*Msigano kiwizara waibuliwa
Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline
MEI 31 kila mwaka dunia inaadhimisha Siku kupinga matumizi ya tumbaku kutokana na zao hilo pamoja na bidhaa zake kuwa na athari nyingi za kiafywa kwa rika zote kwa watumiaji na hata wasiotumia.
Wataalamu wa afya wanaonya kuwa wale wanaokuwa karibu, au kufikiwa na moshi wa sigara au shisha, wanakuwa katika hatari ya kuathirika zaidi kuliko wavutaji.
Tumbaku imekuwa ndiyo chanzo cha Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) kwa jamii ambayo kwa sasa ni janga kuu linalosababisha vifo vingi kuliko mengine duniani.
NCD inajumuisha maradhi mbalimbali kama vile magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani, kisukari, meno, macho, matatizo sugu ya njia ya hewa, athari za akili na mengineyo ya kurithi kama vile selimundu.
Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) linaonya kwenye moja ya machapisho yake ya uelimishaji kuwa moshi wa sigara, shisha na hata ugoro ni chanzo cha NCD.
Kwa Tanzania, TANCDA inasema kuwa NCD inasababisha asilimia 27 ya vifo vyote ambapo tafiti za mwaka 2012 zinaonesha kwa kila watu 100, wenye miaka 25 na kuendelea, tisa wana kisukari na 26 wana shinikizo la damu.
Katika kuadhimisha siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani, hapa nchini wadau mbalimbali wamekusanyika na kujadili mambo mbalimbali kupitia kipindi cha ‘Malumbano ya hoja’ kinachorushwa na kituo cha televisheni hapa nchini cha ITV.
Zaidi ya watu 20 wameshiriki katika mjadala huo uliorushwa mbashara na kituo hicho na kuwajumuisha wataalamu wa afya, wanasheria, wanaharakati na serikali kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini (TMDA).
Washiriki kwenye meza kuu ni Ofisa Mkaguzi na Vifaa Tiba na bidhaa za Tumbaku kutoka TMDA, Jafari Mtoro, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku Tanzania (TTCF), Lutigard Kagaruki na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Francis Furia.
Wengine ni Daktari wa Magonjwa ya Mfumo wa Upumuaji kutoka MNH, Dkt. Mwanaada Kilima na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Anna Henga.
Mada inayojadiliwa ni nini kifanyike ili kuzuia vijana na watoto kurubuniwa na kampuni za tumbaku nchini.
Kagaruki anasema hoja hiyo inatokana na kaluli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ambayo inatokana na ukweli kwamba vijana wengi wanashawishiwa kutumia tumbaku kupitia vitu mbalimbali kama vile sigara za kielektroniki na shisha.
Anaelezea maadhimisho hayo ya kila mwaka yamekuwa yakitumika katika kuishutua dunia dhidi ya janga la tumbaku ambalo limekuwa ni chanzo ya vifo na athari za kijamii.
“Sote tunajua tumbaku ni chanzo kikubwa cha magonjwa ya moyo, saratani, kisukari na matatizo sugu ya njia ya hewa,” anasema.
Anasema kuwa urubuni wa kampuni ili kuongeza watumiaji wa tumbaku unafanyika kwa kushawishi watoto na vijana kuwa waraibu wa tumbaku kwa njia mbalimbali zikiwamo za kuweka vionjo vya kuvutia kwenye shisha na sigara za kielektroniki.
Anasema hali hiyo imesababisha kwa sasa watoto na vijana wengi kujiingiza katika matumizi ya tumbaku zaidi ya watu wazima.
Ni hali anayosema itasababisha kizazi kijacho kiwe cha watu wanaotumia tumbaku zaidi kuliko cha sasa na kuashiria kuwa janga la NCD litaongezeka kwa kiwango cha kutisha.
“Tunatoa tahadhari, kama hakutakuwa na hatua madhubuti, kwa kiwango cha kasi hii ya vijana wanaovuta sigara za kielektoniki, shisha na vitu vingine vipya vya ushawishi vinavyutumika, miaka mitano, kumi ijayo, hali itakuwa ya kutisha.
“Maana hospitali ya Ocean Road (Taasisi ya Saratani – ORCI), (Taasisi ya) Jakaya Kikwete; (JKCI) na hospitali nyingine, kwenye kliniki za kisukari, shinikizo la damu na saratani, kutakuwa hakutoshi kwa mrundikano wa wagonjwa,” anaonya Kagaruki.
Kinachokwamisha Tanzania kupiga hatua ya kudhibiti tumbaku na bidha zake, anasema, ni kukosekana kwa sheria madhubuti inayodhibiti hali hiyo.
Anasema hali hii ni tofauti na nchi jirani kama vile Kenya na Uganda ambako sheria inailinda jamii dhidi ya janga hilo.
Profesa Furia anasema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 80 ya watumiaji wa bidhaa za tumbaku walianza wakiwa wadogo.
Anaonya kuwa kinamama wajawazito wanapaswa kuchukua tahadhari wasitumie au wasikae karibu na watumiaji wa tumbaku kwa sababu itaweza kuwaathiri kwa kiwango kikubwa.
Madhara wanayoweza kupata, anayataja ni kujifungua kabla ya wakati watoto wenye uzito pungufu hivyo kulazimiaka kabaki hospitalini miezi mitatu na vichanga vinakuwa hatarini kuugua magonjwa ya mfumo wa hewa.
