na kupewa majukumu matatu. Moja kuhakikisha mfumo wa kodi nchini unatoa huduma kwa ufanisi na kwa kuongeza ulipaji wa kodi.

Anafafanua kwamba kwa sasa TOST ina ofisi jijini Dodoma na ina mpango wa kuwa na ofisi nyingine jijini Dar es Salaam.

Kuhusu madhumuni ya kuundwa kwa taasisi, Manyama anasema ni kama ifutavyo;

Moja, kushughulikia malalamiko yatokanayo na sheria za kodi zinazosimamiwa na TRA, kwa kanuni, ufanisi, uwazi, uhalisia na usiri wa taarifa za wafanyabiashara.

“Kwa hiyo taasisi inashughulikia malalamiko ya kodi ikizingingatia misingi hiyo,” anasema Manyama.

Mbili, Manyama anasema taasisi ina jukumu la kuhakikisha maeneo katika usimamizi wa sheria za kodi ambayo ndiyo vyanzo vya malalamikoa kwa walipakodi nchini yanaainishwa na kutoa mapendekezo kwa Waziri wa Fedha.

Tatu, ina jukumu la kupunguza mlundikano wa kesi za kodi mahakamani na kuwezesha kupatikana kwa suluhu kwa haraka ndani ya siku 30 kwa usimamizi wa sheria za kodi.

Manyama, anasema lengo lingine ni kuhakikisha unakuwepo ulipaji wa kodi wa hiari kwa kuhakikisha taratibu na huduma za usimamizi wa kodi zinafuatwa bila unyanyasaji.

***Aina za malalamiko yanayoshughulikiwa

Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Tanzania, Robert Manyama, akitoa hotuba wakati wa Kikao Kazi cha Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (Tax Ombudsman Service of Tanzania – TOST) iliyopo chini ya Wizara ya Fedha na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina Ndogo, jijini Dare es Salaam juzi. Kikao hicho kimelenga kuwajengea uelewewa Wahariri hao kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo ili wawe na uwezo wa kuwahabarisha wananchi kwa ufasaha kuhusu majukumu ya Taasisi hiyo inayoenda kusuluhisha malalamiko ya kikodi baina ya wadau na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Manyama anataja aina ya malalamiko yanayoshughulikiwa na TOST kuwa ni malalamiko yote ya walipa kodi yanayotokana na utoaji wa huduma za kodi au maamuzi ya kiutawala yanayofanywa na TRA.

***Nani anaweza kulalamika?

Kuhusu ni nani anaweza kulalamika, Manyama anasema ni mtu yoyote ambaye haridhishwi na utendaji katika maeneo tajwa, mlalamikaji anatakiwa na sheria kuwa amewasilisha malalamiko kwa msuluhishi ndani ya siku 90 tangu kutokea kwa hilo lalamiko.

***Nani anaweza kulalamikiwa

Kuhusu ni nani anaweza kulalamikiwa, Manyama anasema inaweza kulalamikiwa TRA, Kamishna Mkuu wa TRA na mfanyakazi yeyote wa TRA ambaye anakiuka mambo matatu tajwa.

Anasema kwa mujibu wa Sheria ya TOST, malalamiko hayo yatashughulikiwa ndani ya siku 30 na kutoa mapendekezo yake kwa Waziri wa Fedha ndani ya siku 14.

Hata hivyo, utekelezaji huo ndani ya siku 30 unategemea huyo mlalamikaji kapeleka taarifa kuhusiana na lalamiko lake ndani ya muda gani.
***Nafasi ya mwanasheria

Aidha, Manyama anasema taasisi hiyo hahitaji kuweka uwakilishi wa kutumia mwanasheria, mtu binafsi anaweza kuwasilisha lalamiko lake na likashughulikiwa.

***Mbinu inayotumika kutatua malalamiko

Anasema taasisi hiyo inatumia zaidi majadiliano na kushirikishana kwa kuangalia uhalisia wa tatizo na sio kwa kutumia sheria, lakini sio kuvunja sheria.

“Tunaangalia tatizo kwa uhalisi wake, limetokeaje na kuona namna ya kukusaidia ili uweze kuendelea kutelekeza wajibu wako,” anasema Manyama.

Anasema katika kutekeleza majukumu yake, TOST inazingatia misingi ifuatayo, msingi wa kuanza ni kwamba ni taasisi huru , ambayo haingiliwi na taasisi nyingine wala mtu yeyote au kuzingatia maelekezo wanapokuwa wanshughulikia suala la malalamiko ya kodi.

Msingi wa pili, kuhakikisha haki za mlipa kodi na mtoza kodi zinalindwa, taasisi haiengemei upande wowote wa mlipa kodi au mtoza kodi.

Anataja msingi mwingine ni kushughulikia malalamiko kwa gharama nafuu, kwa kuondoa urasmu usioleta ufanisi.

Msingi mwingine ni kushughulikia malalamiko kwa kuangalia uhalisia mazingira ambayo yamesababisha malalamiko kutokea. Alisema taasisi hiyo ina jukumu la kutunza nyaraka na taarifa kwa usiri mkubwa, isipokuwa zitakapotakiwa kwa mujibu wa sheria.

“Hiyo ndiyo misingi inayozingatiwa katika kutenda haki,” anasema Manyama. Hata hivyo anasema taasisi haimlazimishi mtu kupeleka malalamiko hayo kwenye taasisi, bali mtu anaweza kuamua kwenda mahakamani.

Naye Meneja wa Malalamiko na Usajili, Naomi Mwaipola, anasisitiza kuwa Taasisi hiyo inatoa huduma bure kwa wananchi na imejipanga kuwahudumia katika mikoa yote nchini na kutoa rai kwa wahariri hao kufikisha taarifa kwa umma.

“Ninatazamia na ninawaamini kuwa ninyi ni wajumbe wazuri kwa haya mliyosikia na mtapeleka ujumbe kwa Watanzania watakaokuwa wanahitaji huduma yetu na tunafika popote licha ya kuwa Makao Makuu yetu yapo Dodoma, ukiwa mkoa wowote unaruhusiwa kuleta changamoto yako na sisi tutakufikia,’’nasema Mwaipola.

Taasisi ya TOST ilianzishwa mwaka 2019 kwa marekebisho yaliyofanywa katika sheria ya usimamizi wa kodi ya mwaka 2015 na inafanya kazi nchi nzima, na mifumo yake imeanza kujengwa mwaka 2023 ambapo imeanza rasmi kutoa huduma kwa wananchi.

Kutokana na uwepo wa taasisi hiyo sasa wanaoweza kulalamikiwa mbele ya taasisi hiyo ni TRA yenyewe, Kamishna Mkuu wa TRA au mfanyakazi wa mamlaka hiyo.