November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Klabu za shule mwarobaini wa wanafunzi kujilinda dhidi ya ukatili

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa uanzishwaji wa klabu za wanafunzi katika shule za msingi na sekondari kupitia mashirika mbalimbali zimekuwa msaada kwa wanafunzi kujilinda na kuwalinda wenzao na vitendo kwa ukatili dhidi yao.

Baadhi ya wanafunzi kwa nyakati tofauti wakizungumza na timesmajira jijini hapa wameeleza namna Klabu hizo zilivyoweza kuwa msaada kwao dhidi ya ukatili wawapo nyumbani na hata shuleni.

Mmoja wa Wanahabari mtoto kutoka MYCN,mwanakikundi wa Klabu ya Gender katika shule ya sekondari Nyabulogoya Mwajabu Salum,ameeleza kuwa klabu hizo katika shule za msingi na sekondari zimekuwa muhimu sana kwa wanafunzi kuweza kujilinda na kupinga vitendo vya ukatili dhidi yao.

Ameeleza kupitia klabu ya gender wameweza kupata elimu ambayo imewasaidia kujitetea dhidi ya vitendo hivyo huku akitolea mfano kuwa unakuta mtoto kafanyiwa ukatili lakini anaweza kutoa taarifa tofauti na awali.

Pia imewasaidia watoto wa kike kuepuka mimba za utoto hivyo kuanzishwa kwa klabu za shule zimekuwa ufumbuzi katika masuala mbalimbali yanayohusu ukatili na haki za watoto ambapo imewezeshwa wanafunzi kuweza kutoa taarifa endapo kafanyiwa yeye vitendo hivyo au mwenzie.

“Kabla ya kujiunga na klabu hii ya shule nilikuwa siwezi kusimama mbele za watu,kujitetea au kutetea wengine kuhusu masuala ya ukatili dhidi yetu watoto lakini baada ya kujiunga na kupata elimu na kujengewa uwezo kuhusu namna ya kupinga ukatili,kujilinda na wapi pa kutoa taarifa nimekuwa mstari wa mbele katika kujitetea mimi na wenzangu,”ameeleza Mwajabu. na kuongeza kuwa

“Tangu kujiunga kwa klabu hiyo nimefanikiwa kumtetea mwanafunzi mwenzangu wa shule jirani ambaye alifeli mtihani wa kidato cha pili mwaka jana na akaambiwa arudie darasa mwaka huu na yeye alikuwa tayari kurudia lakini mzazi wake alikataa na kusema anapaswa aolewe lakini rafiki yangu anayesoma naye alinipa taarifa hiyo na mimi nikaona ni ukatili kwake hivyo niliamua kwenda nyumbani kwao pamoja na Mwenyekiti wangu wa Klabu kisha tukazungumza na kumuelimisha mzazi wake juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike na madhara ambayo atayapata ya kuolewa katika umri mdogo na mzazi alikiri kuwa alikuwa anaenda kumuozesha hivyo alikubali mtoto wake kuendelea na masomo na mpaka sasa anaendelea na masomo yake ya kidato cha pili,”.

Mwanaklabu ya watoto na vitabu ilio chini ya shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence Oliva Mathias ameeleza kuwa kupitia klabu hiyo imemuwezesha kufanya vizuri katika taaluma yake kwani amefahamu namna ya kujilinda na vitendo vya ukatili.

Pia kumemuwezesha kuwa na kipaji cha uchoraji na uandishi wa kitabu ambapo anaweza kuzuia ukatili kupitia hadithi inayohusiana na matendo ya ukatili na elimu juu ya ukatili ambapo kabla ya kujiunga na klabu hiyo hali haikuwa nzuri sana kwani walikuwa wanafanyiwa vitendo vya ukatili lakini kwa Sasa vimepungua.

Akizungumza na timesmajira kwa njia ya simu Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la kutetea wanawake na watoto la Haki Zetu Tanzania Evodius Gervas, ameeleza kuwa kupitia shirika lao walioanzisha klabu katika shule mbalimbali za sekondari na msingi mkoani hapa.