Profesa Furia anasema bidhaa za tumbaku zimo za aina mbalimbali kama vile kuvuta, kubuya na kutafuna.
Anafafanua kuwa kinababa wanaotumia tumbaku, licha ya kuwasababishia uraibu wa kutumia tumbaku watoto wao, anawaweka hatarini kupata saratani.
Anasema jambo ambalo watu wasiotumia tumbaku hawalifahamu ni kukaa karibu na watumiaji.
Anatoa mfano wale wanokaa karibu na wavutaji au watumia shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 100.
Anasema hali hiyo kwa sasa inasababisha watoto wengi wanaozaliwa MNH kabla ya wakati na wengi wao wana uzito wa chini kupita kiasi.
Hatua za kuokoa watoto, vijana dhidi ya urubuni
Mtoro anasema TMDA inafanya ukaguzi ili kuhakikisha inasimamia sheria inayotoa makatazo dhidi ya matumizi ya tumbaku nchini.
“Kwa mfano sheria inakataza watoto kutumia tumbaku, kununua dukani au muuzaji kuwauzia. Inakataza kuuzwa maeneo yote ya shule au au ya umma,” anasema akionya:
“Wale wanaowatuma watoto dukani kununua sigara wajue wanavunja sheria. Inakataza pia watu kuvuta karibu na watu wengine.”
Hata hivyo, Mtoro anakiri hawajawahi kumkamata mtu yeyote na kumchukulia hatua ingawa kwenye ukaguzi wanawakuta watu wengi wakiwa kinyume na sheria.
“Siku ikifika tutaanza kukamata na kuchukua hatua kali lakini kwa sasa nguvu tumeielekeza katika kuelimisha ili waache wenyewe,” anasema Mtoro.
Mtoro anasema TMDA inachofanya ni kusimamia sheria zilizopo na iwapo zitabadilishwa nao watafanya vivyo hivyo.
Kuhusu kilimo cha tumbaku anasema ni suala la kisera na TMDA haiwezi kulizungumzia kwa kuwa lipo nje ya uwezo wake.
Dkt. Henga anasema tatizo la sheria za Tanzania katika kudhibiti tumbaku pamoja na bidhaa zake ni kutoendana na mkataba wa kimataifa ambao nchi imeridhia.
“Sheria za Tanzania hazijatekeleza mpango mahususi ndani ya ule mkataba. Hivyo sheria zilizopo hazitoshelezi kuilinda jamii, hususani vijana na Watoto,” anasema Dkt. Henga.
Anasema kwa mfano bidhaa za tumbaku zinapaswa kuwekewa kodi kubwa ili kuwakatisha tamaa watu wasitumie.
“Mfano kama pakiti ya sigara itauzwa Sh. 100,000, wengi hawatatumia,” anasema na kuongeza promosheni za bidhaa hizi ni kubwa na ni kinyume na mkataba, akifafanua:
“Unakuta matangazo yanawavuta watoto kuvuta kutokana na kuuzwa zikiwa na maneno yanayoonekana kwa ukubwa yakisema ‘ni freshi nia poa’ huku maelelezo yanayohusu tahadhari yakiwa kwenye maandishi madogo ambayo hayaonekani vizuri.”
Dkt. Kilima anasema baada ya kuona watoto wengi wanaathirika na tumbaku, amekuwa mdau wa kuelimisha jamii.
Anasema watoto wengi wanaathirika mapafu na njia ya mfumo wa hewa hivyo akataka jamii ichukue hatua za haraka kudhibiti hali hiyo.
Akichangia mada, Juma Dubizeti ambaye ni muelimishaji wa vijana anasema hatua ni kuhakikisha kumbi za starehe zinakuwa na maeneo maalumu ya kuvutia na siyo uholela kama ilivyo sasa na hatu zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Mwanaharakati wa kupinga matumizi ya tumbaku, Godi Lazaro anasema shida ipo kwenye serikali kwa sababu ndiyo inayotoa vibali kwa kampuni za bidhaa za tumbaku na wanaruhusu uuzaji na utumiaji holela.
Miongoni mwa hoja zilizoibuliwa kwenye malumbano hayo ni juu ya serikali kuendelea kuhimiza kilimo cha tumbaku wakati inajua wazi ni hatari kwa mazingira na afya za watu wake.
Fraide Yachite anasema kosa la serikali ni kuruhusu kilimo cha tumbaku ambacho kinauwa huku upande mwingine inakataza watu wasivute.
Malumbano hayo yalionesha wizara za serikali zinasigana na kusababisha hali ya sintofahamu kwa jamii.
Wakati wizara ya afya inasema tumbaku ni hatari kwa afya, wizara ya kilimo inasema tumbaku inaliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.
Kwa upande wa wizara ya viwanda inawawaruhusu wawekezaji wa bidhaa za tumbaku, wizara ya sheria nayo inashindwa kutekeleza mikataba ambayo serikali imesaini kwa hofu ya kusigana na sera za nchi.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa njia sahihi ya kutatua tatizo ni viongozi wa serikali kuwa na dhamira sahihi pamoja na utashi wa kisiasa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku nchini.
Udhibiti huo ni lazima ufanyike kwa sheria za nchi ziendane na mkataba wa kimataifa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambao Tanzania iliusaini ili utekelezwe kikamilifu nchini.
More Stories
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa
Utashi wa Rais Samia na matokeo ya kujivunia vita dawa za kulevya nchini
Uwekezaji wa Rais Samia sekta ya afya waendelea kuwa lulu Afrika