Na Penina Malundo, Timesmajira
Wadau mbalimbali kutoka Nchi za Afrika Mashariki wamekutana jijini Arusha katika Kongamano la kwanza Nishati Safi ya Kupikia la Afrika Mashariki linalolenga kujadili masuala mbalimbali yatakayowezesha Jumuiya hiyo kuondokana na matumizi ya Nishati isiyo safi ya kupikia na kwenda kwenye nishati safi ya kupikia.
Akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika ufunguzi wa kongamano hilo, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amesema kuwa Kongamano limehusisha washiriki kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi huku nchi ya Malawi ikishiriki kwa nia ya kujifunza jinsi nchi za Afrika Mashariki zinavyotekeleza Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia.
“Kongamano hili linahusisha majadiliano ya namna ya kutekeleza kwa ufanisi ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwemo masuala ya teknolojia, ufadhili wa miradi ya Nishati Safi ya Kupikia, Sera na miongozo mbalimbali na kubadilishana uzoefu huku Tanzania ikiwa ndiye kinara katika utekelezaji wa ajenda hii ya Nishati Safi ya Kupikia.” Amesema Mhandisi Luoga

Ameongeza kuwa, “Kwa Tanzania safari ya Nishati Safi ya Kupikia tuliianza rasmi mwaka 2022 ambapo Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan alianzisha mjadala wa nishati hii kupitia wadau mbalimbali na kutoa maelekezo mbalimbali ikiwemo ya kuanzishwa kwa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ambao ulizinduliwa mwaka 2024 unaoelekeza kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanapaswa kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034.”
Ameeleza kuwa, Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wanatumia Nishati Safi ya Kupikia ikiwemo kugawa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku, kutoa elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa makundi mbalimbali ya Wananchi na kusambaza gesi asilia kwa njia ya bomba kwa wananchi katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam kwa ajili ya kupikia.
Ameongeza kuwa, hatua nyingine zinazochukuliwa ni kuweka unafuu wa kodi kwa baadhi ya vifaa vya nishati safi ya kupikia vinavyoingia nchini pamoja na kupitia sheria, kanuni na sera ili kuangalia maeneo yatakayorahisisha upatikani wa nishati safi ya kupikia.

Amesema, watu takribani bilioni 2.1 duniani hawatumii Nishati Safi ya Kupikia huku katika nchi zilizo kwenye Ukanda wa Jangwa la Sahara watu wakiwa ni milioni 990. Kwa upande wa Tanzania amesema watu wanaotumia Nishati Safi ya Kupikia wamefikia takribani asilimia 16 lakini Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha wananchi wote wanatumia nishati hiyo.
Katika hatua nyingine, Kamishna Luoga amesema uwepo wa umeme wa kutosha nchini ambao sasa umefikia megawati 4,031 unatoa uhakika pia wa wananchi kutumia nishati safi ya kupikia kupitia majiko ya umeme.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) Shigeki Komatsubara ameipongeza Serikali ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kwa kuwezesha kufanyika kwa Kongamano hilo muhimu.
Ameeleza kuwa uwepo wa Watendaji wa Serikali wa Nchi za Afrika Mashariki katika Kongamano husika ni uthibitisho wa dhamira thabiti ya nchi hizo katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya Nishati Safi ya Kupikia inayolenga katika kuwa na matumizi ya teknolojia safi, bora na endelevu ya kupikia.

Komatsubara amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia jitihada mbalimbali huku kielelezo kikiwa ni uwepo wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao ni Dira katika kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.
Amesema suala la Nishati Safi ya kupikia si la Tanzania pekee bali ni la dunia nzima hivyo ushirikiano unahitajika ili kuhakikisha Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia inafanikiwa duniani kote kwani ni suala linalohusu usalama wa afya na mazingira na kusisitiza kuwa Umoja ni Nguvu na utengano ni udhaifu.

Naye, Mwakilishi kutoka Umoja wa Ulaya, Lemine Diallo amesema lengo kubwa la Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ni kuhakikisha kila kaya barani Afrika inatumia Nishati Safi ya Kupikia, ya kisasa na endelevu.
Amesema katika nchi za Afrika Mashariki zaidi ya asilimia 90 ya watu bado wanategemea kuni na mkaa kama vyamzo vikuu vya Nishati Safi ya Kupikia suala ambalo linaleta athari mbalimbali ikiwemo afya, mazingira na maendeleo kwa ujumla.
Amesema Umoja wa Ulaya unaunga mkono juhudi za kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa namna mbalimbali kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Uwekezaji la UNCDF ikiwemo kutoa ruzuku kwa ajili ya kuendeleza mitaji katika uzalishaji na usambazaji wa nishati safi na salama.

Kwa upande wao, Wawakilishi kutoka nchi za Uganda, Kenya, Malawi na Rwanda kwa nyakati tofauti katika Kongamano hilo wamempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na maono ya kuhakikisha kuwa Afrika inahamia katika Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia huku nchi ya Kenya ikieleza kuwa takriban watu 26,000 wanafariki kwa mwaka kwa magonjwa yanatokana na matumizi ya Nishati Safi isiyo safi kama vile kuni na mkaa.
Pia wawakilishi hao wameipongeza Tanzania kwa kuandaa kwa mafanikio Kongamano hilo la kwanza kwa Nchi za Afrika Mashariki.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria Kongamano hilo ni pamoja na Mshauri wa Rais katika Masuala ya Nishati Safi ya Kupikia, Angellah Kairuki, Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt.John Mboya, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Mhandisi Imani Mruma na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay.
Kongamano limeandaliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Uwekezaji (UNCDF) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya.
More Stories
RMO,DMO waagizwa kumsimamia Mkurugenzi ununuzi vifaa ,vifaa tiba
Mgogoro wa mipaka Ushetu,Kaliua watua Bungeni
Serikali ya nunua hereni za kidijitali kwajili ng’ombe,mbuzi na kondoo