January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kocha Morocco atema cheche kwa Waarabu

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

KOCHA mkuu wa timu ya Namungo FC, Hemed Seleman ‘Morocco’ amesema kuwa hana wasiwasi wowote kuelekea kwenye mchezo wao wa kesho wa Kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya timu ya El Hilal Obeid kutoka nchini Sudan kwani ana uhakika wataweza kuwashushia kipacho kikali kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

Katika michuano hiyo, Namungo itaanzia nyumbani katika mchezo utakaochezwa Desemba 23 katika dimba la Azam Complex huku mchezo wa marudiano ukichezwa Januari 5 nchini Sudan.

Namungo ilifanikiwa kusonga mbele katika michuano hiyo baada ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kufuta mechi ya marudiano dhidi ya timu ya Al Rabita ya Sudani Kusini uliotakiwa kuchezwa jana kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kupewa ushindi wa mezani na goli tatu.

Katika mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo uliochezwa Novemba 28, Namungo FC walipata ushindi mnono wa goli 3-0 zilizofungwa na Stephen Sey dakika ya 19 na 38 huku goli la tatu likifungwa dakika ya 63 na Shiza Kichuya.

Lakini baadaye CAF ilitangaza uamuzi wa kufuta mchezo wa marudiano baada ya Chama Cha Soka cha Sudani Kusini (SSFA) kushindwa kukamilisha taratibu kuhusu Waamuzi waliopangwa kuchezesha mechi hiyo.

Awali mchezo huo wa marudiano ulikuwa kuchezwa Sudani Kusini, lakini Al Rabita kupitia SSFA waliomba uchezwe Dar es Salaam kutokana na kutokuwa na uwanja ambao unakidhi matakwa ya Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) na la Afrika (CAF), kuendelea kufungwa kwa mipaka kutokana na Covid-19 pamoja na hali ya kiusalama nchini mwao kutokuwa shwari na ombi hilo kukubaliwa na CAF.

Kocha huyo ambaye alikuwa akikiandaa kikosi hicho visiwani Zanzibar, ameuambia Mtandao huu kuwa kuwa, tayari vijana wake wapo fiti kupambania ushindi katika mchezo huo wa kwanza dhidi ya wapinzani wao.

Amesema kuwa, katika mechi za kirafiki walizocheza visiwani humo, zimewaongezea kitu wachezaji wake na anaamini kuwa wataweza kuanza vizuri dhidi ya wapinzani wao ambao hadi sasa bado hawajajua watatumia mfumo gani.

“Tumeshinda mechi ya kirafiki dhidi timu ya Mafungo na kisha tukawafunga Zimamoto, jambo kubwa kwetu ni kuwa mechi hizi zimetuonesha mabadiliko makubwa ambayo yanatufanya kuingia katika mchezo wetu tukiamini kuwa tutapata ushindi monono,” amesema Morocco.