Na Philemon Muhanuzi, Timesmajiraonline
KULE kisiwani limemalizika tukio la wiki nzima lenye kujulikana kama Kizimkazi
Festivals. Ni wiki ya sherehe mbalimbali katika eneo alilozaliwa Mheshimiwa Rais
wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan.
Mwaka huu kwa jamii wa wapenda michezo tamasha hili limekuja na kuondoka na
ufunguzi wa shule maalum ya michezo.
Kwa kiingereza ikiitwa Academy. Imefunguliwa Kizimkazi Academy na picha mjongeo
za eneo hilo zinaendelea kutembea katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
Naamini hii ni shule ya kisasa na sio jina tu na mbwembwe zenye kwenda sambamba
na uwepo wa shule nyingi za michezo ambazo tumezoea kuziona katika sehemu
mbalimbali za Tanzania.
Ni matumaini yangu itakuwa ni shule yenye makocha wenye taaluma. Hakuna
anayependezwa kuiona academy ya viwango ikihusishwa na zile habari za undugu na
kujuana.
Kwamba wawepo makocha na wakufunzi wasio na elimu za kutosha za ufundishaji wa
michezo mbalimbali.
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua kuwa maisha haya ni mafupi yenye kujawa
kumbukumbu zinazoishi muda wote akaja na wazo la kujenga shule ya michezo.
Atakapokuwa tayari ni mstaafu awe na jina lenye kuendelea kuwa hai kupitia uwepo
wa wahitimu wenye kuipeperusha bendera ya Tanzania ambao ni zao la Kizimkazi
Academy.
Naamini mpaka kufikia hatua ya kuwa imekamilika shule hiyo maalum Mheshimiwa
Rais atakuwa alipita huko nje ili kupata ushauri wa ubora wa shule yenyewe.
Ni raia namba moja hivyo anao uwezo wa kupata wachoraji bora wa michoro ya namna
shule nzima inavyojengwa.
Anao uwezo wa kupata makocha wa ujunzi wa kulea vipaji vya wanamichezo
mbalimbali kuanzia wakiwa na umri mdogo.
Pia anao uwezo wa kutambua kuwa makocha wenye uzoefu wa kulea wanamichezo ndio
wenye kufaa kuiendesha shule hiyo.
Mheshimiwa Rais kaamua kupita mle mle alimopita Rais wa awamu ya nne Mzee Jakaya
Kikwete alipoamua kujenga shule changamani ya michezo pale katika eneo la
Gerezani.
Ni chanzo kingine cha wanamichezo wenye hadhi ya kushiriki michezo ya kimataifa
katika wakati wowote ule. Rais Samia ameweza kuuhakikishia umma kwamba
uanamichezo wake ni zaidi ya ule wa wanasiasa warasimu.
Kwamba sio uanamichezo wa kuishia kufurahia pale anapomulikwa na kamera za
runinga akiwa amekaa katika kiti maalum cha jukwaa la mgeni wa heshima pale
uwanja wa Taifa.
Wapo waliomchukulia kuwa ni mwanasiasa mtafuta kura kwa kujisogeza karibu na
michezo walipomuona amevaa tracksuit akielekea kukaa katika kiti maalum cha
uwanja wa Taifa na nyuma yake likiwepo kundi kubwa la walinzi na wasaidizi.
Ameamua kwa makusudi kwenda mbali zaidi katika suala zima la michezo.
Ameiheshimisha michezo kwa mapana yake.
Na naamini wadau wa michezo watatambua ni nguvu kubwa kiasi gani iliyotumika
katika kujenga hiyo shule maalum la ukuzaji wa vipaji vya wanamichezo.
Kuna haja ya makusudi kabisa ya kuunganisha Zanzibar kuwa kisiwa cha utalii na
suala la ukuzaji wa michezo.
Muingiliano wa watu huja na tija kwa pande zote mbili zenye kuingiliana kwa
sababu ya utalii kwa ujumla. Pia naamini kila anapokwenda huko nje katika masuala ya kiuchumi ya Tanzania anakuwa pia amesafiri na ujumbe wenye kuihusu michezo haswa hiyo Kizimkazi Academy.
Aliwahi kusema siku alipofanya kikao cha kwanza cha wazi na baraza la mawaziri kwamba hakuna mtu awezaye kuishi sawa na kisiwa kilivyo. Nauona uwepo wa wataalam wengi wa michezo mingi wakianza kumiminika huko visiwani kwa ajili ya shughuli zenye kuhusiana na Kizimkazi Academy.
Ni muda wa vijana wa visiwa vya Unguja na Pemba kuchangamkia uwepo wa shule hiyo ya vipaji.
Ule muda wa kulalamikia serikali wakati familia moja ina vijana wadogo wawili au
watatu wenye vipaji vya michezo mbalimbali, kwa sasa unakwenda kutoweka. Fursa ya bei ghali imesogezwa karibu na mitaa ya Unguja. Ndani ya miaka mitano ijayo inategemewa kuonekana timu ya vijana chini ya miaka 20 yenye kuucheza mpira wa kiwango cha juu itakayoundwa na wachezaji wengi waliopitia Kizimkazi Academy.
Na baadhi yao watakuwa na viwango vya kuuzwa nje ya mipaka ya nchi na hivyo kuiwezesha shule kuwa na heshima kimataifa.
Mawakala wenye kutambuliwa na FIFA huanza kwanza kutafuta vipaji huko Senegal na Ivory Coast wakijua kuna shule makini zenye kukuza uwezo wa vijana. Ikiweza kusimama hiyo Academy huko visiwani itakuwa ni chaguo jingine la uhakika la mawakala hao.
Rais Samia kwa vitendo amewajibu wale wadau wenye hisia za kupinga kila kitu. Walidhani ni mwanasiasa wa aina ile waliyoizoea siku zote. Anayekuwa karibu na michezo kwa nia ya kutafuta upendo ili kujirahisishia safari ya kuelekea mwakani. Kaamua kwenda mbali zaidi kwa kuacha urithi mpana wenye kuonekana kwa kujenga shule maalum ya vipaji.
Ni jukumu la wadau wa huko Zanzibar kuhakikisha shule inadumu kwa miaka mingi. Weledi ni muhimu sana katika safari nzima ya Kizimkazi Academy. Timesmajiraonline
y.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025