Na Mwandishi Wetu
MFANYABIASHARA Msiniege Mwakatumbula (56) Mkazi wa Bunju jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Katika kesi hiyo, Mwakatumbula anakabiliwa na mashtaka mawili, likiwemo la kukutwa akifanya biashara ya madini isivyo halali mali Serikali, huku shtaka la pili likiwa ni utakatishaji fedha. Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yanayomkabili jana.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon, ilidai kuwa, Machi Mosi, 2020 huu maeneo ya Bunju B Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Mwakatumbula alikutwa akifanya biashara ya madini isivyo halali.
Alitaja madini hayo kuwa ni Rubi, Corundum, Hessonite, Sapphirenuts, Moonstones, Garnet na Beryl yakiwa na uzito A gramu 6451. 80.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Vicky Mwaikambo, Simon ilidai kuwa madini hayo yana thamaninya USD 2,950.73 ambayo ni sawa na sh. 6,791,518.20 mali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuwa na kibali.
Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa siku na mahali hapo mshtakiwa huyo alijihusisha na biashara ya madini hayo mali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kujipatia kiasi hicho wakati akijua ama alitakiwa kujua kuwa madini hayo ni zao la kosa tangulizi la kosa la uchimbaji wa madini bila kufuata sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu mashtaka mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana.
Kwa mujibu wa upande wa Mashtaka, upelelezi katika kesi hiyo uko katika hatua za mwisho. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 4, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa. Mshtakiwa alirudishwa rumande.
More Stories
Watumishi wa Mahakama waonywa
CCM ilivyotambua mchango wa wanahabari Mkutano Mkuu Maalum
Wasira :Uamuzi Mkutano Mkuu umezingatia katiba