December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kondo aelezea kilichomkwamisha kwa Kagera, Polisi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KOCHA Mkuu wa timu ya Manispaa ya Kinondoni, KMC FC, Habib Kondo amesema bado ana imani na kikosi chake licha ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) msimu huu.

KMC ilipoteza mchezo namba 28 dhidi ya wenyeji wao Kagera Sugar uliochezwa katika uwanja wa Kaitaba na pia kuruhusu goli 1-0 katika mchezo namba 45 uliochezwa Oktoba 5 dhidi ya Polisi Tanzania.

Kondo ametoa kauli hiyo katika mazoezi yao yaliyoanza jana kwenye uwanja wa Uhuru kujiandaa na mchezo wa mzunguko wa sita dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Oktoba 14 katika Uwanja wa Uhuru.

Amesema, kupitia mazoezi hayo, timu hiyo itajiandaa kikamilifu ili kujiweka sawa dhidi ya wapinzani wao kwani kitu cha kwanza anachoanza nacho ni kurekebisha makosa yaliyofanywa na wachezaji wake katika michezo iliopita.

Kocha huyo amesema kuwa, anakiamini kikosi chake kina uwezo wa kufanya vizuri ila kikubwa kwa sasa ni kuendelea kujenga utulivu kwenye safu ya ushambuliaji ili kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.

“Timu inatengeneza nafasi nzuri za kufunga lakini kwenye umaliziaji inakuwa changamoto, kupitia mazoezi haya, tunakwenda kukisuka kikosi chetu ili kwenye michezo ijayo tupate matokeo ambayo awali tulikuwa tukiyapata,” amesema Kondo.

Hadi Ligi inasimama kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ya Tanzania, timu hiyo ilikuwa inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi tisa walizopata baada ya kushinda mechi tatu na kupoteza mbili.