January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kocha mpya ataka soka la kushambulia, aahidi furaha kwa mashabiki

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

KOCHA mpya wa klabu ya Yanga, Mohamed Nasreddine Nabi ameweka wazi kuwa kazi ya kwanza atakayoanza nayo ndani ya klabu hiyo ni kufumua mfumo unaotumika sasa na kuja na mpya ambao utawapa matokeo mazuri katika kila mchezo ulio mbele yao.

Jana Yanga imemtambulisha rasmi kocha huyo aliyetua hapa nchini na kusaini mkataka wa mwaka mmoja na nusu kuitumikia klabu hiyo ambayo ipo kwenye mbio za kuwania ubingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo ameambatana na kocha msaidizi Sghir Hammadi ambaye pia amesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu lakini pia wanamsubiri kocha ya viongo ambaye ataungana naye kwenye benchi la ufundi ili kuirejeshea makali timu hiyo.

Mara baada ya kutambulishwa kocha huyo ameweka wazi kuwa, Yanga ina kikosi kizuri na wachezaji wanaojituma ila shida ipo kwenye mbinu na mfumo wanaotumia ambao unawakosesha vitu vingi.

Amesema kuwa, atahakikisha anaboresha zaidi eneo hilo na kuja na falsafa yake ambayo itahusisha zaidi kucheza soka la kushambulia na si kujilinda.

“Mimi ni kocha na falsafa yangu ni ya wazi kwani napenda zaidi kucheza soka la kushambualia kuliko kujilinda ambalo linaweza kutupa matokeo mazuri, pia ninathamini kile nilichonacho na naamini Yanga ina wachezaji wazuri ambao wanahitaji kuongezewa vitu vichache ili kuwa bora zaidi,”

“Pia tunahitaji kutengeneza malengo na mikakati imara ambayo ni muhimu zaidi. Kwa sasa kitu tunachokihitaji ni kupewa muda kwani kuunda mkakati, kujenga kikosi imara na kuwa na falsafa bora ni kitu kinachohitaji muda,” alisema kocha huyo.

Hata hivyo kocha huyo aliweka wazi kuwa, matarajio yake ni kuhakikisha klabu hiyo inashiriki mashindano ya Ligi Mabingwa Afrika na kupata matokeo mazuri katika kila mchezo ulio mbele yao yatakayorusisha furaha ya mashabiki.

“Matarajio ya viongozi wa klabu hii pamoja na mashabiki ni kuona Yanga inarudi kwenye makali yake na kuwa miongoni mwa klabu kubwa Afrika hivyo kama kocha nitahakikisha nafanya kazi kwa uwezo wangu wote kutimiza matarajio ya wengo ili kurejesha furaha,”.

Wakati akimtambulisha kocha huyo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Haji Mfikirwa amesema, wamempa mkataba huo Nabi ambao una kipengele cha kuongeza na ametua na wasaidizi wake kwani wanajuana vizuri na wanaamini muunganiko wao utawapa mafanikio.

Amesema, kocha huyo amekuja sasa wakati Ligi inakaribia kuisha ili kumpa fursa ya kuiona na kuifahamu zaidi timu hiyo na hawana wasiwasi nae kwani analifahamu vizuri soka la Afrika.

“Tunaamini atatupa mafanikio makubwa na kutufikisha kule tunapopatarajia ikiwemo kukidhi kiu ya mashabiki wa Yanga. Kama mnakumbuka tumepitia hatua tofauti tofauti na kuwa na walimu mbalimbali lakini yote ni katika kujenga kikosi na ikiwa uongozi utaridhishwa na utendaji wa makocha hawa wapya basi tutawaongeza mkataba,” amesema kiongozi huyo.