November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Korogwe TC yatoa mikopo ya sh. mil. 97

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe

HALMASHAURI ya Mji Korogwe (Korogwe TC) mkoani Tanga imetoa mikopo yenye thamani ya sh. milioni 97 kwa vikundi 16 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2022.

Ni asilimia kumi ya Mapato ya Ndani pamoja na marejesho yatokanayo na mkopo.

Wakati halmashauri hiyo inakopesha fedha hiyo sh. milioni 97, tayari ilishatoa sh. 568,204,502 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2021/2022 kwa vikundi 166 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo katika fedha hizo, sh. 408,904,502 ni za asilimia 10, na sh. milioni 159.3 ni marejesho.

Hayo yalisemwa Januari 11, 2023 na Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji Korogwe Rehema Letara, kwenye hafla fupi iliyofanyika Uwanja wa Soko la Manundu mjini Korogwe, na mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Dkt. Alfred Kimea.

“Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2021/2022 halmashauri imetoa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yenye jumla ya sh 568,204,502. Kati ya hizo, asilimia 10 ni sh. 408,904,502, na marejesho sh. 159,300,000.”

Fedha hizi zimekopesha vikundi 166. Aidha, vikundi vya wanawake vilivyokopeshwa ni 90 na walipata sh. 314,231,815 na wamerejesha sh. 122,072,687, vijana vikundi 55 sh. 236,422,730 na wamerejesha sh. milioni 74.7, na watu wenye ulemavu 21 mkopo wa sh. milioni 131.9 na wamerejesha sh. 53,534,300.

“Katika kipindi cha Julai hadi Desemba, halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya sh. milioni 97 kwa vikundi 16 Fedha hizi ni asilimia kumi ya Mapato ya Ndani pamoja na marejesho yatokanayo na mkopo” alisema Letara.

Dkt. Kimea alivitaka vikundi hivyo kutumia fursa ya mikopo kutoka halmashauri ili viweze kujikwamua kiuchumi, huku akivitaka vikundi hivyo kurudisha mikopo hiyo kwa wakati muafaka ili watu wengine waweze kukopa.

Diwani wa Kata ya Manundu Rajab Mzige ambaye pia alimuwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe Francis Komba, alisema fedha hizo za mkopo hazina riba kama zinavyofanya taasisi za fedha, hivyo ni wakati muafaka kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuchangamkia mikopo hiyo.

Mmoja wa watu wenye ulemavu, Tandu Mwanga ambaye ni mlemavu wa macho kutoka kikundi cha Chinuche Kata ya Masuguru, alisema wanaishukuru halmashauri kwa kuinua maisha ya wananchi, kwani awali kikundi chao kilikopeshwa sh. milioni mbili (2019/2020) na kuweza kununua ng’ombe mmoja wa maziwa, na mwaka huu wa fedha 2022/2023 wamekopeshwa sh. milioni tisa, na kununua bajaj.

“Tunaishukuru halmashauri kwa kuendelea kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja kwa kutoa mikopo. Awali tulikopeshwa fedha tukanunua ng’ombe, na safari hii tumekopeshwa fedha tumechukua bajaji.Walemavu tusijione wagonjwa. Walemavu wanaweza kufanya chochote. Na hata vijana wasikae vijiweni na kuanza kusema hakuna ajira, bali wajitume kwa kuomba mikopo na kufanya kazi za ujasiriamali” alisema Mwanga.

Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Dkt. Alfred Kimea (kushoto) akikata utepe kwenye hafla fupi ya kukabidhi mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa Halmashauri ya Mji Korogwe iliyofanyika Januari 11, 2023 kwenye Uwanja wa Soko Kuu la Manundu. Baadhi ya mikopo hiyo ni bajaji na guta. Kulia ni Diwani wa Kata ya Manundu Rajab Mzige. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Dkt. Alfred Kimea (wa nne kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya sh. milioni 97 kwa vikundi 16 vya ujasiriamali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mkopo uliotolewa na Halmashauri ya Mji Korogwe. Hafla hiyo ilifanyika Januari 11, 2023 kwenye Uwanja wa Soko Kuu la Manundu. (Picha na Yusuph Mussa).
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Dkt. Alfred Kimea (ndani ya bajaj) akiwa kwenye moja ya bajaj iliyotolewa kama mkopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwenye Halmashauri ya Mji Korogwe katika hafla fupi iliyofanyika Januari 11, 2023 kwenye Uwanja wa Soko Kuu la Manundu. Wengine ni Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Korogwe Frank Fuko (wa pili kulia), Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji Korogwe Rehema Letara (kulia), Mwenyekiti wa Mtaa wa Manundu Kati Mussa Mgosi (wa pili kushoto), na Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kwamsisi Vicent Singo (kushoto). (Picha na Yusuph Mussa)
Bajaj na guta (pikipiki ya miguu mitatu) ni moja ya vitu vilivyotolewa kama mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na Halmashauri ya Mji Korogwe. Hafla ya kukabidhi mfano wa hundi ya sh. milioni 97 na bajaj na guta, ilifanyika Januari 11, 2023 kwenye Uwanja wa Soko Kuu la Manundu, Korogwe. (Picha na Yusuph Mussa).