Gervas ameeleza kuwa amekuwa akikumbana na visa vya ukatili ambavyo vinakuwa vimeelekezwa kwao na watoto wenyewe ambao wapo katika klabu mbalimbali za shule.

Ameeleza kuwa kuna matukio mengi ambayo yamekuwa yakiripotiwa na hao watoto ambao wapo kwenye klabu hizo moja kwa moja kwenye shirika lao na hata Polisi lakini kabla ya kuwa na klabu hizo shuleni walikuwa hawawezi kuripoti kwa sababu awali walikuwa hawajui sehemu gani waripoti na nini wafanye baada ya kukutana na vitendo vya ukatili wao au wenzao.

“Kitu ambacho kimekuwa suluhisho na manufaa makubwa watoto wameweza kuongeza uelewa katika masuala ya ukatili na wametufanya sisi tuweze kupata wale watoto ambao wanasimama na kuwasaidia wenzao ambao wamekubana na ukatili kwa kuripoti na kuwaelekeza wapi wanaweza kwenda kupata msaada,”ameeleza Gervas.

Pia ameeleza kuwa klabu za shule zinawasaidia watoto kufanya vizuri katika masomo yao kwani unampo mlea mtoto katika mazingira ya nidhamu na kuweza kuepuka ukatili inasaidia kufanya vizuri darasani na uwezo wao wa kudadisi mambo unaongezeka na uwezo wa kujilinda na kujisimamia dhidi ya vitendo vya ukatili unaongezeka tofauti na mtoto ambaye hajajiunga na klabu za shule.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa bado kuna changamoto kwenye kuwawezesha wazazi kupata elimu ya ukatili kwani mashirika na serikali wamejikita zaidi katika programu za kuwajengea uwezo watoto ambao muda mwingi wanakuwa shuleni juu ya masuala hayo na kuwasahau wazazi.

“Hivyo bado wazazi uelewa wao siyo mkubwa ukiangalia programu nyingi zimeelekezwa shuleni na siyo mtaani hivyo unampo mjengea uwezo mtoto pekee yake jamii yake inaweza kuwa bado changamoto katika uelewa,nafikiri ni muhimu sana kuwekeza pia kwenye jamii kwa kuanzisha programu jumuishi ambazo zitajumuisha watoto, wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kwaio hii itasaidia kwamba watu wote watakuwa wanauelewa wa kitu kile kile kama ni ukatili wote watakuwa wanafahamu,”ameeleza Gervas na kuongeza kuwa

“Wakati mwingine ukimfundisha mtoto pekee yake kuhusu ukatili,mzazi kwa vile ana uelewa anaweza kuhisi kuwa mtoto wake ana kiburi,ameanza kuwa na jeuri,ni kitu kizuri kuangalia kuwa na programu ambazo zitajumuisha na wazazi na jamii na hii itaendelea kusaidia kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto,”.

Hata hivyo Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Edith Mokiwa,ameeleza Mokiwa hali ya vitendo vya ukatili siyo nzuri kwa watoto mfano kwenye robo moja unakuta kuna kesi ambazo zimeisha fikishwa mahakamani kesi 79 au 78 unakuta 46 ni za watoto ambao wamebakwa na kulawitiwa ndio maana wanafanya jitihada za kukabiliana na vitendo hivyo kwa kuzunguka shuleni kuwaelimisha watoto ili wakifanyiwa vitendo hivyo wasinyamaze kimya hata wakitishwa.

Baadhi ya wanafunzi wakiwa katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambayo uadhimisha Juni 16 ambapo kimkoa yamefanyika uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Haki Zetu Tanzania Evodius Gervas, akizungumza na timesmajira online ofisini mkoani Mwanza,juu ya namna Klabu za shule zinavyosaidia wanafunzi kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili.(Picha na Judith Ferdinand)