Na Angela Mazula, TimesMajira Online
KIKOSI cha timu ya KMC jana kimeanza rasmi mazoezi yake kuelekea mchezo wao wa Oktoba 30 dhidi ya wapinzani wao Gwambina GC utakaochezwa kwenye uwanja wa Gwambina Complex uliopo Misungwi.
KMC itakutana na wenyeji wao huku ikitaka alama tatu muhimu baada ya kupoteza mchezo wao uliopita dhidi ya Yanga ambao walikubali kichapo cha goli 2-1 wakitangulia kwa goli lililofungwa dakika ya 27 na Hassan Kabunda huku Yanga wakisawazisha dakika ya 41 kupitia kwa Tuisila Kisinda lakini mshambuliaji Waziri Junior aliifungia Yanga goli la ushindi dakika ya 61.
Matokeo hayo yamewapa machungu zaidi KMC ambao kwa sasa wanahaha kurudi kwenye makali yao waliyoanza nayo msimu huu ambapo walifanikiwa kushinda mechi tatu mfululizo.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Christina Mwagala amesema, kikosi chao kimeanza maandalizi kikiwa na morali ya hali ya juu kwani kitendo cha kupata sare katika mechi zao mbili zilizopita na kufunga mchezo dhidi ya Yanga kimewapa benchi la ufundi sababu zaidi ya kufanyia kazi makosa yaliyowagharimu.
Amesema kuwa, tayari bechi lao ufundi limeweka mikakati ya ushindi na kwa kuanza wanafanyia kazi makosa waliyoyaona kwenye mchezo dhidi ya Yanga.
“Mara baada ya mchezo wetu dhidi ya Yanga, kocha wetu Habib Kondo alifurahishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji kwani walicheza kwa morali ya hali ya juu tena kwa muunganiko mzuri zaidi hata ya wapinzani wetu hivyo nguvu hiyo ikioneshwa kwenye mchezo wetu ujao basi hatuna wasiwasi wa kuondoka na alama tatu, ” amesema Mwagala.
Hata hivyo alisema kuwa, wataingia katika mchezo huo bila kuwadharau wapinzani wao kwani ni miongoni mwa timu zenye bechi bora la ufundi.
“Japokuwa tunahitaji ushindi katika mchezo huu lakini tunatambua hautakuwa mwepesi kwetu na ili kupata alama zote tatu ni lazima tucheze kwa nidhamu kubwa na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ili kuwazidi nguvu na kuwafunga mapema, ” amesema Mwagala.
Kuelekea katika mchezo huo, KMC huenda wakamkosa beki wao Andrew Vicent ‘Dante’ambaye anaendelea na matatibabu baada ya kuumia katika mchezo wao uliopita dhidi ya Yanga.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania