September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kongamano la usafi wa Mazingira kuboresha afya za wananchi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu Dkt.Dotto Biteko amewaagiza wadau wanaohusika na udhibiti na utoaji wa huduma ya usafi wa mazingira ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA),Wizara,Mamlaka za Serikali za Mitaa,sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali , waimarishe ushirikiano hasa katika utoaji wa huduma hiyo kwa lengo la kuboresha afya za wananchi.

Dkt.Biteko ameyasema hayo jijini Dodoma katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu William Lukuvi katika Kongamano la kwanza la Usafi wa Mazingira lililoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

Kongamano hili limeenda sambamba na uzinduzi wa Mwongozo wa Usimamizi wa Huduma za Usafi wa mazingira na tope kinyesi na uzinduzi wa Mfumo ulioboreshwa wa uwasilishaji wa taarifa za mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira (MAJIS) .

Aidha Dkt.Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati ameagiza kuwekwa kwa mazingira mazuri ili kuwezesha jitihada za sekta binafsi katika kuendeleza na kutoa huduma za usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini 

Kwa mujibu wa kiongozi huyo ,wakati umefika wa kuanza kutumia teknolojia sahihi ambazo zitafaa kuendana na mahitaji ya watumiaji na kuhakikisha kuwa vinafaa katika hali halisi na vinafikia viwango vya kiufundi na zinazuia madhara yanayoweza kujitokeza na pia kuchangia katika usimamizi salama wa usafi wa mazingira 

“Kila mtu awajibike katika kuendeleza usafi wa mazingira katika sehemu zote tunapoishi kwa kuwa na mipango jumuishi na kwa kuweka vipaumbele katika makazi duni ambapo kuna vihatarishi vingi vya afya. “amesema Dkt.Biteko na kuongeza kuwa

“Inatia faraja kuona muongozo huo unalenga kulinda mazingira na unaenda sambamba na miongozo mingine ya Kitaifa na Kimataifa ikiwemo mipango ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi shupavu wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inatekeleza miradi ya kimkakati ya kujenga mfumo wa uondoaji wa maji taka katika mji yote na makao makuu ya mikoa nchini. “

Amesema ,uongozi huu umezingatia dhima namba 6.2.1 ya Malengo ya Maendeleo endelevu inayolenga kuhakikisha kunakuwepo uwiano mzuri wa watu wanaotumia huduma salama za maji za usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na huduma ya kunawa mikono kwa sabuni na maji .

Aidha amesema kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kuboresha huduma za usafi wa mazingira kwa kutekeleza miradi ya ujenzi ya miundombinu ya maji taka katika maeneo mbalimbali nchini. 

“Takwimu kwa Wizara ya maji zinaonesha kuwa kufikia Aprili mwaka huu mtandao wa maji taka umefikia kilometa 1,455.93 ikilinganishwa na kilometa 1,416.9 za Aprili mwaka jana ambapo idadi ya maunganisho katika mtandao wa ukusanyaji na usafirishaji na kutibu maji taka imefikia kilomita 58,650 kutoka maunganisho 56,923 katika kipindi kama hicho .”amesema

Dkt.Biteko amesema taarifa ya utendaji wa Mamlaka ya Maji Safi katika mwaka wa fedha wa 2022/23 zinaonesha kuwa mamlaka ya Majisafi na Usafi wa mazingira 21 tu kati ya 85 sawa na asilimia 24.7 ndio zimekuwa na miundombinu ya kutibu majitaka na tope kinyesi.

Amesema,kwa takwimu hizo ni dhahiri kwamba bado kuna changamoto kubwa katika eneo hilo .

Awali Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameipongeza EWURA kwa Kongamano hilo ambalo ndio limefanyika kwa mara ya kwanza huku akisema Mwongozo huo utasaidia mamlaka za maji na wadau mbalimbali katika usimamizi wa huduma za mazingira na tope kinyesi pamoja na kuboresha mfumo wa Majis ili kujumuisha taarifa za usafi wa mazingira.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA James Andilile amesema kuwa kongamano hilo limefanyika kwa kutambua kuwa usafi wa mazingira ni afya .

Kwa mujibu wa Anfilile,katika tathmini waliyofanya na kuzingatia tafiti zilizofanywa kwenye karne ya 19 ,ilithibitika pasipo mashaka kwamba pale watu wanapokaa katika mazingira mazuri au yenye usafi afya zao zinakuwa imara zaidi na kujikinga na magonjwa mengi.

“Ni kweli kwamba serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika kuimarisha afya za watu wake ikiwemo suala la upatikanaji wa maji safi kwa wingi ambayo inasimamiwa na wizara ya maji.”amesisitiza