


Na Joyce Kasiki, Dodoma
KATIKA jitihada za Serikali kupambana na janga la dawa za kulevya, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Jinsia na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amefungua rasmi Kongamano la Elimu kwa Vijana juu ya Madhara ya Matumizi ya Dawa za Kulevya lililofanyika jijini Dodoma, huku akitoa wito kwa vijana kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao.
Akizungumza wakati akifungua kongamano hilo leo Juni 24,2025 jijini Dodoma lililohudhuriwa na mamia ya wanafunzi kutoka shule za sekondari, vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za elimu, Dkt. Gwajima alisema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka nguvu kubwa katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini, kwa kuhakikisha upatikanaji wa tiba, elimu, na uwezeshaji wa vijana wanaoathirika na tatizo hilo.
“Rais wetu amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba tunajenga taifa salama kwa vijana. Tumewekeza katika nyumba za upataji nafuu, kliniki za kutibu waraibu, na sasa tunapeleka vijana waliopona kwenye vyuo vya ufundi ili wapate stadi za kazi na kujitegemea,” meisema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima aliongeza kuwa Serikali haitachoka kuwekeza katika kinga na tiba kwa waathirika, lakini pia aliitaka jamii kutambua kuwa kila kijana anayepotea kwa dawa za kulevya ni hasara kwa Taifa.
“Tunatumia fedha nyingi kuwaokoa vijana waliodanganywa kuingia katika uraibu badala ya kutumia rasilimali hizo kuendeleza maendeleo ya Taifa,hii ni changamoto tunayopaswa kuikabili kwa pamoja,” amesisitiza.
Takwimu zatisha
Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya dawa za kulevya ya mwaka 2024, jumla ya watu 9,362 walipata huduma za tiba ya uraibu katika vitengo vya afya ya akili, huku waraibu 15,637 wakihudumiwa kwenye vituo vya afya kutokana na matumizi ya dawa za kulevya kama afyuni, bangi, na milungi.
Wito kwa Jamii
Pamoja na juhudi za Serikali, Dkt. Gwajima alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa jamii nzima, ikiwa ni pamoja na wazazi, walimu, viongozi wa dini na vijana wenyewe.
“Tunahitaji wanaume na wanawake kushiriki katika kuelimisha jamii. Vijana, tumieni mitandao ya kijamii kueneza taarifa sahihi. Uraibu si fasheni, ni janga la kitaifa,” alisisitiza Waziri.
Awali Kamishna Generali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo, amesema kuwa idadi kubwa ya waathirika ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 25, wengi wao wakiwa wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu.
“Katika operesheni mbalimbali tumeweza kubaini kwamba makundi rika yanayoeneza upotoshaji ndiyo chanzo kikuu cha vijana kuingia kwenye matumizi ya dawa hizo. Wengine huambiwa kuwa bangi inasaidia kusoma au kuongeza uwezo wa kufaulu mitihani, jambo ambalo siyo la kweli,” ameeleza Kamishna Lyimo.
Kaulimbiu ya Dunia Yasisitizwa
Kongamano hilo liliambatana na ujumbe wa kimataifa wa mwaka huu unaosema “Wekeza kwenye kinga na tiba dhidi ya dawa za kulevya.” Kaulimbiu hiyo imechochea Serikali kuongeza kasi ya uwekezaji kwenye huduma za matibabu, elimu, na ustawi wa kijamii kwa waathirika.
Aidha, ilielezwa kuwa Serikali inajenga kituo kikubwa cha utengemao cha kitaifa kitakachowahudumia vijana waliopata nafuu kutoka uraibu kwa kuwapa elimu ya ufundi stadi na ujuzi wa kujitegemea.
Sauti za Vijana
Joshua Siliakusi, mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ameeleza kuwa ukosefu wa ajira ni kichocheo kikubwa kinachowasukuma vijana kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya. Alishauri Serikali kuwekeza zaidi katika ajira na mikopo kwa vijana.
“Vijana wanahitaji kuona mwanga mbele ya maisha yao. Ajira na fursa za kiuchumi ndizo suluhisho la kudumu katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya,” amesema.
Kwa upande wake, Saumu Mode kutoka Chuo cha Mipango amehimiza vijana kujiepusha na makundi yasiyofaa wanapokuwa vyuoni, na badala yake wajikite katika masomo ili kufikia ndoto zao.
“Kwa ujumla, kongamano hilo limeweka msisitizo mkubwa katika kuokoa kizazi cha sasa kwa kutoa elimu, matibabu na nafasi za kujikwamua kiuchumi, ili kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za matumizi ya dawa za kulevya kwa Taifa la Tanzania.”

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi