November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Korogwe inaongoza ukusanyaji mapato TRA

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewapongeza wafanyabiashara wa Wilaya ya Korogwe kwa kuweza kulipa kodi kwa hiyari, huku wakiongoza wilaya za mkoa huo kwa kulipa kodi kila mwezi.

Imesema kuwa Katika wilaya nane za Mkoa wa Tanga ukiacha Wilaya ya Tanga, Wilaya ya Korogwe inaziongoza wilaya nyingine kwa makusanyo ya kodi, ambapo kila mwezi Wilaya ya Korogwe inakusanya kati ya sh. milioni 400 hadi sh. milioni 500.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Thomas Masese kwenye Mkutano wa Wafanyabiashara wa Wilaya ya Korogwe, TCCIA na uongozi wa TRA,uliofanyika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe.

“Napenda kuwapongeza wafanyabiashara wa Wilaya ya Korogwe kwa ulipaji wa kodi kwa hiyari, kwani Wilaya ya Korogwe katika Mkoa wa Tanga ndiyo inaongoza kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Kwetu kwa upande wa TRA, Korogwe inakusanya kwa wastani sh. milioni 400 hadi sh. milioni 500 kwa mwezi” amesema Masese

Masese amesema kodi inayotozwa kwa wafanyabiashara ni rafiki, lakini baadhi ya wafanyabiashara wanaua mitaji yao kwa kukosa usimamizi wa kubaini viashiria vya kuua biashara zao ikiwemo pango la nyumba.

“Biashara zinazokufa hazisababishwi na TRA, bali usimamizi wetu, kwani kodi inayochukua TRA ni ndogo sana,Mfano mtu ameweka duka, lakini pango analipa sh. milioni 20 kwa mwaka, tena anatakiwa alipie mwaka mzima, lakini TRA kwa mwaka analipia sh. milioni 1.5 au milioni mbili kwa mwaka” amesema Masese.

Wakichangia mada, baadhi ya wafanyabiashara walisema kulipa kodi ndiyo msingi wa kwanza kwa nchi kujitegemea, huku wakihamasishana kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa, kwani duniani kote, hakuna nchi ambayo haikusanyaji kodi kutoka kwa wananchi wake kutokana na shughuli mbalimbali wanazofanya.

“Wafanyabiashara tulipe kodi,duniani kote hakuna nchi wananchi wake hawalipi kodi, Kodi ni muhimu sababu ndiyo inasaidia kupeleka huduma za jamii kwa wananchi” amesema Julius Mwandambo, mfanyabiashara wa duka la rejareja Mtaa wa Masuguru, Halmashauri ya Mji Korogwe.

Naye Mfanyabiashara wa duka la rejareja Nico Isanzu kutoka Mtaa wa Masuguru, Halmashauri ya Mji Korogwe amesema kwa kipindi cha miaka miwili, Meneja wa TRA Wilaya ya Korogwe Evason Lushaka amefanya kazi kubwa, kuleta utulivu na kukusanya kodi kwa umahiri mkubwa bila kuleta kero kwa wafanyabiashara.

“Meneja wa TRA Wilaya ya Korogwe (Lushaka) ni mtumishi mkarimu, na Mwalimu anaeheshimu mlipa kodi” amesema Isanzu.

Kwaupande wake, Ofisa wa TRA Wilaya ya Korogwe Innocent Mushi ameeleza umuhimu wa kulipa kodi ambapo amesema umuhimu wa kodi ni chanzo kikuu cha mapato ya Serikali kinachofanya kutekeleza majukumu yake.

“Na matumizi ya kodi ni kuendesha shughuli za Serikali, ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji, na kugharamia huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na maji,”amesema Mushi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Masese amesema moja ya sababu inayowalazimisha TRA kutembelea sehemu za biashara ili kufanya makadirio, badala ya kusubiri ofisini, ni baadhi ya wafanyabiashara kuweka makadirio madogo tofauti na biashara zao.

“Wakati mwingine inatufanya tuweze kutembelea maeneo ya biashara ili kujiridhisha na makadirio yaliyowekwa na mfanyabiashara, kwani baadhi ya wafanyabiashara hawasemi ukweli kwenye makadirio ya biashara zao” amesema Masese.