Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online. Zanzibar
KAIMU Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Sweke amesema kuanza kwa sheria mpya na kanuni za kusimamia na kuendeleza uvuvi wa bahari kuu, kutaongeza uwekezaji wazawa katika bahari na kuisaidia sekta hiyo kwenda mbele.
Sweke ameyasema hayo katika mkutano wa siku moja ulioshirikisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, uliofanyika Ukumbi wa Takwimu Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Amesema sheria hiyo na kanuni zake, inalenga kuchochea uwekezaji katika uchumi wa bluu hasa kwa wazawa katika kuiendeleza sekta hiyo kwani zipo nchi nyingi, zimefanikiwa kutokana na kujiendesha kwa uvuvi na utalii.
Kaimu Mkurugenzi huyo amesema, ili kufikia lengo hilo katika utungaji wa sheria hiyo wametoa vivutio kwa wazawa, hasa kwa vitu ambavyo vinahitaji gharama kubwa ikiwemo vifaa vinavyoingizwa kwa ajili ya uvuvi, kupunguza ada ya leseni na vifaa vingine.
Amesema wazawa wanaweza kufaidika na uvuvi wa bahari kuu, iwapo sekta binafsi zitawekeza katika eneo hilo na kupata faida ikiwemo ajira, chakula na viwanda kukua.
“Wavuvi wetu wadogo wadogo hawana uwezo wa kuvua bahari kuu na badala yake, maji yetu yanavuliwa na meli za nje na kusababisha Tanzania kutofaidika,” alisema.
Sweke amesema, Tanzania ilikuwa inapata chini ya asilimia 10 ya faida katika uvuvi wa bahari kuu hivyo kupitia sheria hiyo mapato ya nchi yanaweza kukua kutokana na uvuvi huo.
Akiwasilisha mada ya sheria na kanuni za mamlaka Ofisa Sheria kutoka mamlaka hiyo, Keis Issa Abdalla amesema sheria hiyo imezingatia mambo mbalimbali ikiwemo uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali katika ukanda wa uchumi wa Bahari ya Tanzania (EEZ).
Amesema mambo mengine ni kuongeza wigo wa mipaka ya usimamizi wa meli zenye kupeperusha bendera ya Tanzania na kuzingatia mikataba na miongozo ya kikanda na ya kimataifa ya usimamizi wa ukanda wa uchumi wa bahari na rasilimali za uvuvi zinazopatikana baharini.
Abdalla amesema, sheria kifungu cha 45 na kanuni 47 imetoa fursa kwa mwekezaji mzawa au kampuni ya Kitanzania, inayomilikiwa kwa zaidi ya hisa 51 na mzawa kuomba vivutio kupitia mamlaka.
Mbali na hayo amesema, sheria hiyo pia imetoa punguzo la ada ya leseni za wavuvi kwa wawekezaji wazawa kwa muda wa miezi sita kwa meli zenye urefu wa mita zaidi ya 50 ni dola 13,500 kwa mzawa na mgeni ni dola 545,000 sawa na upungufu wa asilimia 30, wakati meli zenye urefu wa zaidi ya mita 24 leseni ya miezi sita kwa mzawa atatoa dola 5,000 na mgeni dola 31,000, sawa na upungufu wa asilimia 16.
Amesema hatua hiyo, imefanywa kwa lengo la kutoa fursa na unafuu wawekezaji wazawa, kushiriki katika uvuvi wa Bahari Kuu.
More Stories
Tanzania ipo tayari kupokea wakuu wa nchi,mkutano wa nishati-Dkt.Kazungu
Chunya yafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
HGWT yawarejesha kwao wasichana 88 waliokimbia ukeketaji